Sensa ya Watu na Makazi ilivyobeba majibu ya ustawi bora wa maisha yetu-2

NA GODFREY NNKO

"Sisi Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza kwa ushirikiano wa pamoja na viongozi wote tumepokea maagizo ya Mufti na tumeanza kuyatekeleza kwa kutoa mwongozo wa namna ya kufikisha elimu ya Sensa kwa waumini kupitia nyumba zetu za ibada,"amesema Sheikh Kabeke.

Sheikh Kabeke amesema waumini wa dini ya kiislamu na wananchi kwa ujumla wanapaswa kuhesabiwa kwenye zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ili kupata takwimu sahihi zitakazosaidia Serikali kupanga mipango ya maendeleo kwa ufanisi. Endelea...

Jaji Mkuu

Naye Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe.Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema, Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti 23, 2022 itaisaidia Mahakama ya Tanzania kupanga upya mpango wa ujenzi wa miundombinu, ikiwemo ujenzi wa Mahakama mbalimbali hapa nchini.

Mhe.Prof.Juma ameyasema hayo katika ziara yake ya kikazi ya Mahakama, Kanda ya Tanga hivi karibuni alipokuwa akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Mhe.Kalisti Lazaro ofisini kwake.

Katika mazungumzo hayo, Jaji Mkuu ameainisha vipaumbele vinne, ikiwemo idadi ya watu na wingi wa mashauri, vinavyotumiwa na Mahakama ya Tanzania kubaini maeneo ya ujenzi wa miundombinu, hususani Mahakama za Mwanzo na wilaya.

“Kama mnavyofahamu mwaka huu tutakuwa na sensa ya watu. Kwetu kama Mahakama ni zoezi muhimu sana kwa sababu linatupa mahesabu mapya ya watu na maeneo mbalimbali ambayo yanahitaji huduma.

"Lengo la sensa ni kusogeza huduma, hivyo tutasubiri matokeo hayo ya sensa ili yatusaidie katika Mkoa huu wa Tanga, kwa mfano, tunapotaka kujenga Mahakama ni sehemu gani ambayo pengine idadi ya watu imeongezeka na sehemu gani ambayo inazalisha mashauri mengi,”amesema.

Makamu wa Pili

Makamu wa Pili wa Rais, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe.Hemed Suleiman Abdullah ameeleza kuwa, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga kufanya ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kwa njia ya kidijitali ambapo itarahisisha ukusanyaji wa taarifa wakati wa zoezi hilo.

Amesema kuwa, sensa ya mwaka huu itaendeshwa kwa mifumo ya KI-TEHAMA ambapo itakuwa ni mara ya kwanza kwa nchi kuwa na mfumo mpya utakaongeza ufanisi.

“Sensa ya mwaka huu ni ya sita itakayobebwa na upekee wa aina yake kwani inaunganisha matukio mawili makubwa ya kitaifa ikiwemo la ukusanyaji wa taarifa za majengo yote nchini pamoja na taarifa za idadi ya watu,” alieleza.

Aidha, alisema hadi sasa maandalizi yake yamefiki asilimia 87 na hii inaonesha ni hatua nzuri kwa taifa hivyo watu waendelee kupewa elimu kwa wingi.

“Kuhesabu watu kitaalam itasaidia kupata taarifa kwa urahisi, na kazi hii itafanyika kwa umakini mkubwa hivyo tuifanye kwa weledi na viwango vinavyotakiwa,”aliongezea Mhe. Abdallah

Sambamba na hilo alitoa rai kwa wakufunzi hao kuendelea kuzingatia uzalendo katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Wahitimu wetu wote zingatieni uzalendo na muwe vielelezo vizuri kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha wananchi kujitokeza katika zoezi hili la sensa ili kuleta matokeo makubwa,”alisisitiza.

