Fahamu kilichojiri Kambi ya Kifo ya Sobibor ya Kijerumani nchini Poland 1942

NA CHARLES REGASIAN

BAADA ya utoro wa wafungwa Nazi wakabomoa kambi ya Sobibor na kupanda miti ya misonobari ili kuficha ushahidi.

Eneo hilo likaachwa kwa muongo mmoja baada ya Vita ya Pili ya Dunia,hata kambi yenyewe hapo awali haikuwa maarufu kama ni kambi ya kuteketeza Wayahudi.

Ilikuja kufahamika zaidi baada ya kuoneshwa kwenye kipindi cha mauaji katika televisheni ya Marekani mwaka 1978, na filamu ya "Escape from Sobibor" ya Uingereza ya mwaka 1987.
Pichani ni lililokuwa geti kuu la kuingilia ndani ya kambi ya mauaji ya Wayahudi Sobibor nchini Poland limeandikwa SS SONDERKOMMANDO.

Baada ya anguko la Umoja wa Kisovieti, makumbusho ya Sobibor yalifunguliwa eneo ilipokuwa kambi ya Sobibor na wanaikolojia wakaanza kufukua ili kujua historia ya eneo hilo hadi sasa. Picha ya kwanza ikatoka ikionesha operesheni yake kama sehemu ya uhalifu.

SOBIBOR ilikuwa moja ya kambi tano za mauaji iliyoanzishwa kama sehemu ya operesheni Reinhard,mauaji ya Wayahudi wa ulaya hayakuasisiwa kama malengo ya ghafla bali yalianza kidogo kidogo kulingana na eneo lililoteuliwa.

Kufuatia uvamizi wa nchi ya Poland wa Septemba 1939, Wajerumani walianza kukamilisha mpango wa Nisko ambapo Wayahudi walitoroshwa kutoka katika makazi yao Ulaya kote na kupelekwa katika kazi za surubu ikijumuishwa hifadhi ya Lublin iliyopo Wilaya ya mji wa Lublin, ilichaguliwa kwa sababu ya eneo hilo kutofahamika kwa watu wengi.

Mpango huo wa Nisko, ukaahirishwa mwaka1940 lakini vibarua waliendelea na operesheni katika maeneo hayo yakiwemo, Trawniki,Lipowa,na Sorohucza.

Mwaka 1941 NAZI ya Hitler walianza utafiti juu ya kuwaua Wayahudi kwa gesi, Hitler aliongoza utawala wa NAZI katika kuteketeza vichwa vya Wayahudi milioni 6 ambao yeye aliwaita magugu katikati ya wanadamu,alikusudia kuangamiza kizazi chote cha Kiyahudi katika uso wa dunia,yote yalianza baada ya kuamrisha.

Ilipofika Desemba mwaka 1941 utawala wa NAZI huko Chelmo ulianzisha utafiti ukitumia magari ya gesi na mauaji ya halaiki kwa kutumia gesi yalitekelezwa katika kambi ya Auschwitz, mwezi Januari huko kwenye Mkutano wa Wansee wa Januari 20 mwaka 1942, Reinhard Heydrich alitangaza mpango wa kisayansi wa kuwaua Wayahudi kwa kupitia mtandao wa kambi za mauaji,mpango huo uliitwa operesheni Reinhard.

Hakuna kinachofahamika kuhusiana na mkakati wa mwanzo wa Sobibor, wanahistoria wachache walibashiri kwamba mkakati huo utakuwa ulianza mapema mwaka 1940,kipindi ambacho ramani ya reli inajengwa na kutopitishwa katika miji muhimu lakini ikaelekezwa huko Sobibor na Belzec.

Ushahidi wa mwanzo ulionesha nguzo za miti zilizoonekana kipindi cha vuli mwaka 1941,ambapo maofisa wa NAZI walitafiti ardhi iliyo mkabala na stesheni ya Reli,ndipo mfanyakazi fulani wa mgahawa hapo stesheni alipomuuliza ofisa mmoja wa NAZI,nini kinachojengwa? Na yeye akajibiwa kuwa,atulie ataona hivi punde na kwamba kitakuwa ni kicheko kizuri.

Machi mwaka 1942 ofisa wa NAZI Richard Thomalla akachukua kazi ya ujenzi wa Sobibor, ambao ulianza tarehe isiyojulikana mapema,Thomalla alikuwa mkandarasi wa zamani wa majengo na mtiifu kwa chama cha NAZI cha Hitler, akifanya kazi kama Kamanda wa polisi jamii, na mshauri juu ya vibarua wa Kiyahudi na alikuwa na cheo cha juu katika idara ya ujenzi ya Odilo Globocnik, kwa kuwa alishaona kipindi cha nyuma ujenzi wa kambi ya mauaji ya Belzec akachukua somo alilojifunza na kulipeleka Sobibor.

Thomalla akagawa eneo kubwa la Sobibor zaidi ya lile la Belzec,alijenga vyumba vingi zaidi na nafasi ya kutosha katika huduma zote za kambi.

Thomalla aliyesimamia ujenzi wa awali wa Sobibor,kambi hiyo ilijumuishwa na majengo ya toka kabla ya vita ya kwanza ya dunia yakiwemo ofisi za Posta,Loji ya misitu,Mnara wa misitu na Kanisa dogo, Loji ya misitu ikaja kuwa jengo la utawala ambapo ofisi ya Posta ilitumika kama Loji ya maofisa, ofisi hiyo ya Posta ya zamani ipo mpaka leo imesimama, Wajerumani wakafanya ujenzi wa Reli Mpya toka ile ya awali na kuiingiza mpaka ndani ya kambi kama mita 800 hivi, mkusanyiko huo wa Reli tatu uliwezesha safari tofauti za treni kuendelea bila kubugudhi usafiri wakati wafungwa wapya waliowasili wanapoteremka,vifaa vingine vya majengo vililetwa na ofisi ya Ujenzi ya Lublin,vingine viliagizwa kwa wapasua mbao wazawa na wafyatua tofali binafsi, na mabaki toka kwenye nyumba za Wayahudi zilizobomolewa.

Kundi la kwanza la wafungwa waliojenga Sobibor walikuwa raia wa kawaida toka vijiji vya jirani na mjini,baada ya Thomalla kuwasili Manispaa ya Wayahudi karibu na huko Wlodawa aliipa amri ya kupeleka Wayahudi 150 kusaidia ujenzi wa kambi, vibarua hao walinyanyaswa sana wakiwa kazini,na waliuawa mara ujenzi ulipokwisha lakini kuna wawili ambao walitoroka na kurudi Wlodawa ambapo walijaribu kuionya Manispaa ya Wayahudi kuhusu mpango wa kambi na madhumuni yake,maonyo yao hayakuaminiwa.

