Rais Dkt.Mwinyi:Serikali itatoa tamko kuifanya siku ya mwaka mpya wa kiislamu kuwa ya mapumziko

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa, Serikali itatoa tamko kuifanya siku ya mwaka mpya wa kiislamu kuwa ya mapumziko.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiwahutubia Waumini wa Dini ya Kiislam na Wananchi katika Kongamano la Kuukaribisha Mwaka Mpya wa Kiislam 1444 A.H, lililofayika katika Masjid Jamiu Zinjibar Mazizini Unguja leo.Mheshimiwa Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Julai 31, 2022 katika kongamano la maadhimisho ya mwaka mpya wa kiislamu 1444, lililofanyika msikiti wa Jamiu Zinjibar, Mazizini, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Aidha, amesema kuwa, maadhimisho hayo yatafanyika kwa mzunguko kati ya Unguja na Pemba ili kutoa nafasi kwa Waislamu kushiriki.

Ameipongeza Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar kwa kuandaa maadhimisho hayo ambayo ni utaratibu mpya kufanyika visiwani hapa na inatoa fursa kwa waislamu kujua mwaka wao kwa mujibu wa tahehe za dini yao.

“Hakuna asiyeujua mwaka mpya ule wa kawaida na siku ya mwaka mpya ikifika basi kila mtu anajua, lakini kwa bahati mbaya sana mwaka mpya wa kiislamu watu wengi hawautambui,”amesema Mheshimiwa Rais Alhaj Dkt.Mwinyi.

Hivyo, amesema utaratibu wa kuadhimisha mwaka mpya wa kiislamu utawakumbusha Waislamu kuujua.
Waumini wa Dini ya Kiislam Zanzibar wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) wakati akihutubia katika Kongamano la kuukaribisha Mwaka Mpya wa Kiislam 1444.A.H, lililofanyika katika Masjid Jamiu Zinjibar Mazizini Wilaya ya Magharibi “B” Unguja leo.

Aidha, Alhaj Dkt. Mwinyi amewakumbusha wananchi kushiriki zoezi la Sensa ya Watu na Makazi Agosti 23, mwaka huu kwa sababu lina umuhimu katika kupanga maendeleo ya nchi.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman, alimuomba Rais Dkt.Mwinyi kuifanya siku ya mwaka mpya wa kiislamu kuwa ya mapumziko ili waumini wa dini hiyo wapate fursa ya kusherehekea siku hiyo na familia zao kama zilivyo sikukuu nyingine.

Mapema Mratibu Mkuu wa Kongamano hilo, Sheikh Khalid Ali Mfaume, alisema lengo la maadhimisho hayo ni kuwakumbusha waislamu wajibu wao wa kujua tarehe za uislamu.

Alisema, Sheria namba 4 ya Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar ndio iliyowezesha kufanyika kongamano hilo pamoja na shughuli nyingine zilizoandaliwa.
Sheikh Khamis Abdulhamid akiwasilisha mada kuhusiana na Sensa na Mipango ya Maendeleo wakati wa Kongamano la Kuukaribisha Mwaka Mpya wa Kiislam 1444. A.H, lililofanyika katika Masjid Jamiu Zinjibar Mazizini Unguja leo.

Akitoa mada kuhusu sensa na uislamu, Sheikh Khamis Abdulhamid, alisema sensa imetajwa ndani ya Quran na uislamu haukatazi watu kuhesabiwa kwani ni muhimu kwa sababu inasaidia kupanga maendeleo ya baadae.

Alisema, sensa maana yake ni kujua idadi ya watu na makazi yao na namna walivyo katika maendeleo ya kiuchumi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi akifuatilia Mada ya Uislamu na Sensa na Mipango wa Maendeleo ikiwasilishwa na Sheikh Khamis Abdulhamid (hayupo pichani) wakati wa Kongamano la Kuukaribisha Mwaka Mpya wa Kiislam -1444 A.H, lililofanyika katika Masjid Jamiu Zinjibar Mazizini Unguja na kulia kwa Rais ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba,Sheria Utumishi na Utawala Bora Zanzibar,Mhe.Haroun Ali Suleiman, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar , Alhaj Othman Masoud Othman na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Alhaj Hemed Suleiman Abdulla na kushoto kwa Rais ni Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Mahmoud Mussa Wad na Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Hassan Othman Ngwali.

Kongamano hilo pia lilihudhuriwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Massoud Othman, Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdalla na viongozi wengine wa vyama na serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news