Uhuru wa habari ni haki ya msingi sana-Balile

NA DIRAMAKINI

MWENYEKITI wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Deodatus Balile amesema, kusudio la maboresho ya sheria za habari nchini, yanalenga kuwaondoa wanahabari na vyombo vyao katika sintofahamu.

Amesema, moja ya kitanzi katika tasnia ya habari, ni kosa la mwandishi kuelekezwa kuwa kosa la kituo ama taasisi ya habari.

Amesema, kosa la mwanahabari limekuwa likichukuliwa kama kosa la taasisi ya habari na kusababisha madhara makubwa ya kufungwa kituo ama gazeti tofauti na ilivyo kwenye tasnia nyingine nchini.
Akizungumza kwenye kipindi cha 360 kinachorushwa na Clouds Televisheni leo, jijini Dar es Salaam, mwenyekiti huyo amesema, suala hilo ni miongoni mwa mabadiliko ya sheria za habari yanayopigiwa chapuo.

“Kosa la mwandishi mmoja, unafungia kituo ama gazeti? Kuna watu wengi wanaumia hapo. Yupo dereva ambaye wala hahusiki na habari iliyochapishwa,lakini hata mwananchi ambaye hupata habari kwenye chombo anachokipenda, anakuwa ameumizwa,”amesema Balile.

Ametoa mfano wa daktari aliyemfumua nyuzi mgonjwa baada ya kushindwa kulipa shilingi 10,000 gharama za matibabu, “huyu daktari, waziri hakumfukuza kazi, alimpeleka kwenye bodi ya madaktari na wao wakachukua hatua stahili.”

Amesema, iwapo Bodi ya Ithibati ya Habari itakuwa huru na kujumuisha wadau mbalimbali wa tasnia hiyo, itakuwa na ufanisi mkubwa na kujengea heshima tasnia hiyo.

Pia amesema, mchakato wa mabadiliko ya sheria kandamizi za habari nchini, haulengi upendeleo kwa wanahabari bali haki, wajibu na mazingira mazuri ya tansia hiyo.

“Mchakato wa mabadiliko haya, unalenga kuweka mipaka, lakini pia uhuru wa habari bila kuumiza mtu yeyote. Tunalenga kupata uhuru zaidi wa habari na wajibu kwa mwanahabari.

“Tunapozungumzia uhuru wa vyombo vya habari, sio kwamba tunataka upendeleo kutoka serikalini, la! Tunacholenga hapo kila mmoja apate haki na awajibike,”amesema Balile.

Kwenye kipindi hicho, Balile amesema ingawa wadau wa habari wanasimamia mabadiliko hayo, uhuru wa habari unawahusu hata wale wasio wanahabari.“Tufahamu kuwa uhuru wa habari ni haki ya msingi ambayo wengine wanaitaka. Vyombo vya habari visipokuwa huru, wananchi nao pia wanakosa uhuru ikiwa ni pamoja na kutoa maoni yao pia kupata taarifa zinazowahusu moja kwa moja,” amesema.

Pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kupitia sheria za habari na kuagiza zifanyiwe maboresho ili kuendana na mazingira yaliyopo.

“Tulikutana na Rais (Rais Samia) Ikulu na kwa kuanza, tulimuomba kuhamisha tasnia ya habari na kuipeleka kwenye Wizara ya Mawasiliano, tunashukuru amefanya hivyo,” amesema Balile.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news