Chemba ya gesi ya kwanza Sobibor ilijengwa kufuatia mfano wa zile za kambi ya Belzec, lakini hazikuwa na tanuri, ili kutia gesi ya monoxide, Erich Fuchs alichukua injini nzito ya petroli huko Lemberg akaifungua toka kwenye kifaru.

Fuchs akaifunga injini hiyo kwenye zege hapo Sobibor mbele ya maofisa,Floss,Bauer, stangl,na Barbi na kuiunganisha ekzosi ya injini na manifoldi kuelekea kwenye mabomba mengi yanayoelekea kwenye chemba ya gesi katikati ya April mwaka 1942 NAZI wakafanya utafiti wa kisayansi wa gesi kwenye kambi Mpya.

Christian Wirth, Kamanda wa Belzec na mkaguzi wa operesheni Reinhard, alitembelea Sobibor na kushuhudia moja ya mitambo hiyo ya gesi iliyoua Wayahudi wanawake 30 hadi 40 walioletwa tokea kwenye kambi ya kazi ya Krychow kama majaribio.

Ujenzi wa awali wa Sobibor ulimalizika wakati wa kiangazi mwaka 1942, na msururu wa wafungwa ulianza kuingia kambini, japokuwa kambi iliendelea kupanuliwa na kukarabatiwa, baada ya miezi michache ya operesheni ukuta wa mbao wa chemba za gesi uliopo ulifyonza sana jasho ,mikojo, damu na kinyesi, na kutakiwa kusafishwa ,hivyo chemba za gesi hizo zikabomolewa kipindi cha kiangazi mwaka 1942 na chemba nyingine mpya zilijengwa,kwa kutumia tofali,baadae NAZI wakapanga mradi wa usafi wakaweka ratiba ya usafi wa mabweni na makambi na kupanua mandhari ya upande wa mbele ili paonekane kama kijiji cha Tyrolean.

Wakati Sobibor inasitisha operesheni zake katikati ya mwaka 1943 NAZI walikuwa mbali wanajenga ghala la silaha lililoitwa Lager IV.

Sobibor ilizungukwa na uzio wenye senyenge mbili ulioezekwa kwa miti ya aina ya misonobari yenye miiba ili kuzuia mtu asione ndani, kona ya Kaskazini kuna mageti mawili pande zote,moja la treni na lingine la watembea kwa miguu na magari,eneo liligawanywa katika viwanja vitano,upande wa mbele na Lager nne zenye namba I-IV ,kiwanja cha mbele kuna nyumba za maofisa wa NAZI wanaishi katika nyumba ndogo zenye majina yenye kuandikwa kwa maandishi ya rangi kama,Lustiger Floh (yaani ,Mbun'go mleta furaha) Schwalbennes (kiota cha ndege) na Gottes Heimat (Nyumbani kwa Mungu).

Walikuwa pia na kantini, bakuli ya bowling,kinyozi na daktari wa meno, wote ni wafungwa wa kivita wa Kiyahudi,walinzi waliletwa kama wafungwa wa kivita wa Kisovieti, walitengwa kwa kupewa kantini,saluni,majengo ya burudani.

Eneo la mbele lenye majengo ya kisasa kama (Merry flea) lilisaidia kuficha dhumuni la kambi ya Sobibor kwa wageni wapya, Wanazi walichukulia umakini sana katika muonekano wa eneo la mbele, lilikuwa safi lenye bustani,ngazi ardhi yenye kokoto na alama za rangi zilizo bora, muonekano huu ulisaidia kuficha asili ya kambi kwa wafungwa waliowasili kambini.

Lager I, inachukua makambi na karakana za wafungwa wa karakana hizo zinajumuisha duka la mafundi cherehani,seremala, magari ,mchoraji,mikate.

Lager II, ni kubwa yenye kiwanja chenye jengo la utawala,shamba dogo,jengo la utawala kabla ya vita lilitumika kwa huduma za misitu Poland, kama sehemu ya kambi jengo hili lilitumika kutoa huduma kwa maofisa wa NAZI, Bohari ya vitu vilivyoibwa kutoka kwenye mizigo ya waathirika wa gesi, Duka la dawa ambalo pia vilivyomo humo vilitoka katika mizigo ya waathirika wa gesi, shambani wafungwa Wayahudi walifuga kuku, nguruwe, mabata mzinga na mbogamboga kwa matumizi ya maofisa wa NAZI.

Mlango wa kuelekea pale Erbhof, Lager II, una vifaa ambavyo wanaowasili waliandaliwa kwa vifo vyao, eneo hilo linachukua makambi ya kuwachambua na Majengo mengine yalitumika kuhifadhi mali za wanaouawa kwa gesi, vikiwemo; nguo, chakula, nywele,dhahabu, na mali zingine ,Mashariki mwishoni kuna ua ambapo wageni na mizigo yao ilichukuliwa na walilazimishwa kuvua nguo zao na kuandika barua kuwajulisha ndugu zao kwamba wamefika salama,barua hizo ziliwasaidia maofisa wa NAZI kuwafuatilia ndugu zao hao na kuwaleta Sobibor, eneo hili lilipambwa kwa maua kuficha malengo ya kambi kwa wageni.

Ua huo unaelekea katika njia nyembamba inayoitwa Himmelstrasse,( yaani barabara ya kuelekea peponi) inaelekea moja kwa moja kwenye chemba za gesi, Lager III, barabara kuelekea peponi ilipambwa na uzio wenye matawi ya misonobari. Lager III lilikuwa eneo la mauaji lilitengwa mbali na kambi porini likizungukwa na uzio uliozibwa na miti,wafungwa waliokuwa lager I, hawakuruhusiwa kusogelea eneo hili, na waliuawa mara walipotiliwa shaka kwamba wameona ndani kinachoendelea.

Humo kuna chemba za gesi, makaburi ya halaiki na nyumba maalum zilizotengwa za wafungwa wanaofanya kazi huko bila kuwasiliana na wenzao.

Lager IV, ni eneo lililoongezwa Julai 1943 na lilikuwa chini ya ujenzi kipindi cha utoro,likiwa ni eneo lenye mbao nyingi Kaskazini mwa kambi zingine lilijengwa kwa nia ya kuwa ghala la silaha na kuhifadhi silaha zlizotekwa toka kwa askari wa Red Army.

Sababu Sobibor ilikuwa kambi ya mauaji, wafungwa walioishi pale walifikia takribani 600 ,mazingira magumu kambini yalichukua maisha mengi ya wageni kwa miezi michache tu.