Wizara ya Fedha

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.Hamad Hassan Chande alisema kuwa, zoezi la sensa ya watu na makazi ni nyenzo muhimu kwa kuzingatia tija iliyopo hususani katika masuala ya mipango ya maendeleo ya nchi yetu kwa kuzingatia uwepo wa bajeti yenye kukidhi mahitaji yaliyopo.

“Matokeo ya sensa ya mwaka 2022 yatatoa mwelekeo mzima wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe.Samia Suluhu Hassan kuhusu utekelezaji wa ahadi zilizotolewa kwa wananchi wetu kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025, na matokeo haya ni nyenzo muhimu kwa wizara yangu kwani yatasaidia kufuatilia utekelezeaji wa bajeti katika sekta zote,”alisisitiza.

NGOs

Aidha, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imekutana na Viongozi wa Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali (NGOs) mkoani Dodoma kuzungumzia maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi.

Akizungumza na washiriki wa mkutano huo, Kamisaa wa Sensa, Mhe.Anne Makinda amesema NGOs ni wadau muhimu sana katika kufanikisha sensa, kwani wanafanyakazi na wananchi na wapo karibu na jamii.

“Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali ni wadau wakubwa sana katika kufanikisha Sensa ya Mwaka 2022. Ninyi kama viongozi wa NGOs, katika shughuli zenu za kila siku mkahamasishe wananchi washiriki kwenye Sensa ili Serikali ipate takwimu zitakazosaidia kupanga mipango ya maendeleo,”amesema Kamisaa wa Sensa.

Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt.Albina Chuwa amesema, NGOs ni miongoni mwa makundi ambayo NBS itashirikiana nao kwa ukaribu ili kuhakikisha elimu ya umuhimu wa Sensa inawafikia wananchi wote.

Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Baraza la NGOs, Dkt. Lilian Badi amesema, Baraza la NGOs lipo tayari kutoa elimu ya sensa na kuhakikisha kwenye shughuli za kila siku za wanachama, elimu ya sensa inatolewa.

Wasioona

Kwa upande wake Chama cha Wasioona Tanzania (TLB) Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam kimesema kuwa, wapo tayari kuhesabiwa kupitia Sensa ya Watu na Makazi.

Bw.Protase Mutakyanga ambaye ni Katibu wa chama hicho Wilaya ya Temeke ameyasema hayo kupitia mahojiano maalum na DIRAMAKINI yaliyofanyika katika ofisi za chama hicho zilizopo Mbagala katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam.

"Na sisi wasioona, tupo tayari kuhesabiwa kwa maendeleo yetu na Taifa, kwa hiyo Sensa ya Maendeleo na Makazi tunaisubiria na tumeshajiandaa kwa hilo,"amesema.

Mbali na hayo, Bw.Mutakyanga amesema, wanaandaa mpango wa kufanya mkutano ili kuwahamasisha wanachama wa chama hicho na wananchi wote washiriki kwa ufanisi mkubwa katika zoezi hilo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

"Sisi chama cha watu wasioona Tanzania, tunatambua kuwa ni sehemu ya wananchi wa Tanzania na ni wajibu wetu kuhesabiwa ili Serikali iweze kuweka sawa mipango yake ya maendeleo.

"Hivyo, kama chama tunaandaa mpango wa kuandaa mkutano ili kuhamasisha wanachama wetu washiriki katika Sensa ya Watu na Makazi na pia kuhamasisha jamii inayokaa na wanachama wetu kuondoa dhana kwamba watu wenye ulemavu ni wa kufichwa ndani.

"Tunazo taarifa za wanajamii ambao wana mtazamo hasi ambao kwanza wao kama wao hawapendi kuhesabiwa, wakiamini kwamba wao ni peke yao wanapaswa kuwatimizia mahitaji yao, jambo ambalo halina ukweli wowote. Ili Serikali iweze kutekeleza mipango yake kwa manufaa ya wananchi inapaswa kufahamu idadi ya watu ambao inapaswa kuwahudumia, na huko ndiko tunakoelekea Agosti 23, 2022." amesema.

