Maagizo ya OR-TAMISEMI yawagusa viongozi wote

NA ANGELA MSIMBIRA, OR-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amewaagiza viongozi wa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha wanawatumia maafisa habari katika kuhabarisha umma kuhusu kazi zinazofanywa na Serikali.
Ametoa kauli hiyo leo Julai 2, 2021 wakati akifungua kikaoa kazi cha Maafisa Uhusiano wa Taasisi, Maafisa Habari wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kilichofanyika katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa jijini Dodoma.

Mheshimiwa Bashugwa amesema kuwa, ni wajibu wa viongozi hao kuhakikisha wanaitumia Timu ya Maafisa Habari nchini kutangaza miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchi nzima ili kuwapasha habari wananchi na kuwawezesha kuelewa kazi kubwa inayofanywa na Serikali yao.

“Suala la Kuhabarisha Umma ni la kufa na kupona kuhusu utendaji kazi wa Serikali kwa watanzania ni muhimu, si jambo la hiari bali ni lazima kuhabarisha umma juhudi za Serikali katika kuwatumikia wananchi,"amesitiza Waziri Bashungwa.

Amewataka Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wilaya, wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi katika mwaka wa fedha 2022/2023 kuhakikisha wanatoa habari kuanzia ngazi ya kijiji, Mtaa, Wilaya, Mikoa na Taifa kwa ujumla ili kila Mtanzania aweze kujua kazi zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita Chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Pia, Bashungwa amewataka viongozi hao kuhakikisha wanawasimamia Maafisa Habari wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili waweze kutimiza wajibu wao wa kuhabarisha umma kwa wakati kwa kuzingatia sheria, taratibu na Miongozo ya Utumishi wa umma.

Amesema kuwa Maafisa Habari wote nchini wakitimiza majukumu yao kwa weledi kutasaidia kuuhabarisha umma kuhusu miradi mbalimbali inayotekelezwa katika maeneo yao na kujua kazi iliyofanywa na Serikali katika Kuleta maendeleo.
Naye, Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dkt. Charles Msonde amewataka Maafisa Habari wa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha wananchi wanapata habari sahihi na muhimu ambazo serikali inawafanyia.
Aidha, Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO, Gerson Msigwa amewataka Maafisa habari wote nchini kutumia radio na television za kijamiii katika maeneo yao kutangaza mafanikio na aJenda ya kitaifa ili kuweza kuisaidia Serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news