Wafungwa Sobibor walifanya kazi kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa 12 jioni huku pakiwa na mapumziko machache ya chakula cha mchana saa 6 ,Jumapili ilikuwa nusu siku ya kazi,lakini sio kila siku kuna wakati ni kazi tu kama kawaida, wafungwa walikuwa ni wafanyakazi wengi wenye ujuzi maalum kama wafua dhahabu,rangi ,bustani au kushona, wafungwa hao hawakuuawa ili kusaidia shughuli za awali za kambi,kazi zao nyingi ziliwasaidia maofisa hao kuwa matajiri,wafungwa wenye ujuzi maalum waliangaliwa na walihudumiwa tofauti na wengine.

Wasiokuwa na ujuzi maalum walifanya kazi mbalimbali, wengi walifanya kazi katika Lager II Kuchambua mabweni na kulazimishwa kuchambua mizigo iliyoachwa na marehemu wa gesi ,kupakia vifaa vya thamani kama zawadi kwa Wajerumani ambao ni wahitaji, pia walitumika kule stesheni ya Reli kupokea wageni wanaowasili,kazi ya kuogofyeka ni ile ya vinyozi wa wanawake wanaoelekea kwenye chemba za gesi, kazi hii mara kwa mara walipewa vijana wadogo wafungwa wa kiume nia ni katika kujaribu kuwadhalilisha vijana hao wote pamoja na kinamama ambao kipindi hicho huwa hawana nguo zao ambao walikatwa nywele na vijana hao,walinzi wenye silaha walisimamia zoezi hilo kuhakikisha kwamba vinyozi hawawasiliani kitu au kuwatahadharisha wageni hao.

Kule Lager II, palikuwa na kitengo maalum cha wafungwa wayahudi waliolazimishwa kusaidia zoezi la mauaji,kazi zao zilikuwa kuiondoa miili, kuondoa damu na vinyesi kwenye chemba za gesi na kuchoma mizoga ,sababu wafungwa walio katika kitengo hiki walishuhudia mauaji ya halaiki walitengwa vikali na wengine ,na maofisa wa NAZI mara nyingi waliwapiga risasi wote walioshindwa kufanyakazi pia hakuna waliopona katika eneo hili kwa hofu ya kutoa siri au kuwa mashahidi siku za mbele.

Wakati Lager IV inaanza ujenzi wake mwaka 1943,wanazi waliwaweka makomandoo msituni waliofanya kazi ya kukata magogo kwa ajili ya joto, kupikia na kuchomea watu, kwa sababu walijua kinachofuatia ni kifo wafungwa mara nyingi walikuwa wakilia na jioni wote walijifanyia mambo yaliyobakia katika maisha yao, waliimba na kucheza jioni, na mahusiano ya mapenzi yalishamiri sana kama njia ya kujiliwaza.

Baadhi vya mapenzi yalikuwa ya kulazimishwa au biashara hasa wale waliokati ya wafungwa wa kike na manyapara, na wengine walikuwa na mapenzi ya ukweli kwa sababu wapo ambao baada ya vita waliooana,maofisa walifurahia sana mahusiano haya,pia waliwafundisha kuimba kwaya kwa vitisho,wafungwa wengi walitafsiri hii kama njia ya kuwaweka wafungwa katika udhibiti na kuwazuia wasifikirie kutoroka.

Wafungwa walipewa amri kulingana na umuhimu wao, waligawanyika katika sehemu tatu,wale waliotumika na kutupwa wakati wowote hawa walitegemea huruma ya maofisa, wale wenye upendeleo ambao kazi zao maalum zinatoa faraja kubwa, na wengine wale wasanii wenye elimu maalum inayowafanya wawe muhimu na kupewa huduma mahsusi.

Kambi zingine Nazi waliteua nyapara wa kuwapanga wafungwa wenzao katika mstari, nyapara alifanya kazi zake za kusimamia kazi shughuli na kutekeleza amri zake kwa mjeledi,waliteuliwa bila ridhaa yao na walitofautishwa kimaeneo kwa jinsi walivyoitikia shinikizo la kisaikolojia la sehemu zao.

Nyapara Moses Sturm alipewa jina la utani "Mad Moisz" kutokana na kuwa na hasira za ajabu,alipiga wafungwa kiasi cha kutisha bila mazungumzo na mtu lakini baadae aliomba msamaha daima,alikuwa akiongelea suala la utoro.

Wakati mwingine aliwagombeza kwa kiasi bila kupinga wakati mwingine kufanya mipango inayowezesha kutekelezwa kwa mambo muhimu ya wayahudi,Sturm aliuawa baada ya kusalitiwa na nyapara mdogo, Herbert Naftaniel, Naftaniel akapewa jina la utani "Berliner" akawa ni mwiba kambini alijiona ni Mjerumani badala ya myahudi akaanza kuongoza kwa vitisho, lakini muda mfupi utoro ulipotokea kundi la wafungwa lilimpiga hadi kifo kwa ruhusa ya ofisa Karl Frenzel.

Mbali na mgawanyiko huo kambini,wafungwa walipata njia zao za kuwasaidia wagonjwa na majeruhi walipewa chakula kwa siri, dawa na vifaa vya afya vilivyoibwa katika duka la dawa kambini,wafungwa wenye afya walitegemewa kuchukua nafasi za wagonjwa ambao pengine wangeuawa.

Nesi wa kambini Kurt Ticho aliendeleza mbinu za kupotosha rekodi zake ili wafungwa wagonjwa waongeze zaidi siku tatu za kupona zilizowekwa na utawala,wapokea wageni stesheni ya Reli walijaribu kuwaonya wageni wanaowasili kuhusu ujio wa vifo vyao, lakini walikutana na kutoaminiwa na wageni hao.

Jambo lililofanikiwa zaidi lenye umoja pale kambini lilikuwa ni utoro wa Oktoba 14 mwaka 1943, ambao ulipangwa kiasi kwamba wafungwa wote kambini wangepata nafasi ya kutoroka.

Wafungwa walikumbwa na tatizo la kukosa usingizi,utapiamlo,kuongezeka kwa kazi, na vipigo,chawa, ugonjwa wa ngozi, na maradhi ya kupumua yalikuwa ni kawaida,ugonjwa wa homa ya matumbo uliitesa kambi ya Sobibor, wakati Sobibor inafunguliwa kwa mara ya kwanza wafungwa walionekana ni wa kupita tu, na kuuawa mara walipoonyesha alama ya kuumwa au kupata jeraha.

Baada ya miezi michache tu maofisa walitambua kuna wimbi kubwa la vifo na kupungua uwezo wa kambi kujiendesha, maofisa wakaweka amri ya kuwaruhusu wafungwa kupona ndani ya siku tatu tu, wale walioshindwa kupona ndani ya siku tatu na kushindwa kufanya kazi walipigwa risasi.

