MHE.UMMY AWATAKA WATOA HUDUMA KUILINDA NHIF, AONYA UDANGANYIFU UNAOFANYIKA ASEMA HILO HALIKUBALIKI

NA MWANDISHI WETU

WATOA Huduma nchini wametakiwa kuacha vitendo vya udanganyifu dhidi ya huduma za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa kuwa Wizara haiko tayari kuona na kuvumilia vitendo hivyo.
Akizungumza na Watoa Huduma za matibabu wanaohudumia wanachama wa NHIF wa Mkoa wa Dar es Salaam, Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema vitendo hivyo havikubaliki hata kidogo kwa kuwa vina madhara makubwa na vinalenga kuua Mfuko. 

Aidha amesema kuwa Serikali itaendelea kuthamini mchango wa Hospitali binafsi kutokana na umuhimu wake katika uimarishaji wa huduma za matibabu nchini.
"Tunafurahi kuona uwekezaji ukifanywa katika utoaji wa huduma za matibabu lakini hatuko tayari kuona usajili wa vituo hivyo ukileta madhara kwa Mfuko. Mfano baadhi ya vituo vya kitalaam vinaanzishwa na vinakuwa uchochoro wa udanganyifu, hili hatuko tayari, mtasajili lakini tutatoa vigezo vya kuhudumia wanachama wa NHIF," 

"Ni jukumu letu sisi wote na nyie Watoa huduma kuhakikisha Mfuko huu unadumu na tunaulinda na ni ukweli usiopingika kuwa bila NHIF uendeshaji wa vituo vyetu utakuwa mgumu sana na hili ndio linaumiza kwa kuwa NHIF tunaitegemea na wakati huo huo tunaihujumu" alisema Mhe. Ummy.

Alisema kuwa asilimia 70 ya mapato ya vituo vingi yanatokana na malipo ya huduma kutoka NHIF hivyo unaweza kuona ni kwa namna gani kila mmoja anapaswa kuulinda Mfuko.
"Natamani kuona vituo vya kitalaam vikisajiliwa kila siku lakini tatizo kubwa ni uaminifu wa watumishi wetu ambao wanadiriki hata kufanya vitendo vya kuhamisha wagonjwa kutoka Hospitali za Serikali kwenda vituo binafsi, hili halikubali hata kidogo na huu ni udanganyifu," alisema Mhe. Ummy.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Hospitali Binafsi Dkt. Egina Makwabe aliweka wazi msimamo wa umoja huo kuwa hautetei aina yoyote ya udanganyifu na inachoelekeza ni utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa. 
Akitoa maelezo ya awali Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga alionesha takwimu za maendeleo ya Mfuko na maboresho mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa mifumo ambayo inarahisisha utoaji huduma na kuimarisha uendelevu wa Mfuko.

"Mfuko umeendelea kuwekeza katika mifumo ambayo inarahisisha huduma lakini pia kudhibiti udanganyifu na kuimarisha uendelevu wa mfuko," alisema Bw. Konga.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi NHIF Bw. Juma Muhimbi alisema kuwa Bodi yake inawathamini Watoa Huduma na imekuwa ikifanyia kazi maoni yanayotokana na vikao kama hicho kwa lengo la kuboresha huduma kwa wanachama.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news