Sababu zinazochochea wivu wa mapenzi unaoleta madhara katika jamii

NA MWAHIJA ZIMBWE-SJMMC

MWANDISHI wa nyimbo, mashairi na nguli wa riwaya nchini Canada, Bw.Leonard Norman Cohen katika moja ya maandiko yake amewahi kuandika,"Mapenzi hayana tiba, lakini ndiyo dawa pekee ya magonjwa yote". (Rejea,The Nature of Love in the Work of Leonard Cohen).
Picha na dreamstime.

Ni wazi kuwa, mapenzi hujengwa na hisia, zinazowaunganisha watu wawili kwa maana ya mwanamke na mwanaume wanaoamua kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na mwisho wa siku wengine huishia kuanzisha familia kabisa. 

Mbali na uhusiano huo ambao umekuwa ukijengwa kila siku duniani kote, bado tafiti na taarifa mbalimbali za habari zimekuwa zikionesha namna ambavyo kumekuwa na matukio mengi ya ukatili na mauaji ya kutisha yanayotokana na wivu wa kimapenzi.

Vijana wengi wadogo ndio wahanga wakubwa katika suala hili, suala la wivu katika mapenzi ni jambo la kawaida, lakini wivu ukizidi au wivu uliokithiri unaweza kusababisha athari mbalimbali katika jamii kama vile vifo na ulemavu wa kudumu.

Mathalani, kupitia takwimu za hivi karibuni za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, mauaji kati ya wapenzi yanaongezeka hasa kutokana na wivu wa kimapenzi. Mfano takwimu zinaonesha asilimia 82 ya waliouawa mwaka 2017 walikuwa wanawake na asilimia 12 walikuwa wanaume. 

Ili kufahamu chanzo cha hayo yote, DIRAMAKINI ilizungumza na baadhi ya wananchi mbalimbali jijini Dar es Salaam ambao wameeleza sababu zinazochangia wivu katika mapenzi.

Mwajuma Salimu mkazi wa Kijitonyama ameeleza kuwa, sababu mojawapo inayopelekea wivu wa kimapenzi ni ukosefu wa elimu juu ya suala zima la mahusiano.

Hawana elimu

Anasema, vijana wengi wamekua wakiingia katika mahusiano bila kuwa na elimu juu ya suala hilo huku akitolea mfano kwamba, vijana wanatakiwa kufahamu kuwa katika mahusiano kuna changamoto mbalimbali kama vile usaliti ambapo kijana anapokutana na changamoto kama hiyo inampelekea moja kwa moja kuwa na wivu wa kimapenzi.

"Hivyo kupelekea kufanya maamuzi magumu kama kutekeleza mauaji. Hivyo elimu itolewe kwa vijana ili waweze kujikinga na wivu uliokithiri katika mapenzi,"anasema Mwajuma.

Umri mdogo

Naye Bw.Issa Makala ambaye ni mkazi wa Makumbusho jijini Dar Salaam amezungumzia pia juu ya sababu inayoweza kupelekea wivu wa kimapenzi ambapo amezungumzia suala la mapenzi katika umri mdogo.

Amesema, vijana wanapoingia katika mapenzi wakiwa katika umri mdogo hupelekea wivu kutokana na kwamba wanakuwa hawana ukomavu,"hawana ukomavu katika kuchanganua mambo mbalimbali katika mahusiano, hivyo hupelekea wivu uliokithiri katika mapenzi unaopelekea athari mbalimbali katika jamii,"anasema.

Mwanasaikolojia

Masozi Isam ambaye ni mwanasaikolojia katika Taasisi ya Kujitegemea ya Furahia Maisha naye pia ameeleza sababu zinazoweza kupelekea wivu katika mapenzi ambapo moja ya sababu ni simu za mkononi ambazo zinahusisha mitandao mbalimbali ya kijamii kama vile Faceebok, Instagram na Whatsapp.