Chakula kambini hakikutosha ,kama vile tu kambi za wilaya ya Lublin, wafungwa walipewa gramu 200 tu ya mkate kama kifungua kinywa kwa kahawa ,cha mchana kilikuwa ni supu chache na viazi au nyama ya farasi,cha jioni kinaweza kuwa kahawa, wafungwa walilazimishwa kuishi katika mlo huo na kusababisha afya zao kubadilika kutokana na njaa, wengine walijiongeza kwa kuvizia chakula toka katika mizigo ya waathirika wa gesi au wanapofanya kazi huko makambini au stesheni ya Reli, biashara ya bidhaa (Barter trade) ilifanyika sana kambini.

Mfano wafungwa walibasilishana almasi kwa pesa,baada ya kuchambua mizigo makambini,pia walipata chakula baada ya kubadilishana na pombe toka katika mizigo ya wageni.

Wafungwa wengi hawakupata huduma ya afya na usafi wa mazingira,hawakuoga huko katika maeneo ya Lager I, na maji safi yalikuwa ni adimu,ingawa nguo ziliweza kufuliwa au kubadilishwa baada ya kuchambua za makambini,kambi ilishambuliwa na wadudu, baadhi ya wafungwa wa kufua nguo na kupiga pasi walikuwa na unafuu.

Sobibor ilijazwa na kundi linalozunguka la maofisa Wajerumani 18 hadi 22 wakiwemo wa Austria ,maofisa hao kwa ujumla ni wale wa tabaka la kati chini, ambao nyuma walifanya kazi za wafanyabiashara, wasanii, wakulima,manesi, na mapolisi, Karibu maofisa wote hapo awali walitumika huko Aktion T4, mpango wa uhamasishaji wa jeshi la Nazi,wengi walihudumu katika kituo cha uhamasishaji cha Hartheim.

Mengi yaliyofanywa kituo cha Hartheim yaliendelea kutekelezwa Sobibor,ikiwemo kuwadanganya waathiriwa njiani kuelekea chemba za gesi, kabla hawajaanza kufanya kazi Sobibor pamoja walikutana na Odilo Globocnic huko Lublin kusaini makubaliano ya Siri juu ya kozi ya operesheni, takribani maofisa wa NAZI 100 walihudumu Sobibor.

Wakati Sobibor inaanza kufunguliwa kamanda wake alikuwa ni Franz Strangl,mratibu jasiri aliyefanya kazi ya kuongeza ufanisi wa mchakato wa mauaji,Strangl hakuwa na muingiliano na wafungwa alikuwa daima na tabasamu usoni mwake,akahamishiwa kambi ya Treblinka Agosti 19, mwaka 1942 na nafasi yake ikaja kujazwa na Franz Reichleitner, Reichleitner alikuwa mtu wa kinywaji sana asiye Msemiti, asiyezingatia sana kinachoendelea kambini zaidi ya mchakato wa mauaji katika chemba za gesi, Afisa F├╝hrer Johann Niemann, alihudumu kama kaimu kamanda wa Sobibor.

Operesheni za kila siku kwa ujumla zilisimamiwa na Kamanda,Gustav Wagner, mtu aliyeogopwa na kuchukiwa zaidi ya wote pale Sobibor, wafungwa walimsema kuwa ni katili,asiyetabirika,mwangalifu,mhitaji uangalifu, na mkimya, walimwita kwa jina la " Mnyama na mbwa mwitu",aliyeripoti kwa Wagner alikuwa ni Karl Frenzel.

Na aliyesimamia Lager I na kutenda kama mwanasheria wa kambi,Kurt Bolender na de Hubert Gomerki walisimamia Lager II eneo la mauaji,wakati Erich Bauer aliratibu uchomaji gesi yeye mwenyewe.

Maofisa hao walivutiwa na kazi zao, pale Sobibor waliweza kufurahia starehe ambazo hazipo kwa askari wanaopigana huko Mashariki, maeneo ya maofisa hao yana Kantini, Saluni,Klabu, n.k kila ofisa wa NAZI aliruhusiwa kwenda likizo ya wiki tatu, kila baada ya miezi mitatu, ambapo wangeweza kula bata huko Haus Jchoberstein mapumzikoni kwa sababu kila ofisa alilipwa pesa ndefu sana,kiasi cha Reichmarks 58 ,pia palikuwa na posho ya kila siku ya Marks 18 na bonasi maalum ya nyongeza ya mauaji ya wayahudi ,kila ofisa Sobibor alikusanya pesa kiasi cha Marks 600,pesa ndefu kwa miaka hiyo, kwa kila mwezi,pia walilipwa posho ya usumbufu, kazi ya Sobibor ilitoa ofa ya fursa zisizokuwa na mwisho kwa maofisa wake, ikiwemo kujitajirisha kwa kuwakandamiza wafungwa na kuwaibia mali zao wale waliouawa katika chemba za gesi.

SOBIBOR ililindwa na takribani walinzi 400,waathirika wa gesi mara nyingi waliwaita "Blackies" weusi, askari au waukrania,hawa walikamatwa kama wafungwa wa kivita na Nazi, walinzi hao walitarajiwa kusimamia maelekezo ya kazi na kuwasimamia wafungwa ikiwemo kuwapa adhabu na kuwaua.

Pia kushiriki mchakato wa mauaji katika chemba za gesi, kuwashusha na kuwasindikiza waathirika kwenye chemba za gesi,walinzi hao walivaa mchanganyiko huku wakifanana na vipande vya unifomu ya NAZI,Kisovieti na Poland, mara nyingi zenye rangi nyeusi na ndio maana waliwaita "Blackies" hawa walilipwa pesa na posho sawa na zile za wale waffen ikiwemo posho ya familia na likizo za mapumziko, ingawa walinzi walikuwa wanawaogopesha wafungwa, uaminifu wao Kwa maofisa wa NAZI haukuwa mzuri sana walifanya biashara ya kubadilishana vitu kimya kimya kama wafungwa na walipiga sana mtindi (pombe) pamoja na kukatazwa tabia hiyo, maofisa hawakuwaamini walinzi na waliwadhibiti kuzifikia silaha.

Walihamishwa mara kwa mara kati ya kambi tofauti ili kuwazuia kujenga ufahamu au mawasiliano na wananchi majirani,baada ya wafungwa kuanzisha mgogoro maofisa wa NAZI waliogopa walinzi nao wangefanya utoro, hivyo waliwarudisha huko Trawniki chini ya ulinzi lakini uoga wao ulithibitika kwani wallnzi waliua wasindikizaji hao na kutokomea porini.

Wafungwa waliadhibiwa kwa makosa madogo madogo mfano kuvuta sigara, kupumzika wakati wa kazi, kuonyesha ukaidi wakati wa kuimba, adhabu zilikuwa sio kutekeleza sheria za kambi bali hata kwa ajili ya vikwazo binafsi vya walinzi hata katika Kutaka mapenzi kinguvu.