Aidha, chama hicho kimetoa ombi kwa wadau mbalimbali nchini wajitokeze kukisaidia fedha shilingi milioni nne kwa ajili ya kuandaa mkutano wa kutoa elimu kwa wanachama wao na jamii kwa ujumla kuongeza ufanisi wa ushiriki katika Sensa ifikapo Agosti 23, mwaka huu.

"Tunaandaa mkutano pale tutakapopata mdau wa kutusaidia kama milioni nne hivi, kusudi tuweze kuandaa mkutano wa wanachama wetu wote ili tuweze kutoa elimu ya namna gani wanachama wetu waweze kushiriki kwenye zoezi la Sensa ya Watu na Makazi,"amesema Mutakyanga.

HGWT

Rhobi Samwelly ni Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) naye ametoa rai kwa Watanzania wote kushiriki kikamilifu kuhesabiwa katika Sensa ya Watu na Makazi ili kuiwezesha Serikali kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo.

Rhobi amesema, Watanzania wote wana wajibu wa kuhesabiwa katika kuiwezesha serikali kupata takwimu sahihi ambazo itazitumia kupanga mipango ikiwemo ya afya, uchumi, miundombinu, elimu, huduma za jamii na kupeleka maendeleo kwa wananchi kwa manufaa yao,jamii na taifa kwa ujumla.

"Asiwepo mtu yeyote atakayeachwa bila kuhesabiwa Agosti 23, mwaka huu. Serikali ina dhamira njema sana ya kuendelea kufikisha Maendeleo kwa wananchi, ili izidi kufanikiwa zaidi lazima iwatambue Watanzania wote. Hivyo sensa ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu.

"Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan na viongozi mbalimbali wa Serikali wameendelea kutoa msisitizo juu ya mwitikio chanya wa kila mtanzania kuhesabiwa siku hiyo. Naomba Watanzania kuzingatia maelekezo hayo muhimu kufanikisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi liweze kuwa na ufanisi mkubwa kwa ustawi wa nchi yetu," amesema.

Pia, Rhobi amewaomba viongozi wa dini, na wenye nafasi mbalimbali katika jamii kuendelea kutoa elimu kwa wananchi katika maeneo yao juu ya umuhimu wa sensa, kwani jambo hilo ni Muhimu sana lazima liendelee kuzungumzwa mara kwa mara, kusudi siku ikifika Watanzania wote wahesabiwe.

Wafanyabiashara

Nao wafanyabiashara nchini wameshauriwa kufanyia kazi wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan wa kusaidia kuweka matangazo ya nembo ya Sensa ya Watu na Makazi kwenye bidhaa mbalimbali ili kuhamasisha zoezi hilo nchi nzima.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Sensa ambaye pia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Dkt. John Jingu ameyasema hayo jijini Dar es Salaam hivi karibuni alipokutana na wawakilishi wa sekta binafsi na wafanyabiashara kuelekea katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi.

Amesema, licha ya maandalizi hayo kufika asilimia 80, kazi ya kukamilisha na kufanikisha zoezi hilo kwa asilimia zote 100 inaendelea sehemu mbalimbali nchini bila kuchoka.

"Sensa hii itakuwa ni sensa ya sita tangu nchi yetu ilivyoanza, hivyo ni jambo kubwa ambalo linafanyika kila baada ya miaka 10 na mwaka huu tuna bahati ya fursa ya kufanya sensa ya kitaifa,"amesema Dkt.Jingu.

Kwa upande wake Mwenyekiti Mwenza kutoka Zanzibar, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Thabit Faina amesema suala la uhamasishaji wa sensa linakwenda vizuri kwa kiasi kikubwa na sasa wamebakisha hatua ndogo ya asilimia 20.

Faina amesema, matarajio yao ni kuona wapi panahitaji huduma ya afya, kujenga shule mpya, kuwekeza aina ya biashara mbalimbali katika maeneo tofautitofauti.

