TANZIA:Mwanahabari Dkt.Gideon Shoo afariki, fahamu kwa nini alikipenda kilimo hai

NA DIRAMAKINI

MWANAHABARI nguli na mkongwe wa siku nyingi Dkt.Gideon Shoo ambaye pia alikuwa mchambuzi wa masuala mbalimbali ya kisiasa, kijamii na kiuchumi ndani na nje ya Tanzania amefariki.

Kwa mujibu wa taarifa za awali zilizoifikia DIRAMAKINI zinaeleza kuwa, Dkt.Shoo amefariki leo Julai 9, 2022 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salam.

Wakati wa uhai wake,Dkt.Shoo amewahi pia kuwa miongoni mwa wamiliki wa vyombo vya habari nchini na mshauri wa masuala yahusuyo tasnia hiyo.
Dkt.Gideon Shoo wakati wa uhai wake.

Kilimo hai

Miaka kadhaa, Dkt.Shoo aliamua kuingia katika kilimo hai cha kisasa ambacho hakitumii dawa za kemikali kutoka viwandani. Dkt.Shoo alikuwa anafanya kilimo hicho nyumbani, kwenye shamba lake lililopo Kata ya Kerege wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani.

Wakati wa uhai wake, akizungumza wakati alipotembelewa shambani na nyumbani kwake na maofisa kutoka Envirocare, asasi isiyokuwa ya kiserikali inayojihusisha na mazingira, haki za binadamu alisema kilichomhamisha kuingia kwenye shughuli hiyo ni kutokana na kukulia kwenye kilimo.

‘’Kingine kilichonivuta zaidi ni kwamba nimestaafu. Ni kwamba nimestaafu kwa maana ya pilikapilika, kustaafu kwenyewe labda ni sababu ya umri. Tangu nimeondoka kwenye ajira rasmi mwaka 1987 kwenye magazeti ya Uhuu na Mzalendo sijawahi kuwa tena kuwa kwenye na ajira rasmi. 

"Nimekuwa nikifanya shughuli zangu mwenyewe. Hata pale watu wanadhani nimekuwa kwenye ajira. Hapana shughuli zangu nazifanya mwenyewe.Nikasema mimi nadhani sasa nipumzike, lakini kupumzika lazima nipate shughuli ya kufanya, shughuli hii nilibuni siku nyingi nilikuwa nasubiri tu wakati wa kutekeleza. Shughuli hii nilibuni mwaka 1993 hadi 1994 nikiwa na malengo labda mwaka 2000 nitakuwa nimeanza, lakini haikuwa hivyo hatimaye nilianza mwaka jana (2014) na nikafanikiwa kuhamia huku,"alisema Dkt.Shoo wakati huo. 

Alisema kabla ya kuhamia hapo tayari alishapanda miti ya matunda ya kudumu. "Nilipanda miti kwa ajili ya kilimo chenyewe na miti yenyewe ni miarobaini na mirusina.Mwarobaini ni dawa na umekuwa ukitumika kwa kilimo nchini India tangu kabla ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo na hakuna haja ya kufanya utafiti kwa sababu Wahindi tayari walishaufanya,"alisema Dkt.Shoo wakati wa uhai wake.

Alisema, Wahindi walifanya utafiti kwa miaka mingi sana kiasi kwamba unapozungumzia kilimo cha kisasa cha kutotumia dawa za kuuwa wadudu za viwandani hakuna haja ya kufanya utafiti mwingine kwani walishamaliza.

"Mwarobaini mbegu yake inatoa mafuta ambayo yana uwezo wa kuuwa wadudu na magonjwa aina 600 kwa kiasi kikubwa uchanganyaji wake ni rahisi tu. Mafuta unachanganya na sabuni ya unga kidogo na kupulizia kwenye mmea bila matatizo yeyote. Kwa hiyo mwarobaini ni mti ninaupenda na niliupanda kwa miaka mingi nikiwa na malengo hayo.

"Mwarobaini unachofanya ni kufubaza wadudu wasiwe na uwezo tena wa kufanya madhara na pia wakati huo huo majani yake yanatumika kuuwa vijidudu vilivyoko kwenye udongo. Kwa hiyo nimehamasika na nakifanya kilimo hiki nikiwa na imani kwamba nitapata mafanikio na watu wengine wanaweza kuiga,"alisema Dkt.Shoo wakati huo. 

UONGOZI WA DIRAMAKINI UNAWAPA POLE NDUGU JAMAA NA MARAFIKI KWA KUONDOKEWA NA MPENDWA WAO DKT.GIDEON SHOO, MWENYENZI MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU MAHALI PEMA. TAARIFA ZAIDI ZITAENDELEA KUKUJIA KUPITIA DIRAMAKINI.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news