Isam anasema, wenza wanaposhikiana simu hupelekea wivu kutokana nakwamba huweza kukutana na vitu ambavyo si vizuri kwa yeye kuona kama vile message ambapo mwenza wake anaweza kuwa anatumiana na watu wengine na hivyo kupelekea wivu kwa mwenza wake.

Lakini pia sababu nyingine anasema, ni wazazi kuchagulia watoto wenza wao, hivyo unakuta mtu amechaguliwa na wazazi mwenza wake hivyo kunakua hakuna mapenzi ya dhati kati ya wawili hao.

Mwanasaikolojia huyo anasema kuwa, hali hiyo hupelekea wenza hao kutoaminiana na kufikiriana vibaya na kupelekea kuwa na wivu wa kimapenzi kati yao kwa sababu uaminifu unakosekana kabisa baina yao na hapo ndipo ugomvi unapoanzia na kuleta athari za kimwili na kisaikolojia kwa ujumla.

Viongozi wa dini

Juma Mwenda ambaye ni mmoja wa viongozi wa dini katika msikiti wa Akachube uliopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam amelezea pia sababu moja wapo inayoipelekea wivu wa kimapenzi ni kuporomoka kwa maadili katika mahusiano.

Ametolea mfano mmoja kuwa ni mwenza anaweza kuanzisha tabia ambanzo zitampelekea mwenza kumuhisi vibaya mfano dharau au kumnyima mwenza wake tendo la ndoa, jambo ambalo linaweza kumfanya kujihisi anasalitiwa na hivyo kupelekea wivu huo kwa mwenza wake, hivyo wenza wanapaswa kuelewana na kuwa na maadili mazuri kati yao ili kuepuka madhara yanayotokana na wivu wa kimapenzi 

Nay Ian Etiene ambaye ni kiongozi wa dini katika Kanisa la Betheli Mikocheni jijini Dar es Salaam amesema, sababu inayoweza kupelekea wivu katika mapenzi ni misingi mibovu katika mapenzi ambapo vijana wengi wamekuwa wakijihusisha katika mahusiano kwa nia ya kujiridhisha kingono na sio kwa mapenzi ya dhati.

Amesema,ongezeko la wivu linazidi kuongezeka kutokana na kwamba mmoja kati yao anaweza kuwa ana mapenzi ya dhati kwa mwingine, lakini mwingine akawa hana hivyo kupelekea matukio ya kikatili kutokana na wivu uliokithiri katika mapenzi.

Wakati huo huo, suala la mahusiano bora ni muhimu kupatiwa ufumbuzi ili kuepuka athari zinazotokana na wivu wa kimapenzi kama vile vifo, ni jukumu la jamii, Serikali na vyombo visivyokuwa vya kiserikali wakiwemo viongozi wa dini kuhakikisha wanafanya jitihada zozote zile ili kuweza kukabiliana na tatizo hili.

Pia elimu itolewe kwa vijana ili waweze kufahamu changamoto zilizopo katika mahusiano ili waweza kujizuia kuwa na wivu mbaya na uliokithiri unaoweza kuleta madhara katika jamii. 

Aidha, ingawa hakujato bado hamna takwimu rasmi za kitaifa katika siku za karibuni, takwimu za Jeshi la Polisi za zilizotolewa Julai, 2021 zilionesha katika kipindi cha miezi miwili tu Mei hadi Juni, 2021 mauaji yalikuwa 275 na kati ya hayo mauaji ya wivu wa mapenzi yalikuwa 21. 

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini (LHRC) kiliwahi kukusanya matukio makubwa ya aina hiyo katika miaka ya hivi karibuni. 

Mfano, mwaka 2017 LHRC kilikusanya matukio makubwa 13 na mwaka 2020 matukio yaliongezeka mpaka 39 yaliyotokana na wivu wa kimapenzi. 

Hata hivyo, kituo hicho kinasema mwezi Mei pekee 2022, kumeripotiwa matukio saba ya mauaji yatokanayo na wivu wa kimapenzi huku mwaka 2021 kuliripotiwa kuwa na mauaji ya aina hiyo 35, ambapo wanaume waliouawa walikuwa wanne na wanawake 31.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news