'CRDB Bank Instaprenyua' kufanyika Julai 16

NA DIRAMAKINI

KATTIKA kuendeleza jitihada zake za kuwajengea uwezo na kuwawezesha wajasiriamali vijana nchini, Benki ya CRDB imetangaza kuandaa semina maalum iliyopewa jina la “CRDB Bank Instaprenyua”, itakayofanyika Julai 16,2022 Makao Makuu ya benki hiyo, kwa ajili ya kuwawezesha vijana ambao wanafanyabishara kupitia mitandao ya kijamii. 
Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Benki ya CRDB, Joseline Kamuhanda akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu Semina kwa wajasiriamali wanaofanya Biashara ya Mtandao “CRDB Bank Instaprenyua” inayotarajia kufanyika Julai 16,2022 katika Makao Makuu ya Benki hiyo. Wengine pichani, ni Kaimu Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na Wakati, Bonaventura Paul (wapili kulia), Afisa Mauzo wa Silent Ocean, Dotto Mayanga, wapili Kushoto, Meneja Mahusiano Infucus Studio Ltd, Clair Mtui na Operesheni Meneja Simba courier, James Mwambona. Mkutano huo na waandishi wa habari ulifanyika katika Tawi la Benki ya CRDB lililopo katika Viwaja vya SabaSaba Jijini Dar es salaam. 

Mkuu wa Kitengo cha Masoko cha Benki ya CRDB, Joseline Kamuhanda ameyasema hayo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika mkutano huo, Joseline alisema katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na mwamko mkubwa kwa vijana kujishughulisha na shughuli za ujasiriamali hususani kupitia mitandao ya kijamii ambayo imerahisha namna ya kuendesha biashara, na kuyafikia masoko kwa urahisi. 

“Vijana wamekuwa wakitumia vizuri fursa zilizopo hususani fursa za mitandao ya kijamii kufanikisha shughuli zao za ujasiriamali. Katika maonesho haya tumewaona pia vijana wajasiriamali ambao wanafanya vizuri kupitia maduka mtandao, jambo ambalo limetusukuma kuwapa elimu na kuwajengea uwezo,” alisema Joseline. 

Joseline alisema biashara mtandao ni moja ya eneo linalokua kwa kasi, na linalopaswa kuangaliwa, ikiwa ni pamoja na kutafuta suluhu ya kuwawezesha wajasiriamali hao. Mitandao ya kijamii hususan Instagram imekuwa chachu kubwa kwa vijana wajasiriamali hapa nchini kuishi ndoto zao za ujasiriamali. 

Takwimu zinaonyesha Instagram ndio mtandao wa kijamii wenye watumiaaji wengi zaidi duniani, bilioni 1.074, vivyo hivyo hapa Tanzania, mtandao huo unaongoza pia ndio unaongoza kwa wafuasi zaidi ya milioni 2.86. “Hii ndio sababu ya kuipa jina la Instaprenyua semina hii kwani ndipo hasa vijana wengi wapo, lakini lengo ni kuwafikia vijana katika majukwaa yote ya mtandaoni,” aliongezea. 

Akizungumzia kuhusu malengo ya kuandaa semina hiyo, Mkuu huyo wa Kitengo cha Masoko alisema Semina hiyo ina malengo makuu matano ikiwamo; kutoa mafunzo ya namna bora ya kuendesha biashara kwa wajasiliamali wanaofanya biashara mtandao, na kutoa elimu ya usimamizi wa fedha katika biashara. 

Malengo mengine ni pamoja na elimu ya masoko ya fedha na mitaji, na namna bora za kuyaendea masoko hayo, elimu juu ya fursa zinazotolewa na Benki ya CRDB kwa wajasiriamali nchini, pamoja na elimu ya urasimishaji wa biashara, na faida zake kwa wajasiriamali. 

Benki ya CRDB pia iliutumia mkutano huo na waandishi wa habari kuwashukuru washiriki wote wa maonesho, wafanyabiashara, taasisi, makampuni na wateja binafsi, ya sabasaba kwa kuendelea kuichagua benki hiyo kuwa mtoa huduma. 

Akitoa salamu hizo za shukrani, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wateja Wadogo na Wakati Benki ya CRDB, Bonaventure Paul alisema msimu wa sabasaba wa mwaka huu umekuwa na mafanikio zaidi ambapo benki hiyo imeweza kuboresha huduma zake kwa wateja na kuweza kuwahudumia wateja wengi zaidi kupitia tawi maalum la benki lililopo katika viwanja vya sabasaba pamoja na CRDB Wakala.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news