Akizungumza kwa niaba ya Sekta Binafsi, Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini, Paul Makanza amesema kupitia zoezi hilo la sensa, sekta binafsi itafaidika na takwimu hizo za idadi ya watu na makazi na kuzifanyia kazi ipasavyo hususani katika Sekta ya Biashara kulingana na uhusiano wa sekta hiyo na idadi ya watu.

Vyombo vya habari

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Abdulla ameiagiza Idara ya Habari (MAELEZO) kwa kushirikiana na vyombo vya habari hapa nchini kushirikiana kutoa elimu ya sensa ya watu na makazi ili wananchi waweze kuelewa lengo na faida ya sensa hiyo kwao binafsi na kwa Taifa.

“Naiagiza Idara ya Habari (MAELEZO) kushirikiana na Ofisi ya Takwimu pamoja na wanahabari kutoa elimu ya sensa kwa Watanzania ili waweze kutoa taarifa sahihi wakati wa kuhesabiwa,”amefafanua Naibu Katibu Mkuu.

Aliendelea kusema kuwa, vyombo vya habari vitoe elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kutoa taarifa sahihi wakati wa sensa, kwani utoaji wa taarifa sahihi ni jambo muhimu sana katika sensa, ambapo ikiwa taarifa zitakazokusanywa zitakuwa sahihi maana yake kutakuwa na Sera na Mipango sahihi ya maendeleo ya nchi kwa ujumla.

“Serikali inapokuwa na takwimu sahihi itafanya maamuzi sahihi ambayo yataakisi hali iliyopo ya watu wake na mazingira wanayoishi,”alifafanua Naibu Katibu Mkuu huyo.

Aidha, amevitaka vyombo vya habari kuwa na angalau na kipindi kimoja kwa wiki kinachozungumzia sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 pamoja na masuala muhimu yatakayomfanya mwananchi kujiamini na kushiriki vyema katika sensa hiyo.

Kwa upande wake, Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Mhe.Anne Makinda amevipongeza vyombo vya habari kwa namna vinavyoshiriki kutoa elimu ya sensa kwa wananchi kupitia vipindi mbalimbali vya redio, televisheni, mitandao ya kijamii pamoja na habari na makala kupitia magazeti mbalimbali.

“Sisi wenyewe tusingeweza kufika maeneo yote ya Tanzania, lakini kupitia vyombo vyenu vya habari mmeweza kuwafikia asilimia kubwa ya Watanzania, ambapo mmetoa elimu kwa makundi yote ya Watanzania, kama vile wakulima, wafugaji, vijana, wazee na watu wenye ulemavu,"amefafanua Kamisaa Makinda.

Miss Tanzania

Miss Tanzania kwa mwaka 2022, Halima Kopwe naye ametoa rai kwa Watanzania wote kujitokeza kwa dhati kushiriki kuhesabiwa Agosti 23, mwaka huu ambapo zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litafanyika ambapo amesema sensa ina umuhimu mkubwa kwa uchumi na maendeleo ya nchi.

"Mimi kama Halima Kopwe nimejiandaa kuhesabiwa, nitaungana pamoja na Serikali na Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ili niweze kuhesabiwa mwezi wa nane mwaka huu.

"Nawahamasisha Watanzania wenzangu wote pia wajiandae kuhesabiwa, itatusaidia sana kwenye uchumi wa nchi yetu. Mimi ni Halima Kopwe Miss Tanzania 2022 nimejiandaa kuhesabiwa,"amesema Halima Kopwe.

Sensa ya Makazi

Kwa upande wake, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imesema kuwa, Sensa ya Watu na Makazi Agosti 23, 2022 nchini imebeba uzito wa kipekee ikizingatiwa kwamba, kwa mara ya kwanza tangu tupate Uhuru tunakwenda kufanya sensa ya makazi (majengo) nchini.

Hayo yamebainishwa na Deogratius Kalimenze ambaye ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

"Lengo la sensa hii ni kutaka kufahamu gharama za ujenzi zinazotumika kuendelea majenzi nchini na mchango wa Serikali na sekta binafsi katika uwepo wa nyumba za makazi na matumizi mengineyo.