Adhabu, maarufu Sobibor iliyotolewa na walinzi Ilikuwa ni kuruka kichurachura,maofisa walibeba mijeledi ya ngozi yenye urefu wa sm 80 iliyotengenezwa na wafungwa kutokana na mizigo ya waliouawa katika gesi, adhabu ya kichurachura ilipomjeruhi sana mfungwa alibadilishiwa adhabu na kupewa ya kifo cha risasi, maofisa waliwataka wafungwa waimbe wakiwa kazini au wanapotembea,hata wakati wa mauaji ya watu wengi, au walipiganishwa kama majogoo, huku maofisa wakitazama na kufurahia huku mikono yao ikiwa imefungwa kwa nyuma na kamba ngumu, mfano ;waliambiwa waimbe nyimbo.

"Mimi ni Myahudi mwenye pua kubwa" wafungwa wa kike walifanyiwa ukatili wa kijinsia katika matukio kadhaa, mfano; Waustria wawili wa kike,Ruth na Gisela walifungiwa makambini na kubakwa na maofisa Kurt Bolender na Gustav Wagner.

Ofisa Joham Klier alikuwa wa kipekee na mwenye utu, hata wafungwa kadhaa Walitoa ushuhuda kuwa hawakuelewa kwanini alikuwa pale Sobibor, wafungwa waliwaona walinzi ni katili zaidi kuliko maofisa wa NAZI, ingawa baadhi ya walinzi walikuwa na huruma kwa wayahudi ,wakiwapa kazi za kiasi na kuwasaidia kutoroka ,kuna siku walinzi wawili ,Victor Kisiljow, na Wasyl Zischer, walitoroka pamoja na wafungwa wawili Lakini walishikwa na kupigwa risasi.

Wafungwa walijitahidi kuzoeana na watesaji wao ili kupunguza ukatili wao uliopitiliza ,walijaribu kuwasifia au kujipendekeza ,mfano kuimba nyimbo za asili za kijerumani , au pale ofisa Karl Frenzel ,alipompenda Saartje Wijnberg, daima alitabasamu kwake na kumchekea au kumtaniatania na kumwita mchumba, Frenzel alimlinda wijnberg asipewe kazi ngumu na Wakati mwingine kumtetea anapokuwa mgonjwa makambini.

Mara tu treni inapowasili Sobibor wayahudi hawakujua, walielewa wapo katika kambi na wanaendelea na safari ,walilazimishwa kukabidhi mali zao zote na kutenganishwa kutokana na jinsia, na kuelezwa kuvua nguo ,wanawake wasio na nguo walichanganywa na wasichana, waliona aibu sana, walikutana na Wafanyakazi Vijana wayahudi waliowanyoa nywele zao kwa sekunde chache ,kati yao ni kinyozi ,Toiri Blatt, (miaka 15) wafungwa hao walipangwa kwa makundi na kuelekea barabara yenye urefu wa m 100 (barabara ya kwenda peponi) huko waliuawa kwa gesi ya Carbon monoxide iliyotoka katika Eksozi ya mabomba ya matenki ya injini.

Kabla wayahudi hawajauawa ofisa Hermann Michel aliwatolea hotuba ,Michel alivalia koti jeupe kama mfizikia ,Michel aliwaeleza kuwa watapelekwa kufanya kazi lakini kabla ya hapo wanapaswa kuoga, na kuzuia maambukizi ili kuzuia kuenea kwa magonjwa ,Baada ya kuvua nguo wayahudi walichukuliwa na kupelekwa kupitia tyubu huku ofisa akiongoza njia mbele, huku waukrania sita au watano wakiwa nyuma yao wakiwahamasisha kuwahi kwa nyuma.

Baada ya kuingia katika chumba cha gesi wale waukrania wanafunga ghafla milango ,Mota ya injini iiliwashwa na askari msovieti,Emil Konstebo, na dereva mjerumani, Erich Bauer ,toka Berlin baada ya kuwachoma gesi milango inafunguliwa na mizoga inaondolewa na Wanachama wa Sonderkomando.

Baada ya mauaji katika chemba za gesi mizoga ilikusanywa na sonderkomando na kupelekwa katika makaburi ya halaiki au kuchomwa moto ,mashimo ya makaburi yalifikia urefu wa m 50-60(futi 160-120) ,upana m10-15(futi 30-50) ,urefu m5-7(futi15-20) pakiwa na ukuta wa mchanga ili kurahisisha uzikaji wa mizoga hiyo.

Kati ya wayahudi 170,000 na 25,000 waliuawa Sobibor kiwango hiki kilitolewa mwaka 1947 na jaji wa Poland ,Zbigniew Lukaszewics, aliyewahoji waathirika, watu wa relini na mashahidi wa nje.

Kilikuwa ni kipindi cha jua mwaka 1943 minong'ono ikasikika ikizunguka kwamba Sobibor itasimamisha operesheni yake, wafungwa wakaelewa kwamba hilo lilimaanisha wote watauawa,kwani kambi ya Belzec kabla ya kusimama iliua wafungwa wake wote, kamati ya kutoroka ikaundwa kufuatia minong'ono hiyo, viongozi wao walikuwa ni Leon Feldhendler, mwanachama wa zamani wa Judenrat huko Zoikiewka kazi yake ya kuchambua makambini ilimpa nafasi kufikia chakula cha ziada na kutokuwa na njaa, ingawa kamati hiyo ilifanya vibaya wakati huo wa kiangazi kwa kuhofia usaliti na kupelekea adhabu ya pamoja itakayowapata,pia kati yao hapakuwa na mwenye mbinu za kijeshi au uzoefu, walihitaji kuweka usiri hadi Septemba mjadala wao ulikoma.

Ilipofika Septemba 22 mwaka 1943 mambo yalibadilika kwa kasi baada ya wayahudi 20 kuwasili Sobibor kama wafungwa wa kivita wakitokea Minsk Ghetto, wakachaguliwa kuwa wafanyakazi, kati yao alikuwepo Alexander Pechersky ,mcheza filamu, mtunzi wa nyimbo ,na kamisaa wa siasa, aliyeongoza utoro kambini Sobibor, ile kamati ya Wanachama wa utoro ikawapokea wageni hao warusi kwa shauku lakini pia waliwatahadharisha.

Upande mwingine hao warusi walikuwa ni askari na walikuwa na uzoefu hata wa kusukuma mbele mipango ya utoro,kwa upande mwingine palikuwa na wasiwasi wa kutoaminiana katika zoezi hilo.


Leon Feldhendler alijitambulisha kwa Pechersky akitumia jina la bandia la Baruch, huku akimchunguza kwa siku kadhaa za mwanzo kambini hapo, siku hizo Pechersky alijitofautisha na kuwa si kwamba amesimama upande wa maofisa wa NAZI lakini kwa kuonyesha busara jinsi alivyofanya mambo yake .

