Kamusi ya Kiingereza ya Oxford yaingiza misamiati 200 ya Kiswahili

NA DIRAMAKINI

LUGHA ya Kiswahili imeendelea kuenea kwa kasi duniani baada ya toleo jipya la kamusi ya lugha ya Kiingereza ya Oxford kuingiza maneno ya Kiswahili takribani 200 tofauti na mwaka juzi ambapo kamusi hiyo iliingizwa maneno ya Kiswahili matano pekee.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Bi. Consolatha Mushi wakati akitoa mkakati wa utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzanaia, Dkt. Philip Mpango katika siku ya maadhimisho ya siku ya Kiswahili ulimwenguni iliyofanyika Julai 7, mwaka huu na kuelekeza kuanza rasmi kwa utekelezaji wa matumizi ya lugha ya Kiswahili ili kuendana na maendeleo yake ya kasi ulimwenguni.

''Tunafahamu kamusi ya Oxford inatumika sana duniani, ni kamusi ya kiingereza ila katika toleo hili imehusisha maneno ya Kiswahili mengi zaidi, hii ni tabia ya lugha ya kuchota maneno katika lugha nyingine, na inatupa fahari kubwa na inadhihirisha kuwa Kiswahili kimefika mbali,"amesema.

Amesema, baadhi ya maneno yaliyoingizwa katika kamusi hiyo ni pamoja na neno 'daladala' likimaanisha magari yanayotumika kusafirisha abiria na 'jembe' kifaa kinachotumika kulimia.
''Maneno yaliyoingizwa katika kamusi hii na kuwa rasmi ni maneno yaliyozoeleka kimatumizi, neno 'chapo' likimaanisha chapati linalotumika sana nchini Kenya limeingizwa katika kamusi hiyo, pia neno 'Mama Ntilie ' limeingizwa katika kamusi ya Oxford kwa maana ya Mama anayepika chakula na kuwauzia watu kwa gharama nafuu ili kila mtu aweze kumudu na kupata chakula, aidha neno 'Singeli' limechukuliwa kama muziki ambao asili yake ni Tanzania, neno 'Kolabo' na 'sambaza' pia yameingizwa katika Oxford...Hii ni dhahiri kuwa Kiswahili kwa sasa kinaenda kwa kasi kubwa,"amesema.

Aidha amesema kuwa, Kiswahili kinazungumzwa na watu wapatao milioni 500 duniani msamiati wake unakua na kukuza lugha nyingine na kuingizwa kwa maneno hayo katika kamusi ya Oxford kutasaidia katika kusambaza msamiati wa Kiswahili pamoja na utamaduni wa Mswahili.

''Neno jingine lililoingizwa katika kamusi ya Oxford ni 'chips yai', wengi watataka kufahamu chakula hiki cha chips yai kipoje na kinatengenezwaje tayari tumepeleka utamaduni wa vyakula katika lugha ya kiingereza..Hii ni tija kubwa na fahari kubwa mabaraza yapo kwa ajili ya kutengeneza msamiati ili kusonga mbele zaidi,"ameeleza.

Amesema kuwa, mabaraza yaliyoundwa kisheria yataendelea kufanya usanifishaji na utafiti mkubwa wa kuchukua maneno mengine ya lugha za kiafrika na kuyaingiza katika lugha ya Kiswahili.

Akitoa tamko juu hatua ya kuanza utekelezaji wa maagizo ya matumizi ya lugha ya Kiswahili ili kuendana na kasi ya maendeleo ya lugha ya Kiswahili yaliyotolewa na Makamu wa Rais Dk. Philiph Mpango, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa Bi. Consolatha amesema kuwa maagizo hayo yanayotakiwa kuanza kutekelezwa kuanzia sasa ni pamoja na nyaraka za Serikali kati ya ofisi moja na nyingine, idara na idara, taasisi za Umma na binafsi na mashirika kuandikwa kwa lugha ya Kiswahili na ikiwa nyaraka hizo zinaandikwa kwa mgeni nyaraka mbili za kiingereza na Kiswahili zitumike.

''Makamu wa Rais pia ameelekeza katika majina ya barabara, mitaa na majina ya vifaa mbalimbali yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili..Katika zoezi linaloendelea nchini la kuweka majina ya mitaa tumeona lugha inayotumika pengine inakosewa hivyo agizo la Makamu wa Rais la kuandika majina ya mitaa kwa lugha ya Kiswahili lizingatiwe na lugha itakayoandikwa iwe fasaha na sanifu..Baraza lipo tayari kutoa msaada wa kuhakiki majina hayo,"amesema.

Aidha amesema maeneo mengine ambayo utekelezaji wake unapaswa kuanza mara moja ni pamoja na mabango ya matangazo yote yaliyopo barabarani kuwa katika lugha ya Kiswahili, maelezo ya bidhaa zote zinazozalishwa viwandani,fomu za usahili pamoja maelezo ya matumizi ya dawa yawe kwa lugha ya Kiswahili ili kuweza kumlinda mlaji dhidi ya athari hasi zinazoweza kutokea kwa kushindwa kuelewa maelezo yaliyotolewa.

''Miradi yote inayohusu wananchi lazima iandikwe kwa Kiswahili ili kuwasaidia wananchi kuelewa miradi hiyo, sheria na kanuni zinaendelea kutafsiriwa kwa Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Baraza ili kukipeleka Kiswahili mbele zaidi..BAKITA na BAKIZA tunaendelea kusimamia utekelezaji wa maelekezo ya maagizo hayo.'' Amesema.

Aidha, amevitaka vyombo vya habari vinavyotumia lugha ya Kiswahili kuzingatia agizo la Makamu wa Rais la kuzingatia matumizi sahihi na fasaha na sanifu ya Kiswahili na wakishindwa watumie mabaraza ya kuelekezwa matumizi fasaha ya lugha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news