"Na jambo la pili msingi wake unajikita kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo sisi sote tunaitekekeza ibara ya 76 ( d) ambayo kimsingi inaitaka wizara kutambua na kuandaa kanzi data ya nyumba zote nchini kwa kushirikiana na wadau na kuweza kuimarisha uhusiano kati ya wapangaji na wamiliki wa majengo nchini.

"Kwa hiyo, huo ndio msingi ambao umesukuma Serikali kuweza kufanya kwa mara ya kwanza tangu tupate uhuru Sensa ya Majengo nchini.Yako mambo mbalimbali ambayo ni faida zitakazotokana na faida ya sensa."

Faida

"Kwanza kabisa kupata takwimu ambazo zitasaidia sisi kuwa na kanzi data ya majengo yetu nchini na aina mbalimbali za matumizi ya hayo majengo, pili kuiwezesha Serikali kufanya mapitio na maboresho ya sheria, kanuni, sera na programu mbalimbali ambazo zinasimamia sekta ya uendelezaji wa nyumba na makazi nchini.

"Tatu, kuiwezesha Serikali kupata taarifa za matumizi ya majengo mbalimbali nchini kama ni mangapi yanatumika kwa makazi, biashara, huduma mbalimbali za jamii ikiwemo shule, vituo vya afya, hospitali, vituo vya polisi na kadhalika.

"Jambo la nne ni kuiwezesha Serikali kujua mchango wake katika upatikanaji wa nyumba za makazi nchini kama inavyoelekezwa na Sera ya Maendeleo ya Makazi.

"Na hapa tunafahamu kwamba ujenzi wa nyumba au majengo nchini unafanywa na taasisi za Serikali, Serikali yenyewe pamoja na watu binafsi, lakini hatuwezi kusema kwa uhakika mchango wa Serikali katika ujenzi wa nyumba ni kiasi gani, lakini kutokana na mchango wa sensa tutaweza kutambua na kujua mchango wa Serikali katika majenzi ni kiasi gani,"amesema Mkurugenzi huyo.

Amefafanua kuwa, jambo la tano, ni kuiwezesha Serikali kufanya tathmini ya kiwango cha nyumba zilizojengwa maeneo yaliyopangwa, maeneo ambayo hayajapangwa na uwiano wa upatikanaji wa huduma za jamii katika majengo hayo.

"Na hapa kwa kipindi kirefu tumekuwa tunasema kwamba Tanzania zaidi ya asilimia 70 ya wakazi wake wanaishi katika maeneo yasiyopangwa, lakini kuna programu ya urasimishaji imefanyika karibu nchi nzima na kuna faida nyingi zimejitokeza kwa hiyo katika zoezi hili tutakwenda sasa kutambua ni kiwango gani makazi yetu yapo yaliyopangwa na ambayo hayajapangwa mpaka sasa,"amesema.

Bw.Kalimenze anataja jambo la sita kuwa ni kuiwezeaha Serikali kutambua hali ya uendelezaji wa miji katika ujenzi uliopo kama maghorofa, majengo ya kawaida na mambo mengine, na kujua sifa za hayo majengo yanayozungumziwa ni ya aina gani.

"Ambapo katika utekelezaji wa sensa ya majengo tunakwenda kupata viashiria mbalimbali vya utekelezaji wa malengo endelevu ambayo lengo namba 11 linataka tuwe na miji ambayo ni jumuishi,salama na stahimilivu na endelevu katika nchi zote ulimwenguni na katika kutekeleza sensa hii kuna viashiria vingi ambavyo tunaweza kupata majibu yake na kujipima utekelezaji wa malengo haya endelevu,"amesema.

Aidha, jambo la nane, Bw.Kalimenze amesema ni kusaidia tafiti mbalimbali ambazo zinafanyika nchini katika masuala ya nyumba na uendelezaji wa miji.