Leon Feldhendler akamkaribisha Pechersky kushiriki katika habari za nje ya kambi katika kikao hicho eneo la makambi ya wanawake ,mwanzo Leon Feldhendler alishtuka kusikia kuwa Pechersky hawezi kuongea lugha ya Kiyidi, Lugha mama ya wayahudi wa ulaya Mashariki, ingawa wawili hao waliweza kuwasiliana kwa kirusi na Pechersky akakubali kuhudhuria katika kikao hicho, Pechersky akatoa hotuba na kuchukua maswali Wakati rafiki yake Solomoni Leitmann akitafsiri kwa lugha ya kiyidi (Leitmann alikuwa ni myahudi wa Poland aliyekutana awali na Pechersky huko Mink ghetto) Leon Feldhendler na Wanachama wengine wa kamati ya utoro walikuwa na wasiwasi wa wazi juu ya propaganda za kikomunisti za Pechersky hata Hivyo walivutiwa nae ,walikuwa na hofu juu ya Swali alilolijibu Pechersky kuhusu kwamba kama washirika wa Kisovieti wataweza kuikomboa kambi, "Hakuna mtu yeyote anayeweza kufanya kazi yetu."

Wiki chache mbele Pechersky mara chache alikutana na kamati ya utoro ,vikao hivi vilifanyika makambi ya kinamama ,Pechersky na Leon Feldhendler wakakubaliana kwamba utoro ufanywe na wafungwa wote 600 lakini baadae wakamalizia kwamba wasiwashirikishe wafungwa 50 wa Sonderkommando waliotengwa peke yao pale Lager III chemba za gesi, mwanzo Pechersky na Leitmann walijadili mpango wa kuchimba handaki kuanzia katika karakana ya Fundi seremala ya lager I iliyo karibu na uzio wa kusini ,wazo hilo likaachwa kuwa itakuwa vigumu, kama handaki hilo lingekwenda chini sana lingejaa maji na kuleta Mafuriko , na pia wangelipua mabomu pori la madini nje lililozunguka kambi, zaidi ,waratibu walitia shaka kwamba wafungwa wote 600 wangeweza kushikwa kabla ya hata hawajatoka ndani ya handaki.

Wazo la mwisho la kutoroka lilitoka kwa Pechersky Wakati akifanya kazi ya kupasua kuni nje msituni Karibu na Lager III alipokuwa akifanya kazi alisikia sauti ya Mtoto ndani ya chemba ya gesi akipiga kelele "mama ! mama! " akamkumbuka mtoto wake ,Elsa, akaamua kuwa mpango wa utoro uwe ni wa utoro wa kukurupuka ,alishauri kuwa utoro huo hautakuwa mwepesi ,wiki iliyofuata Pechersky na Leitmann wakaandaa mpango wa utoro.

Utoro ulianza mchana oktoba 14 Mwaka 1943, mpango ulikuwa wa awamu mbili ,awamu ya kwanza wafungwa watawaita maofisa wa NAZI maeneo yao ya kazi yaliyofichama ndani ya kambi na kuwaua, mauaji haya yatafanyika masaa machache kabla ya wito wa kufoleni jioni Wakati wa kutambuana, mpango wa pili utaanza jioni Wakati wa kufoleni ,baada ya wafungwa wote watakapofoleni uwanjani Lager I manyapara watawatangazia kwamba askari wamesema kuna kazi maalum ndani ya msitu nje ya kambi hivyo kundi lote litawanyike huru kuelekea geti la mbele.

Wakati walinzi watakapotia shaka kuhusu hilo na kuona sio la kawaida watataka kwenda kuthibitisha kwa maofisa ambao watakuwa tayari walishauawa. Saa 10 jioni Kaimu kamanda Johann Niemann huku akiendesha farasi wake anaelekea kambi ya mshona nguo alikoitwa na fundi Mkuu wa nguo kambini, ili apimwe jaketi lake la ngozi lililochukuliwa Kutoka kwenye mizigo ya waathirika wa gesi, wapanga dili Walitoa kipaumbele cha mauaji ya Niemann aliyemshikia Kamanda mkuu wa kambi aliyekuwa likizo ,Reichleitner, hata kama mpango wa utoro hautafaulu waliamini kifo cha kamanda huyo kingeleta mtafaruku na wao kutoroka kirahisi.

Wakati Kamanda akilishangaa koti lake ,akamuona mrusi mfungwa mmoja amesimama pembeni na shoka ,Niemann akauliza;" yule anafanya nini pale"? Lakini aliridhika na jibu la mshoni mkuu kwamba yupo pale anakarabati meza ,alipopokea ombi la mshoni la kwamba ageuke nyuma kuona kama kuna kasoro zozote nyuma ya koti lile, akairudisha bastola yake ndani ya jaketi na kugeuka nyuma, ikawa kosa kubwa sana ,mara wafungwa wawili wenye mashoka wakajitokeza na kumpasua kichwa chake kwa nyuma ,mwili ukafichwa chini ya meza ,damu ikafunikwa na vumbi la mbao.

Masaa machache baadae maofisa wa Nazi waliuawa kila baada ya dakika sita ,mbali na Niemann Wengine waliouawa ni pamoja na ;Josef Vallaster, Siegfried Graetschus, Ivan Klatt, Friedrich Gaulstich, na Fritz Konrad ambao waliuawa kule Lager II ,Josef wolf na Rudolf Beckman ,Walter Ryba aliuawa kule mbele ya kambi ,wengine ni ,Max Bree, Anton Nowak ,Thomas Steffi, Erst Stengelin.

Wafungwa walipanga kumuua Rudolf Beckmann pale Lager II bohari ya makambi ,lakini alipokuwa njiani anaelekea kwenye wito akashtuka, machale yakamcheza akarudi ofisini ,Chaim Engel akajitolea kwenda kumuua Beckman huko ofisini kwake, baada ya kusikia sauti ya Leon Feldhendler anajadili suala na Nyapara Hersh Pozyczki , Pozyczki na Engel wakaelekea pamoja jengo la ofisi ndipo Engel akamchoma Kisu Beckmann, Wakati huo Pozyczki akamshikilia vizuri, Wakati Engel anamdidimiza Kisu alipiga kelele ,"Kwaajili ya Baba yangu ,kwaajili ya kaka yangu kwa wayahudi wote" Beckmann akafanya purukushani kidogo Wakati Kisu kinamuingia na kusababisha kiteleze na kukikata kiganja cha Engel, alipokufa wafungwa hao wakausukuma mwili wake chini ya dawati bila kuuficha wala kusafisha damu.

