Waziri Bashungwa aipa mikoa 15 wiki moja kuwasilisha taarifa

NA OR-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI),Mhe. Innocent Bashungwa ametoa wiki moja kwa mikoa 15 ambayo haijatekeleza maagizo ya kuhuwisha tovuti zao yaliyotolewa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye katika kikao kilichofanyika Tanga kufanya hivyo.
Amesema, kutokana na kuanzishwa kwa kitengo kipya cha mawasiliano serikalini kwenye mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa anataka kuona maelekezo ya kihabari yakoyekelezwa kwa haraka na itakuwa ni miongoni mwa kipimo kwa maafisa habari kukaimu nafasi za ukuu wa kitengo. 

“Unaweza usipewe Kukaimu Kitengo hiki kwa uzembe kama huu kushindwa kutekeleza maagizo ya viongozi kuhusu taarifa zitakazowezesha upatikanaji wa taarifa kwa wananchi,"amesema Mheshimiwa Bashungwa. 

Amesema, kwa sasa halmashauri 118, mikoa minne bado hazina maofisa habari na kusisitiza kuwa Serikali imetoa nafasi 38 za ajira kwa maafisa habari kwenye mikoa na halmashauri.

Waziri Bashungwa pia ameagiza kufanyika msawazo wa maofisa habari ndani ya mwezi huu ili kufanyika tathmini ya kamili ya upungufu wa maafisa habari hao.
Pia amehimiza maofisa hao kuwakumbusha watanzania umuhimu wa kushiriki Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23, mwaka huu. 

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu TAMISEMI, Dkt.Charles Msonde, amesema moja ya kikwazo wanachokabiliana nacho maofisa hao ni kutowatumia kuingia kwenye kikao cha kisheria na wamekuwa wakitekeleza majukumu mengine ambayo si yao. 

“Kumekuwa na tabia ya baadhi ya mamlaka kuwapuuza maofisa habari hali inayowapelekea kutekeleza majukumu ambayo sio ya taaluma yao kama usaidizi wa wakuu wa mikoa na ukatibu,”amesema.

Awali, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema jambo la kusikitisha ni kwa baadhi ya maafisa habari kutowajibika kujibu hoja pale panapotokea upotoshaji. 

Amesema, kati ya zaidi ya maafisa habari 350 waliopo nchini kati ya silimia 70 hadi 80 wanatoka mamlaka za serikali za mitaa na kushangaa kushindwa kukemea watu wanaoisema vibaya serikali. 

Amesema kupitia mkutano wao uliofanyika jijini Tanga walikubaliana mambo mbalimbali ikiwemo kuongeza ufanisi kwenye utendaji na kutangaza ajenda za kitaifa na taarifa zipelekwe Idara ya Habari Maelelezo, lakini cha kusikitisha hakuna kilichofanyika mpaka sasa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news