Hatua

"Hatua ya kwanza kabisa ilikuwa ni uandaaji wa nyenzo kwa maaana ya madodoso na miongozo mbalimbali ya usimamizi ya makarani na wakufunzi kwa ajili ya kuendesha zoezi la Sensa ya Majengo na hili lilifanyika kuanzia Julai, mwaka jana na limeendelea mpaka mwezi huu ndipo tumekamikisha kuboresha nyenzo hizo baada ya kuwa tumefaya sensa ya majaribio na pre-test tena nyingine mwezi uliopita mwishoni,"amesema.

Anasema, hatua ya pili ilikuwa ni mafunzo kwa makarani ambao waliwatumia katika zoezi la sensa ya majaribio ambayo inatakiwa kwa mujibu wa sheria ya takwimu ifanyike mwaka mmoja kabla ya sensa haijafanyika na zoezi hilo lilifanyika.

"Hatua ya tatu, ni uandaaji wa mikakati ya uelimishaji na mkakati huu ulizinduliwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kule Dodoma mwaka jana na sisi wote kama wanahabari tunao wajibu wa kutumia mwongozo huu katika uhamasishaji na uelimishaji wa jamii kuhusiana na maandalizi ya sensa na sensa yenyewe,"amesema.

"Lakini sensa ya majaribio ilifanyika mwaka jana mwezi Septemba tarehe 8 hadi 19 na matokeo yake yakachambuliwa na kupata tathmini ya nyenzo zilizotumika na ubora wa nyenzo ili kupata takwimu sahihi kwa ajili ya sensa kuu ambayo itafanyika mwezi wa nane mwaka huu.

"Kazi zilizofanyika baada ya sensa ya majaribio na kuandaa rasimu sasa ni kuboresha miongozo na kuandaa majedwali ambayo yatatumika kutoa taarifa au uchambuzi wa takwimu zinazotokana na sensa ya majengo.

Usimamizi

"Usimamizi wa sensa ya majengo na sensa nyingine mbili ambazo nimezitaja ukoje? Kwanza tunayo Kamati Kuu ya Kitaifa ya Sensa ya Watu na Makazi ambayo Mwenyekiti wake ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa huku Mwenyekiti mwenza wa Kamati Kuu ya Kitaifa ya Sensa ya Watu na Makazi akiwa ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleman Abdulla.

"Pia tunayo Kamati ya Ushauri ya Kitaifa ambayo inaongozwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu ambaye ndiye Mwenyekiti wa kamati hiyo,"amesema.

"Tunazo ofisi zetu za Takwimu ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, nne tunazo kamati za sensa za kila mkoa ambazo zinaongozwa na waheshimiwa wakuu wa mikoa, hao ndio wasimamizi wakubwa wa zoezi hilo na pia tunazo kamati za sensa za wilaya na mwisho kabisa tunazo kamati za kata, mitaa,vitongoji na shehia kwa upande wa Zanzibar,"amesema Deogratius Kalimenze ambaye ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi.

Ameongeza kuwa, "pia tuna makamisaa wawili wa sensa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, lakini hapo katikati kuna sekretarieti ya Kitaifa ambayo inaongozwa na zile Kamati Kuu mbili ya Mawaziri na makatibu wakuu, lakini tuna kamati ya taifa ya uhamasishaji Kitengo cha Uhamasishaji na Uelimishaji na Kamati ya Wabunge,"amesema.

Dodoso

Deogratius Kalimenze ambaye ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi anasema kuwa, "Dodoso lina maswali 23 kwa ufupi nitazungumzia tu aina za majengo, jinsi ya umiliki, sifa za majengo, urefu wa majengo, aina za uniti, idadi za uniti zilizopo kama jengo linakaliwa na wakazi zaidi ya mmoja au ghorofa, hali ya ujenzi, kama majengo yaliyokamilika ni mangapi, yanayoendelea na ujenzi, yalivyo katika hatua za msingi na kadhalika,"amesema.