Wakati mauaji yakiendelea ,Szlomo Szmajzner alikwenda uwanja wa mbele kuchukua silaha zaidi za makambini kwa walinzi ,wakati wa kikao cha mwisho cha oktoba 12 alijitolea kufanya kazi hiyo, akiwa fundi mashine wa kambi ya Sobibor Szmajzner ,alikuwa mara nyingi akiitwa kusafisha na kukarabati majiko ,Hivyo ikawa ni nafasi yake ya kuingia makambini na kubeba mapipa ya majiko ya kuyabadilisha kwa kuyabeba mabegani mwake.

Aliingia kambi ya walinzi na kujichukulia silaha sita na risasi ,ingawa aliweza kubeba bunduki mbili ndani ya mapipa yake ya jiko hivyo zingine alizizungusha ndani ya blanketi kabla ya bigura halijalia la saa 11 jioni aliwaona wafungwa watoto wawili akawaingiza wabebe blanketi lenye bunduki ,waliogopa akawalazimisha kwa kuwatolea Kisu baada ya bigura kulia akafikisha bunduki kwa warusi ,lakini walimtaka abakie na moja kwaajili yake.

Wakati muda wa kufoleni unakaribia Pechersky akawa na mashaka kwamba utoro utashtukiwa alishangaa alipoona umefanikiwa pia mauaji waliyotarajia hayakutokea ,wafungwa wenye msukumo walimuua ofisa ,Walter ryba ,nje ya gereji ya mbele ya geti ,Pechersky alitaka utoro uanze mapema lakini alisita ,sababu ofisa Karl Frenzel alikuwa bado yupo hai na ndiye ofisa hatari sana Sobibor, alichelewa bafuni hivyo akachelewa wito waliompa wa kufika dukani kwa seremala karibu na saa 11 jioni Pechersky na Leitmann mwishowe wakaamua kukata tamaa na Frenzel na kumtuma mpuliza tarumbeta ,Judah, kupanda kidunguni na kupuliza bigura kuashiria muda wa kazi umekwisha.

Kipindi hiki wafungwa wengi wa Lager I tayari waliacha kazi zao na kusimama uwanjani kufoleni au wapo waliojificha katika Majengo ya karibu ,pale lager II wafungwa walichanganywa na bigura la mapema na kujikusanya bila mpangilio kuelekea lager I, Leon Feldhendler akashuku kwamba mpangilio wa mistari usio wa kawaida labda utawashtua walinzi hivyo akaamua kuongoza Matembezi hayo kuelekea uwanja wa foleni, akawapanga na kutembea nao wakiimba wimbo wa kijerumani, Wakati wanafika uwanjani minong'ono ikaanza kusambaa kati yao kuhusu utoro huo ,wakati mlinzi anawasukuma wapange mstari haraka ,kundi la wafungwa likapiga kelele na kumwambia "Hivi hufahamu kwamba vita vimekwisha" wakamwua kweupe, kwa mshangao wa wengi Pechersky akawaeleza wafungwa nini kinachoendelea; "Siku yetu imefika wajerumani wengi wameshauawa sasa tufe kwa heshima ,kumbukeni yeyote atakayepona lazima auambie ulimwengu nini kilichotokea hapa."

Wakati wafungwa wanajaribu kutawanyika wakasikia risasi toka Lager II, risasi hizo zilipigwa na ofisa Erich Bauer, aliyerudi toka Chelmi akiwa na Lori lililojaa pombe aina ya Vodka, Kabla ya lile bigura halijalia ,Bauer aliwaagiza wafungwa watoto wawili kushusha pombe na kubeba kupeleka stoo ndani ya jengo la ofisi ,ambako Beckmann aliuawa, Wakati Pechersky anatoa hotuba Lager I mlinzi alikimbia kwa Bauer akipiga kelele na kudhania wale watoto walikuwa ndio wahusika wa kumuua Beckman ,Bauer akawafyatulia risasi na kumuua Mmoja akamkosa mwingine ,Wakati wafungwa Walioko lager I wanasikia milio hiyo, umati ukatawanyika na kukimbia uelekeo tofauti ,kundi la wafungwa likamvamia mlinzi mwenye baiskeli na kumuua ,wafungwa wengi walikuwa hawaelewi kinachoendelea na walioelewa hawakuwa na maelezo ya kina.

Leon Feldhendler na Pechersky wakakimbia uwanjani hapo kujaribu kuwasonga wafungwa watoroke lakini kama 175 hivi walibakia kambini. Pakawa na kuchanganyikiwa kwani walinzi vidunguni hawakuanna kuwamiminia risasi wafungwa ,baadhi ya walinzi walijificha wakidhani majeshi pinzani yameiteka kambi ,baadae walinzi walianza kuwafyatulia risasi wafungwa ,baadhi ya wayahudi nao wakafyatua risasi zao zilizotoka kwa Szmajzner ,na bastola zilizotoka kwa maofisa waliouawa, Szmajzner akampiga risasi mlinzi aliye juu ya kidungu.

Kundi moja la wafungwa lilikimbilia nyuma ya duka la fundi seremala ,Mafundi waliacha vitu kama ,ngazi,shoka,koleo, vilivyolalla katika majani karibu na uzio wa kusini kama mpango tu iwapo geti kubwa litashindikana kupitika ,wafungwa wakaushusha uzio huo, wakavuka mitaro na kuanza kukimbia kuelekea pori lenye madini linaloelekea msituni, Wakati wanakimbia mabomu yalilipuka na kuua baadhi yao ,hilo liliwavutia walinzi katika vidungu na kuanza kuwamiminia risasi, Esther Raab, alihisi risasi imemkwangua kichwani juu ya sikio lake, akaendelea kukimbia ,kisha akahisi anapungukiwa nguvu ,akaamua kumshika mwanamke aliyekuwa anakimbia mbele yake ,yule mwanamke akamsukuma pembeni na kumwambia "Niache".

Kundi kubwa la wafungwa lilisonga kuelekea makambi ya mbele ,hawa walijaribu kutoroka kupitia geti la mbele hawa walijaribu kutoroka kupitia geti kuu au kusini mwa uzio, wakati huo kundi la wasovieti lilijaribu kuvamia ghala la silaha huko wakakutana na Frenzel ambaye Kipindi hicho alikuwa katoka kuoga na alikuwa anapata chai kantini akasikia kuna vurugu ,akachukua bunduki mashine(Machine gun) ,akatoka nje ,akaona kundi la wafungwa wanaelekea mlango mkuu akaufyatulia risasi umati wa wafungwa.

Pechersky akamlenga shaba Frenzel akitumia bastola ya vallaster ,Lakini akamkosa, kundi la wafungwa likajaribu kubomoa lango kuu na kutokomea nje ya geti. Wengine kule makambi ya mbele walijaribu kutoroka juu ya waya wenye miiba nyuma ya makambi ya maofisa wa Nazi wakifikiri kutakuwa na mabomu machache upande ule, wengi wao walinaswa na senyenge .

