Rais Dkt.Mwinyi:Ukodishaji visiwa vidogo una manufaa mengi

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi amesisitiza kuwa, ukodishaji katika visiwa vidogo vidogo hapa nchini unafanyika kwa kuhakikisha Serikali inanufaika kutokana na uwekezaji mkubwa, kodi pamoja na wananchi wa maeneo husika kuwekewa mazingira mazuri zaidi katika shughuli wanazofanya.

Dkt. Mwinyi ametoa ufafanuzi huo Ikulu jijini Zanzibar leo katika mkutano na waandishi wa habari wa kila mwezi, kufuatia kuwepo kwa malalamiko na upotoshaji kutoka kwa wanasiasa pamoja na mitandao ya kijamii.

Amesema, Serikali ya Awamu ya Nane imefaya mabadiliko katika utaratibu wa kukodisha visiwa hivyo tofauti na ilivyokuwa zamani, ambapo hivi sasa kipaumbele hutolewa kwa kuzingatia aina ya mradi, fedha zitakazotangulizwa na mwekezaji, pamoja na namna ambayo wananchi watajengewa mazingira bora ya shughuli wanazofanya katika eneo husika.

Amesema, Serikali inahitaji uwekezaji mkubwa na kutolea mfano wa kisiwa cha Kwale kilichowekezwa kwa Dola Milioni 80, na akibainisha kuwa zaidi ya Dola Milioni 400 zimetumika katika uwekezaji wa visiwa vidogo vidogo 10.

Amewataka wananchi walioko katika maeneo ya visiwa hivyo kuondoa wasiwasi kwani watawekewa mazingira bora zaidi ya kufanyia shughuli zao.

“Serikali ina dhamira njema na mipango mizuri katika kuwahudumia wananchi,"amesema Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi. Akigusia suala la Mji Mkongwe, Dkt. Mwinyi amesema, Serikali inalazimika kuyahami majengo yaliochakaa katika eneo hilo kwa kuwa na utaratibu wa kuyatenegeneza kupitia kwa wananachi wenye uwezo na kusisitiza matengenezo hayo kuzingatia asili ya muindo wake.

Aidha, ameeleza kuwa serikali inahitaji kuwa na viwanja vya kisasa vya michezo au vile vyenye sura za Akademia.

Dkt.Mwinyi amewataka viongozi wa Shirika la Baishara Zanzibar (ZSTC) kuzingatia wajibu walionao katika kuliimarisha zao la Karafuu ili liweze kuleta manufaa kwa Taifa pamoja na wananchi (wakulima).

Sambamba na hilo Dkt.Mwinyi amesema, wakati umefika sasa wa kuhakikisha Mji Mkongwe unakuwa katika hali ya usafi pamoja na huduma zote za kijamii ikiwemo maji safi na salama pamoja na umeme kupatikana , ili kuleta ustawi wa sekta ya Utalii.

Mkutano huo ni mfululizo wa utaratibu wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi wa kukutana na waandishi wa vyombo vya habari nchini na kuzungumzia mamabo mbalimbali yanayolihusu Taifa.

Post a Comment

0 Comments