Mjue Moshe Katsav, Rais wa Israel aliyewahi kufungwa kwa kosa la kubaka

NA CHARLES REGASIAN

MOSHE KATSAV, ambaye alikuwa ni rais wa nane wa Israel,alizaliwa katika mji wa Yazd nchini Iran. Lakini alirejea nyumbani akiwa na miaka mitano,familia yao ilijikuta kwenye mahangaiko makubwa pale mdogo wake alipouliwa akiwa na miezi miwili tu, kutokana na siasa za machafuko zilizopo kati ya Israel na Palestina.
Makazi yao ndani ya Israel yalikuwa katika hema linaloweza kuhamishwa, lakini makazi ya eneo hilo la Kiryat Malachi yalibadilishwa na kuendelezwa zaidi hivyo kuwafanya waisrael waliokuwa wakiishi kwenye mahema kupata makazi ya kudumu.

Katsav aliwahi kusoma katika Chuo Kikuu cha Hebrew kilichopo Jerusalem,alimaliza chuoni hapo mwaka 1971 ikiwa ni miaka miwili kabla ya kumuoa mkewe Gila. 

Katika ndoa yake hiyo ana watoto watano na kwa sasa ana wajukuu wawili,mkewe alikuwa anafanya kazi benki kabla ya kuamua kufanya kazi za kujitolea hasa kuhusu kupinga unyanyasaji wa wanawake na kupigania haki za watoto.

Katsav alijiunga na chama cha Likud, akiwa na miaka 24 alichaguliwa kuwa Meya wa Mji mdogo wa Qiryat Mal'akhi, akiwa ameweka rekodi ya Meya mwenye umri mdogo kuliko wote waliowahi kuchaguliwa ndani ya Israel. 

Wakati wa utawala wa Serikali ya Yitzhak Shamir,Katsav aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Nyumba kuanzia mwaka 1981-84.

Aliteuliwa tena kuwa Waziri wa Kazi,mnamo mwaka 1984-88 kabla ya kupewa jukumu la kuongoza Wizara ya Usafirishaji na wakati wa uongozi wa Benjamin Netanyau mnamo mwaka 1996-1999, alikuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Utalii.

Baada ya kushikilia cheo hicho,Katsav aliamua kugombea nafasi ya urais akichuana na Shimon Peres. Akamshinda Peres,kwa kuchaguliwa na Bunge la Knesset hapo Julai 31,2000. Alishinda kwa kura 63, akaapishwa Agoati 1,mwaka 2000.

Baada ya hapo alianza kuandamwa na kashfa ya kumbaka mwanamke,kitu ambacho kilionekana kuanza kumsumbua kwa kiasi kikubwa. 

Mnamo Agosti 22,nyumba ya Katsav ilivamiwa na Polisi ambao walichukua kompyuta na nyaraka nyingine ili kutafuta ushahidi wa madai yaliyotolewa dhidi yake. Huku pia akiandamwa na shutuma za kumtaka ajiuzulu kutoka kwenye cheo chake.

Waliokuwa wanataka ajiuzulu walifanya hivyo baada ya Waziri wa Sheria, Haim Ramon kujiuzulu kutoka kwenye nafasi yake mara baada ya Polisi kuivamia makazi hayo ya Rais. Siku iliyofuata alihojiwa na Polisi waliokuwa wakitaka kumuunganisha kwenye tuhuma hizo na zile za rushwa.

Alidaiwa pia kumlazimisha mwanamke mwingine kufanya naye mapenzi. Agosti 25,Taasisi ya Uchunguzi ya Israel ilipewa jukumu la kuanza kuchunguza suala hilo kutokana na maagizo yaliyotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Menachem Mazuz. 

Ilipofika Septemba 7 ikiwa ni baada ya siku kadhaa za uchunguzi ikiwa pia kuwahoji wanawake wanne waliolalamika kusumbuliwa kimapenzi na Rais huyo. Jeshi la Polisi lilitoa taarifa na kusema kwa sasa lina ushahidi mzito juu yake na kinachotakiwa ni mahojiano ya mwisho dhidi yake.

Septemba 13 Bunge liliamua kumwondoa madarakani kwa siku moja Rais huyo ili aweze kuhojiwa,akaapishwa mtu mwingine kushika madaraka kwa siku hiyo, Polisi walitumia vema siku hiyo kwa kumuhoji katsav toka saa nne asubuhi mpaka saa moja usiku.

Akizungumza kwa mara ya kwanza hapo Septemba 18 toka kashfa hiyo iibuke, Mwanasheria Mkuu, Menachem Mazuz alisema Rais alilalamika kwa kufanywa mhanga wa jambo hilo wakati hajalitenda,lakini inashangaza kuona idadi ya wanawake wanaomlalamikia wanazidi kuongezeka.

Oktoba 15,Polisi walitoa taarifa na kudai kuwa ushahidi umeshaonekana dhidi ya tuhuma zinazomkabili na ilipofika Oktoba 29,Katsav alipewa maagizo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Menachem kuacha shughuli za Urais ili Polisi wamalize uchunguzi wa tuhuma dhidi yake. 

Baada ya polisi kumaliza uchunguzi wao, Katsav alifikishwa mahakamani na kufungwa jela miaka saba toka mwaka 2011 na alikuja kuachiliwa kupitia Bodi ya Parole mwaka 2016.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news