"Hali ya ukaazi ikoje, sababu ya majengo kutotumika, ubora wa majengo, hali ya ujenzi nani anamiliki jengo, aina ya umiliki aidha ni serikali au mtu binafsi, matumzi makuu ya jengo, nyaraka za kisheria wanazomiliki watu, vifaa vya ujenzi wanavyotumia watu, maeneo gani yamepimwa na maeneo gani hayajapimwa kama nilivyosema tunataka tupime, vifaa vya ujenzi vinavyotumika, huduma zinazopatikana, na gharama za ujenzi na vyanzo vya mapato," amesema.

Bw.Kalimenze anasema, hayo yote yataisaidia Serikali kufanya tathmini ya namna gani sekta ya uendelezaji sekta ya majenzi nchini inavyofanya kazi na baadhi ya viashiria vitatumika kupima hali ya umasikini usiokuwa wa kipato.

"Nitoe mfano wa maswali machache kwenu Wahariri mnapokuwa mnazungumzia jambo fulani ni vizuri mkawa na uelewa mpana mnamaanisha nini? Kwa mfano swali linalouliza jengo hili ni la aina gani? Sisi tunafahamu kuna aina kuu mbili za majengo, majengo ya kawaida na majengo ya ghorofa, lakini tumeongeza aina ya tatu aina nyingine ni hatua ya majengo ambayo yanajengwa hayajafikia utimikifu wake,"amesema.

"Haya tutayachukukulia ni aina nyingine ya kihatua kwamba jengo hili lipo katika hatua ya kwanza kabisa, labda kama ni msingi kwa hiyo ni vizuri sana tunapotoa taarifa na takwimu zinazotakiwa kuchukuliwa wananchi wafahamu, watoe taarifa gani katika hali fulani,"amesema.

"Lipo swali linauliza kwamba jengo hili lina sifa gani, tunapozungumzia sifa za majengo kuna aina kuu tatu nyumba iliyo peke yake iliyojengwa kuanzia msingi hadi paa bila kuungana na nyumba nyingine. Lakini tunazo nyumba mbili za aina moja ambazo zimeungana, ni nyumba mbili zilizokamilika, lakini zimeungana zinashare ukuta. Na tuna Nyumba tunasema safu za nyumba, nyumba zaidi ya tatu zimeungana, lakini zote zinaishi watu tofauti tofauti," amesema.

"Swali lingine muhimu ambalo ni vizuri mkalifahamu ni hali ya ujenzi wa jengo lililokamilika hapa tunataka kupata taarifa ya jengo lililokamilka, limeezekwa kuta zote na lina madirisha na milango na limesakafiwa haijalishi limepakwa rangi au halijapakwa rangi, lakini hatua zote hizo zimekamilika tunasema jengo limekamilika.

"Yapo majengo ambayo yamejengwa upande na watu wanaishi na upande mwingine ujenzi unaendelea. Kuna majengo ya muda, haya ni majemgo ambayo hayawezi kudumu kutokana na hali aidha uchakafu au kutokana na madhumuni yake, au vifaa vikivyotumika si vya kudumu, majengo haya tunayaona katika maeneo mbalimbali ambako ujenzi unaendelea na vijijini watu wengi tunayaita (full suit) hizi ni nyumba, lakini ni nyumba za muda . Ukienda kule kwa Wahandizabe utakuta nyumba zao katika hali hiyo.

"Swali lingine muhimu nini hali ya uhitaji wa ukarabati wa jengo, ambalo lipo katika hali nzuri hilo halihitaji ukarabati mdogo, unahitajika ni jengo linalohitaji ukarabati mdogo mfano rangi imeharibika, baadhi ya bati zina kutu, madirisha au milango inahitaji ukarabati mdogo au nyufa kidogo tunasema.

