Serikali yatoa wito kwa wadau wanaotoa Elimu Jumuishi

NA MWANDISHI WyEST

WITO umetolewa kwa viongozi wa taasisi na wadau wanaojishughulisha na utoaji wa Elimu Jumuishi, kuendelea kushirikiana na Serikali katika kujenga shule kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Wito huo umetolewa jijini Arusha na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omari Kipanga (Mb) wakati akizindua rasmi Shule Jumuishi ya Mfano ya Sekondari Patandi.
Amesema shule hiyo imejengwa na Serikali kupitia Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) kwa gharama ya zaidi ya Sh. bilioni 3.8 na mpaka sasa ina jumla ya wanafunzi 288 wakiwemo 217 wenye mahitaji maalum na 72 wasio na mahitaji maalum.
"Serikali inatambua kuwa pamoja na kuwa na mfumo wa Elimu Jumuishi, bado kuna wanafunzi wenye mahitaji maalum ambao hawawezi kutumia mfumo huo kutokana na changamoto walizo nazo hivyo ni muhimu kuweka msukumo zaidi katika kuimarisha mifumo tofauti ya ufundishaji kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kama vile shule maalum na vitengo," ameongeza Mhe. Kipanga.

Prof. Carolyne Nombo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu amewashukuru wazazi kwa kuwapeleka watoto wenye mahitaji maalum katika shule hiyo ili kupata Elimu.
"Naendelea kuwatia moyo na kuwapongeza wazazi kutoka sehemu mbalimbali nchini kwa kuwaleta watoto kuja kupata elimu katika shule hii jumuishi ya Patandi," amesema Prof. Nombo.

Naye Dkt. Charles Msonde, Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI amesema Wizara yake imeleta walimu bora na mahiri kuja kufundisha shuleni hapo na ameahidi kuzifanyia kazi changamoto zote ambazo zipo katika shule hiyo ili kuendelea kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji shuleni hapo."Kazi ya walimu hawa inaonekana wazi ilivyo bora kwa jinsi wanavyowapa watoto hawa maarifa, ujuzi na stadi kwa nadharia na vitendo. Naamini baada ya miaka minne tutashuhudia makubwa sana kutoka kwa watoto hawa," amesema Dkt. Msonde

Akifafanua kuhusu shule hiyo, Dkt. Magreth Matonya, Mkurugenzi wa Elimu Maalum, Wizara ya Elimu amesema shule hiyo sio maalum bali ni jumuishi kwa kuwa inachukua wanafunzi wenye mahitaji maalum na wasio na mahitaji maalum.
"Ukisema shule maalum ina maana inachukua watoto wa aina moja tu yaani wenye mahitaji maalum, lakini shule hii ni jumuishi inachukua na wasio na mahitaji maalum ili wote waweze kusoma kwa pamoja,"ameongeza Dkt. Matonya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news