Takribani wafungwa 300 walitokomea msituni, muda huohuo baada ya utoro ,huko msituni kundi la wafungwa 50 lilimfuata Pechersky na wengine ,Warusi 7 wakaoondoka wakidai wanafuata chakula lakini badala yake walivuka mto Bug, na kufanya mawasiliano na majeshi yao ,baada ya Pechersky kutorudi wafungwa waliobaki wakagawanyika makundi madogo na kuelekea njia tofauti tofauti.

Baada ya vurugu kusimama maofisa waliopona wakaanza kuzungukia kambi ,wakawakuta wafungwa waliobaki lager I, wakawaua wote waliosalia , wakamtafuta Naibu mkuu wa kambi ,Niemann, waliendelea na ukaguzi mpaka Usiku, wafungwa walikata nyaya za umeme na simu ,wakaukuta mwili wa Niemann kambi ya mshoni ,Frenzel akakusanya askari wote akitegemea kwamba wafungwa waliotoroka wanaweza kurudi na kuishambulia kambi, walipogundua kuwa wafungwa wamekata hadi nyaya za simu ,akaelekea stesheni ya Sobibor kutuma telegram na simu ,alianzia saa 8 mchana kuvipigia simu vikosi vya Lublin na chelm, pia Karibu na vikosi vya Wehrmacht, vikosi hivyo vilichelewa kuwasili sababu ya miundo mbinu yake kuharibiwa na majeshi ya nchi nyingine ,ingawa ulipotinga Usiku kundi la maofisa liliwasili akiwemo ,Gottliey ,Hering na Christian wirth, Wirth akampa amri Bauer kwenda kuwaleta polisi wa Chelm ,sababu Frenzel alishindwa kuwapata kwa simu ,Bauer akasita akiogopa anaweza kuvamiwa njiani na wafungwa.

Mapema Siku iliyofuata Oktoba 15 ,Wanazi wakaungana na maofisa kadhaa kama ,Hermann Hofle, na askari 8 wa Wehrmacht ,wakawasaka wafungwa 159 waliokuwa lager III, na kuwapiga risasi wote, wakaanzisha msako mkali ,wakihofia kwamba warusi watafika hadi vijijini Poland wakisambaza ushahidi wa jinai waliofanya maofisa wa NAZI , Maofisa,Wehrmacht na ndege ya Luftwaffe wakafagia eneo lote linalozunguka kambi ya Sobibor, huku wananchi jirani wakiahidiwa zawadi nono wakiwaona wafungwa. Maofisa kadhaa walioshiriki msako huo walipewa tuzo za medali kwa tendo hilo sahih na Hitler.

Watoroo 59 walishikwa vijiji vya Sobibor na Rozanka Oktoba 17 na 18 ,wajerumani wakarudisha silaha zao Kutoka kwao vikiwemo mabomu ya mkono ,siku chache baadae oktoba 21 wayahudi wengine 5 waliuawa na askari wa Wehrmacht karibu na Adampol na wengine 8 huko Sawin .Takwimu ilionyesha watoro 107 waliuawa na wajerumani, Wakati 23 waliuawa na wasio wajerumani.

Oktoba 19 Chifu Heinrich Himmer, akaamuru kambi ifungwe, wayahudi watumwa wakapelekwa Sobibor toka kambi ya Treblinka ili kuivunja Sobibor, walibomoa Majengo mengi yakiwemo chemba za gesi, lakini baadhi waliyaacha kazi ilimalizika Oktoba na wayahudi wote walioletwa toka Treblinka wakapigwa risasi kufuta ushahidi kati ya Novemba 1 na Novemba 10.

Ofisa Erich Bauer akawa wa kwanza kupanda kizimbani kwa makosa ya jinai ,Bauer alikamatwa mwaka 1949 wakati wafungwa wawili waliokuwa Sobibor kumtambua ,Samwel Lever, na Esther Terner, Mwaka mmoja baadae Bauer alihukumiwa kifo ,ingawa adhabu yake ikabadilishwa na kuwa kifungo cha maisha ,Kesi ya pili ya Sobibor ilikuwa ya Hubert Gomerski aliyehukumiwa kifungo cha maisha lupango, baliJohann Klier aliachiliwa huru .

Frenzel alihukumiwa kifungo cha maisha kwa kuua wayahudi 6 na kushiriki mauaji ya halaiki 150,000 ,Kurt Bolender alijiua kabla hata hajahukumiwa. Walinzi wachache waliohudumu Sobibor walipanda kizimbani huko umoja wa Kisovieti wakiwemo ,B. Bielakow ,M. Matwijenko, I. Nikifor, W. Podienko ,F. Tichonowski, Emmanuel Schultz, na J. Zajjerew ,walihukumiwa kwa uhaini na jinai ya vita, wote walipigwa kitanzi ,April 1963 mahakama ya Kiev, ambapo Alexander Pechersky akiwa Shahidi upande wa mashtaka ,walinzi 10 walikutwa na makosa na kuuawa ,Mmoja alihukumiwa miaka 15 jela ,kesi ya tatu ya Kiev urusi Ilikuwa ya walinzi watatu wa Sobibor na Belzec waliuawa na kikosi cha kupiga risasi .(Firing squad)

Mei 2011 ,John Demjanjuk ,alifungwa jela kwa vifo vya wayahudi 28,000 akiwa mlinzi wa Sobibor ,alifungwa Miaka 5 jela lakini aliachiwa kwa rufaa, alifariki nchini Ujerumani akitibiwa nyumbani kwake ,machi 17 Mwaka 2012 akisubiri rufaa yake.

Hadi Miaka ya 1990 Wavumbuzi walifika eneo la Sobibor, kambi iliharibiwa na ikapandwa miti, kuficha Ushahidi wa kilichotokea ,walikuta mashimo saba yenye ujazo wa mita za mraba 19,000 baadhi yanaonyesha yalikuwa ni makaburi ,mengine kwaajili ya kuchomea maiti ,mabaki ya senyenge katika miti wakagundua ni mabaki ya uzio wa kambi hadi mwaka 2018 makaburi ya halaiki ya lager III yalijazwa na mawe meupe na ujenzi ulianza wa jengo jipya la makumbusho ,jengo ambalo limebakia Kutoka Katika kambi ya Sobibor ni la ofisi za Posta lenye rangi za kijani na linamilikiwa na watu binafsi au ofisi ya misitu .

Pia Mwaka 2007 timu ya Wavumbuzi walikuta msingi wa chemba za gesi ,kati ya Mwaka 2011 na 2015 walikuta ,mawani, nyembe,mikasi,dawa za meno,saa,sarafu,sahani,vitana nk. Mwaka 1987 ikachezwa picha ya "Escape from Sobibor" ya British TV film.

Post a Comment

0 Comments