'Tuache tabia ya kukwapuakwapua mizigo ya watu na wizi,msitumie bodaboda vibaya ninyi ni watu muhimu sana'

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka waendesha bodaboda na bajaji nchini kuacha kutumika katika Vitendo vya wizi pamoja na kukwapua mizigo ya watu ili kulinda heshima yao.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Julai 24, 2022 wakati alipompigia simu Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka kuzungumza na madereva wa bodaboda na bajaji.

Madereva hao walikutana katika kongamano la kuimarisha ushiriki wa waendesha Bodaboda na Bajaji katika sensa ya watu na makazi itakayofanyika Agosti 23 mwaka huu liliandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu.

Rais Samia amesema kuwa baadhi ya madereva boda boda wamekuwa wakikwapua mizigo ya watu pamoja na vipochi hasa vya wanawake.

“Tuache tabia ya kukwapuakwapua mizigo ya watu na wizi,msitumie bodaboda vibaya ninyi ni watu muhimu sana na ninawaombea sana hilo muwe walinzi wa amani wa taifa kwani ninyi ni maafisa wa usafirishaji wa taifa msikwapue mizigo ya watu,”amesema.

Amewataka waendesha bodaboda na bajaji nchini kutambua kuwa wao ni wasafirishaji wa kitaifa hivyo watumie nafasi hiyo kufanya mambo mema kwa jamii ikiwemo kuhamasisha zoezi la sensa ya watu na makazi na kuacha ukwapuaji wa mizigo ya watu.

“Mama yenu nipo pamoja na mtakayozungumza, RC ataniletea changamoto zenu ili tuweze kushughulikia,”amesema Rais Samia.

Hata hivyo, Rais Samia ametoa wito kwa waendesha bodboda na bajaji kushiriki kikamilivu katika suala nzima la sensa ya watu na makazi Agosti 23,2022.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news