Huyu ndiye David Berkowitz (Mtoto wa Sam), muuaji aliyewalenga wanawake tu

NA CHARLES REGASIAN

DAVID Richard Berkowitz, ambaye alipenda kujiita "Mtoto wa Sam" ni mmoja kati ya wauaji wakubwa waliopata kutokea katika jiji la New York ,ambaye aliendesha mauaji ya kutisha mwishoni mwa miaka ya 70.

Pamoja na kuendesha mauaji hayo na kuwasumbua polisi kwa kiasi kikubwa na kushindwa kumpata, hivyo kulazimika kufanywa uchunguzi upya mwaka 1996, ili kuweza kujua nani hasa aliyeendesha mauaji yale ya kinyama.

Berkowitz alizaliwa katika kitongoji cha Brooklyn, New York ,wazazi wakiwa ni Betty Broder na Joseph Kleinman, lakini upatikanaji wa mimba yake hadi kuzaliwa kwake ilikuwa ni balaa kubwa. 

Kutokana na 'kusakiziwa kwa baba kibao' muuaji huyo aliyetingisha New York,alishawahi kujiunga na Jeshi la Marekani mwaka 1971, na alishiriki pia katika vita vya Vietnam na vilipomalizika alikuwa ni mtu wa dini na kuamua kuoa kabla ya kujikuta akiajiriwa na Shirika la Posta akiwa ni msambazaji barua kabla ya kukamatwa.
Berkowitz shambulio lake la kwanza lilikuwa dhidi ya wanawake katika miezi ya mwisho ya mwaka 1975, mwenyewe anakiri kwamba aliwakamata wanawake wawili kwa kuwateka baada ya kuwatisha kwa kisu wakati wa Siku ya Christmas, polisi walihangaika sana kipindi hicho ikiwa hawajui ni nani aliyewateka na kuwaua wanawake hao.
Picha na Mike Groll/AP/Shutterstock.

Jioni ya kipindi cha Julai 29,1976, wasichana wengine wawili Donna Lauria (18) na Jody Valentine(19) miili yao ilikutwa imepigwa risasi karibu na eneo la kuegeshea magari katika eneo la Bronx,Lauria tayari alikuwa amekufa,lakini Valentine alionekana bado anapumua kwa mbali,muuaji hakujulikana.

Oktoba 23,1976, kulitokea mauaji mengine ambayo yaliwachanganya zaidi Polisi safari hii ni eneo la Queens kwa mara nyingine tena walengwa walikuwa katika eneo la kuegeshea magari, aliyepigwa risasi alikuwa ni Carl Denaro(19),lakini alinusurika kiajabu pamoja na mwenzake Rosemary Keenan. 

Mwezi mmoja baadae Novemba 26,1976 Donna DeMas (16) na Joanne Lomino (18) ambao walikuwa wanatembea kuelekea nyumbani kutoka kutazama picha nao walipigwa risasi katika eneo la Queens, DeMas alinusurika huku Lomino akijikuta anapooza kwa maisha yake yote.

Mwaka mpya ulijikuta watu wengi wakiwa wamepigwa risasi na ilikuwa Januari 30,1977 wakati wachumba wawili Christine Freund (26) na John Diel walipopigwa risasi wakiwa katika eneo la kuegeshea magari, Diel alinusurika,lakini Freund alikufa. 

Polisi baadae walitoa taarifa kwamba mtu anayewalenga zaidi wanawake anatumia silaha aina ya 44 Arms Bulldog,huku wakisema mtuhumiwa anawalenga zaidi wanawake,ana nywele nyeusi na anapenda kuwaua watu waliokuwa katika eneo la kuegeshea magari.

Machi 8,1977, mwanafunzi wa chuo, Virginia Voskerichian (21) alipigwa risasi wakati akitembea katika eneo la Queens. 

Alikufa papo hapo,miezi michache iliyofuata mtu mwingine alipigwa risasi akiwa katika eneo la kuegeshea magari. 

Kutokana na hayo polisi ilibidi waanzishe operesheni Omega ili kumpata muuaji,operesheni ambayo ilihusisha polisi 300 ambao walikuwa wakiongozwa na Inpekta wa Polisi, Timothy J. Dowd. Polisi walizidi kusisitiza muuaji anawalenga wanawake.

Polisi walizidi kumsaka, lakini mauaji yaliendelea kwani Aprili 16,1977, Alexander Essau (20) na Valentina Suriani (18) waliuliwa katika eneo la Bronx. 