"Lakini ukarabati mkubwa unahitajika ni majengo ambayo yanahitaji utengenezaji mkubwa sana mfano paa zima limeezuliwa, au nyufa kubwa ambayo inahatarisha usalama wa wakazi, milango imeondoka kabisa halifai kabisa kwa matumizi ni jengo ambalo haliko katika hali nzuri kabisa,"amesema.

Changamoto

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi anasema kuwa,changamoto waliyokutana nayo katika zoezi la sensa ya majaribio ni kukosa kwa taarifa hasa kwa majengo ambayo hayajakamilika kutokana na maeneo hayo kukosekana wakazi wanaoishi.

"Hivyo ndugu zangu wahariri na wanahabari tunawaomba mshiriki kikamilifu katika uhamasishaji wa wananchi ili wananchi hao wanaomiliki majengo ambayo hayajakamilika labda ni msingi, boma waache taarifa zao kwa wenyeviti wa mitaa wa maeneo husika ili karani atakapokwenda katika zoezi la kuhesabu majengo basi tayari viongozi wa mitaa wawe na taarifa za jengo husika.

"Pia mwezi huu tutakuwa na mafunzo kwa ajili ya wakufunzi kwa siku 21, sasa wakufunzi hawa watatawanywa kwenda kufundisha kuanzia mwezi wa saba, kufundisha makarani wote zaidi ya 200,000 ambao watatumika katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi,"amesema Deogratius Kalimenze ambaye ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi.

NEC

Naye Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dkt.Wilson Mahera Charles amewataka watanzania kuwa tayari kushiriki kikamilifu zoezi la Sensa ya Watu na Makazi .

Amesema kuwa, zoezi la Sensa ya watu na makazi ni muhimu kwa maendeleo ya nchi, kwani hata Tume ya Taifa ya Uchaguzi hutegemea takwimu za sensa kukadiria idadi ya wapiga kura wapya watakaoandikishwa pamoja na waliopoteza sifa za kuandikishwa.

“Kimsingi wapiga kura au shughuli za uchaguzi kwa ujumla zina uhusiano mkubwa na takwimu zitokanazo na sensa, kwani katika sensa ndipo Tume inaweza kubainisha idadi ya watu itakayowaandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura,”amesema Dkt.Mahera na kuongeza:

“Nawahimiza watanzania wote kujitokeza kuhesabiwa kwenye sensa ya watu na makazi mwaka huu na kila mmoja kumhamasisha mwenzake kuhesabiwa.”

Amesisitiza kuwa ili Tume huyo ifanye shughuli zake vizuri ni lazima ipate takwimu sahihi za watu, makazi na kutambua makundi maalum ambayo ni ya wanawake, wazee, vijana na watu wenye ulemavu.

Mkurugenzi wa Uchaguzi ameongeza kuwa,"kutokana na sensa ya mwaka huu kufanyika kwa kutumia teknolojia ya kisasa ambayo itawezesha kutambua idadi ya majengo ya umma na makazi ya watu, tume tutatumia takwimu hizo, kuweka vituo vya uboreshaji wa daftari la kudumu la mpiga kura,"amefafanua na kuongeza;

"Sensa ya mwaka huu itafanyika kidijiti na itaweza kubainisha idadi ya majengo ya umma ambayo sisi huyatumia kuweka vituo vya kujiandikisha, lakini pia itatusaidia pia kuweka vituo hivyo kwa mujibu wa anuani za makazi ambazo pia sensa inakwenda kuzitambua rasmi,”amesema Dkt.Mahera.

Dkt.Mahera pia amesema, tume imekua ikipanga mipango yake kwa takwimu kuanzia ngazi ya kata, lakini sasa kwa kuwa sensa inakwenda kuweka kumbukumbu hadi ngazi ya kitongoji, itaweza kupanga mipango yake kwa urahisi zaidi na matumizi ya teknolojia katika uchaguzi yataongezeka.

Sensa ya watu na makazi hufanyika kila baada ya miaka 10 na mara ya mwisho Sensa hiyo ilifanyika mwaka 2012 ambapo watanzania milioni 44,929 walihesabiwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news