Ifahamu reli iliyounganisha Pwani ya Bahari ya Atlantiki na Pwani ya Bahari ya Pasifiki nchini Canada 1871

NA CHARLES REGASIAN

MIAKA 150 iliyopita sehemu kubwa ya Canada,nchi ya pili kwa ukubwa duniani, haikuwa imewahi kutembelewa.

Hivyo mwanahistoria Pierre Berton alisema kwamba,asilimia 75 ya wakazi nchini humo waliishi mbali na watu wengine kwenye mashamba, na hali mbaya ya barabara ilifanya usafiri uwe jambo gumu sana.

Pia usafiri wa majini ulitatizwa sana, kwani maziwa na mito iliganda na kuwa barafu kwa miezi mingi kwa mwaka.
Kwa sababu ya magumu hayo yote mnamo mwaka 1871,Waziri Mkuu wa Canada, Bw. John MacDonald alipendekeza reli ijengwe ambayo ingeunganisha Pwani ya Bahari ya Atlantiki na Pwani ya Bahari ya Pasifiki.

Ingawa Reli ya aina hiyo ilikuwa imejengwa nchini Marekani mwaka 1869,nchi ya Canada ilikabili magumu yote ya kipekee kama vile upungufu wa pesa.

Reli hiyo ingepitia eneo kubwa zaidi kuliko ile ya Marekani na pia idadi ya wakaazi wa Canada ilikuwa asilimia 10 zaidi ya ile ya Marekani.

Kiongozi mmoja wa kisiasa wa Canada alisema kwamba, wazo hilo ni mojawapo ya mambo ya kipumbavu zaidi kuwazika, mwingine pia alimdhihaki Waziri Mkuu na kusema kuwa sasa angependekeza reli ijengwe kuelekea kwenye mwezi.

Licha ya hayo,Serikali ya Canada iliahidi kukamilisha ujenzi huo wa reli baada ya miaka kumi, Sandford Fleming aliyekuwa Mhandisi wa Reli Mskoti, alikadiria kuwa ujenzi wa reli hiyo ungegharimu dola milioni 100 hivi, pesa nyingi sana wakati huo, ingawa ingekuwa rahisi sana kupitisha sehemu fulani ya reli kwenye eneo la Marekani, MacDonald alisisitiza kwamba reli ijengwe kwenye eneo la Canada pekee bila kupitia nchi nyingine, ili kulinda maslahi ya kanada iwapo vita vingezuka.

Wawekezaji wengi hawakutaka kushiriki mpango huo, kwasababu waliuona kuwa ghali sana na pia usiotegemeka.

Hata hivyo, kufikia mwaka 1875,Shirika la Reli la Canada Pacific Railway (CPR) lilianza ujenzi, lakini miaka kumi baadaye ,ujenzi huo ulikuwa karibu kukatishwa,shirika hilo lilikuwa limeshindwa kulipa deni lake la dola 400,000 za Canada ambalo lilipaswa kulipwa kufikia saa 9 Julai 10.

Lakini alasiri hiyo hiyo mwendo wa saa 8, Bunge la Canada lilikubali kutoa mkopo zaidi, na ujenzi ukaendelea.

Ujenzi wa Reli ulipokuwa ukiendelea huko Ontario Kaskazini, wafanyakazi walifika mahali palipokuwa na mwamba mkubwa uliokuwa futi moja chini ya ardhi. Hivyo walilazimika kusafirisha mchanga kutoka mbali sana.

Huko Canada ya Kati, wakati wa msimu wa baridi kali,viwango vya joto vilishuka chini kufikia nyuzi 47 selsiasi chini ya sifuri, na hivyo kusababisha matatizo mengi ya ujenzi ulipokuwa ukiendelea.

Zaidi ya hayo ilikadiriwa kwamba kiwango cha theluji iliyomwagika kila mwaka ilifikia mamia ya sentimeta juu ya ardhi.

Eneo la milima ya Rocky iliyopo upande wa Magharibi ilisemekana kuwa mahali ambapo kifo hutokea ghafla, walihitaji kujenga madaraja na barabara za chini ya ardhi kufanya kazi saa kumi kwa siku ilikuwa kawaida licha ya mvua,matope au theluji.

Hatimaye,Novemba 7, mwaka 1885, bila mbwembwe nyingi,msumari wa mwisho ulipigiliwa kwenye eneo la Eagle Pass huko British Columbia, iliyoko Magharibi, kituo hicho kiliitwa Craigellachie, jina linalofanana na kijiji fulani huko Scotland ambalo lilijulikana kwa upinzani wake mkali,

Baada ya kuombwa atoe hotuba fupi Meneja mkuu wa CPR alisema kwa ufupi,; "kile tu ninachoweza kusema ni kwamba kazi hii imefanywa vizuri sana."

Maelfu ya Wachina waliokuwa wameletwa nchini Canada ili kushiriki kwenye ujenzi huo, walihakikishiwa kupata ajira ya kudumu kwenye kampuni hiyo ya reli, mara nyingi kazi ilikuwa yenye kuhatarisha hasa kwenye milima ya Rocky,wengi wa wafanyakazi hao hawakufaulu kupata pesa za kutosha kulipia nauli ya kurudi nyumbani hadi miaka mingi baada ya kazi hiyo kwisha.

Kwa sababu ya reli hiyo,viwanda na biashara zilianzishwa upande wa Magharibi mwa nchi hiyo,jambo ambalo liliathiri sana tamaduni za hapo awali.

Miji na majiji yalianzishwa na wenyeji wakahamishwa kwenye hifadhi,njia za biashara za hapo awali ,biashara ndogondogo kama vile migahawa ya barabarani ilifungwa.

Kwa upande mwingine, inasemekana kwamba ujenzi wa reli hiyo ulisaidia jamii iepuke vumbi na matope na pia ikawaepusha na athari za majira ya baridi kali.

Zaidi ya hilo ilichukua siku chache tu kwa vyakula vilivyosafirishwa kutoka nchi za Mashariki, kupitia Pwani ya Bahari ya Pasifiki, kufika kwenye majiji yaliyo upande wa Mashariki.

Ingawa treni bado zinatumiwa kusafirisha mizigo nchini Canada,kuongezeka kwa matumizi ya magari na ndege kumefanya watu wengi waache kusafiri kwa treni.

Hata hivyo, bado watu wengi leo huepuka pilikapilika za maisha ya leo kwa kufurahia mandhari zenye kupendeza wakiwa ndani ya treni yenye kustarehesha kutoka Toronto hadi Vancouver.

Kwa hiyo badala ya kufanya maisha yasonge kwa haraka kama ilivyokuwa hapo mwanzo, usafiri wa treni umewawezesha abiria wapumzike na kutafakari kuhusu historia yake yenye kupendeza wanaposafiri kutoka bahari moja mpaka nyingine wakitumia reli au utepe wa chuma huko Canada.,

Post a Comment

0 Comments