Makamu wa Rais, Dkt.Mpango alielekeza Benki Kuu kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa wananchi

NA MWANDISHI WETU

MAKAMU wa Rais, Dkt. Philip Mpango, ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kukaa na sekta ya fedha kuangalia namna watu wanavyoweza kupata mtaji kwa ajili ya biashara na uwekezaji.
Akizungumza baada ya kutembelea Banda la Benki Kuu wakati wa kilele cha Maonesho ya Sabasaba leo, Dkt. Mpango amesema mfumo wa watu kupata mtaji kwa ajili ya kuanza biashara au uwekezaji ni changamoto kubwa sana ambayo inawakabili Watanzania walio wengi.

“Mfumo wa kupata mtaji,startup capital ni changamoto kubwa. Hebu mliangalie, mlichambue zaidi” ili kulipatia ufumbuzi, alisema Makamu wa Rais.
Aidha, Dkt. Mpango ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania kuisaidia Serikali kutoa elimu kuhusu faida ambazo wafanyabiashara wanaweza kupata katika soko huru la biashara barani Afrika (African Continental Free Trade Area (AfCFTA). 

“AfCFTA kuna fursa ya soko kubwa sana. Huko nako mtusaidie kuelimisha wafanyabiashara waweze kunufaika, na sisi kama taifa tufaidike,” alisema Dkt. Mpango wakati akielekea kufunga rasmi Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam katika viwanja wa Mwalimu Julius Nyerere wilayani Temeke. 

Aidha, Makamu wa Rais ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania kwa kazi zake inazofanya, ikiwemo kuishauri serikali kuhusu masuala ya uchumi.

Katika Banda la Benki Kuu ya Tanzania, Makamu wa Rais alikaribishwa na Mkuu wa Chuo cha Benki Kuu Mwanza, Dkt. Nicas Yabu na Mkuu wa Banda la Benki Kuu katika maonesho haya, Kaimu Meneja wa Uhusiano wa Umma na Itifaki, Bi. Victoria Msina.

Bi. Msina alimweleza Makamu wa Rais huduma ambazo Benki Kuu ya Tanzania imekuwa inatoa katika maonesho kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu shughuli mbalimbali inazofanya, pamoja na kujibu maswali mbalimbali ambayo wananchi wanakuwa nayo kuhusu majukumu ya Benki Kuu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news