Pembeni ya miili hiyo ya watu waliouawa ilikutwa barua iliyoelekezwa kwa Kapteni Joe Borrelli wa operesheni Omega. 

Barua hiyo ilikuwa inaelekeza ni kwa nini anaamua kufanya mauaji hayo kwa kuwalenga wanawake,kwani alikuwa anataka damu baada ya kushiba huku akisisitiza amewabaka wengi kabla ya kuwaua.

"Kwa watu wa eneo la Queens nawapenda niwaambie nawapenda na kuwatakia pasaka njema,kwa sasa napenda kusema kwaherini na tutakuja kuonana,Polisi; nataka niwaambie kitu kimoja,nitarudi ili kuendeleza milio ya bang, bang, bang,- ugh!! Ndimi mtuhumiwa ,Mr. Monster ".

Baada ya kutoa barua hiyo ilipofika Juni 26,1977, kulitokea mauaji mengine kwani Sal Lupo na Judy Placido (17) waliokuwa wakitoka disko katika eneo la Queens, walipigwa risasi, watu hawa inadaiwa walikuwa kwenye gari. 

Yalipokuja kutokea mauaji ya Moskowitz na Violante. Cacilia Davis ambaye alikuwa akiishi jirani na sehemu watu hao walipopigwa risasi alisema alimuona mtu katika eneo la kuegeshea magari na maelekezo yake yalionyesha mtu aliyehusika ni Berkowitz.

David Berkowitz alikamatwa katika eneo analoishi la Yonkers,New York hapo Agosti 10,1977, neno la kwanza alilolisema ni "kwa nini mmechukua muda mrefu kunikamata "? Alipopekuliwa nyumbani kwake alikutwa na ushahidi kadhaa wa kumtia hatiani. 

Muuaji huyu alipokamatwa alijitetea kwa kudai aliyemlazimisha kuanza kuua alikuwa mbwa wa jirani yake kutokana na matendo aliyokuwa akimtendea, lakini alihukumiwa kifungo na mwaka 2005 aliamua kuandika kitabu akizungumzia yote yaliyotokea kwa kipindi hicho.

Mwaka 2006,Berkowitz alimtimua wakili wake kwa madai ya kutaka kumlazimisha aandike kitabu halafu kiwe chake,wakati nia yake kubwa ilikuwa ni kuwapa pesa za mauzo familia za wahanga wa watu aliowaua au kuwajeruhi.
 
Katika mahojiano na CBS mwaka 2013, Berkowitz alijaribu kurekebisha maoni potofu kumhusu. Alisema hakuagizwa kuua na mbwa wa jirani yake, wala haikuwa sehemu ya ibada ya mashetani.

Badala yake alidai kwamba alijisikia kufanya hivyo, kama askari aliyekuwa katikamisheni.Alisema, aliamini kwamba shetani angemwachilia kutokana na maumivu yake ya kihisia, moyo na upweke ikiwa angeua. Pia alisema hakuwa amekunywa dawa yoyote na hakuwa mgonjwa wa akili.

Berkowitz alisema kwamba katika 1987 alipata kuzaliwa upya kiroho, na kwamba Mungu alimsamehe. Mnamo 2007, aliandika msamaha kwenye wavuti yake mwenyewe. "Ninahuzunika kwa ajili ya wale waliojeruhiwa, na kwa wanafamilia wa wale waliopoteza mpendwa kwa sababu ya matendo yangu ya ubinafsi," Berkowitz aliandika. "Najuta kwa kile nilichokifanya na kinanisumbua sana."

Alipoulizwa mnamo 2017 ikiwa ndiye mpiga risasi pekee katika kila tukio, Berkowitz alisema, alichukua jukumu la risasi zote. Alipoulizwa tena ikiwa kuna mtu mwingine yeyote aliyehusika, alisema, "Hebu tuseme hivi, kulikuwa na mapepo."

Berkowitz mwenye umri wa miaka zaidi ya 60, kwa sasa amefungwa katika Kituo cha Marekebisho cha Shawangunk huko Hudson Valley.

Katika mahojiano mwishoni mwa mwaka juzi, aliulizwa tena ikiwa kuna watu wengine walimsaidia kufanya mauaji hayo, alikataa na kudai kuwa, “Kwa sababu Bwana amezichukua dhambi zangu zote na kuzitupa katika vilindi vya bahari, kama Maandiko yanavyosema, hazitakumbukwa tena. Kwa hivyo kwa nini niende kuvua samaki huko na kuvuta vitu hivyo?".

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news