TPDC:Asilimia 62 ya umeme nchini inatokana na gesi asilia

NA DIRAMAKINI 

SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema asilimia 62 ya umeme nchini unatokana na gesi asilia huku kiasi kinachobakia kama asilimia 20 kinatumika katika maeneo ya majumbani na kwenye magari.
Hayo yameelezwa na Mkurungezi Mtendaji wa TPDC, Dkt.James Mataragio wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara maarufu Sabasaba yanayoendelea kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam. 

Amesema, kwa sasa wanajenga miundombinu mbalimbali itakayosaidia kusambaza gesi majumbani, vyuoni na kwenye magari.

“Tuna mpango wa kujenga vituo vitano vya gesi ambavyo vitakuwa katika maeneo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Feri, Muhimbili, Kibaha na Ubungo, vituo hivi tunategemea vitakamilika mwakani mwezi Machi. Vitakuwa ni moja ya vichocheo vya upatikanaji wa gesi asilia katika magari na majumbani,”amesema.

Vilevile amesema kiasi cha gesi asilia kilichogunduliwa mpaka sasa ni futi za ujazo trilioni 57.5 huku kiasi kikubwa kikiwa baharini.

Amesema, kiasi kikubwa cha gesi ambacho kipo baharini kinatarajiwa kuvunwa kupitia mtambo wa Kuchakata Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG) unaotarajiwa kujengwa nchini huku gesi itakayopatikana itasafirishwa kwenda kuuzwa kwenye masoko nje ya nchi na nyingine kubaki nchini kwa ajili ya soko la ndani.

Aidha, alizitaka sekta binafsi kujitokeza kwa wingi kujenga vituo vidogo vidogo vya gesi asilia ili kurahisisha upatikanaji wa bidhaa hiyo kwa wananchi.

"Watanzania watarajie makubwa juu ya uwepo wa gesi, tutanataka kuhakikisha magari yanafaidika kutumia gesi, hata hivyo gesi hii iliyogundulika huku baharini tunataka iwanufaishe wananchi kwa kiasi kikubwa na serikali kupata mapato kupitia fedha za kigeni pindi tutakapoanza kuiuza nje ya nchi,”amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news