Wahukumiwa kunyogwa kwa hatia ya mauaji Njombe

NA DIRAMAKINI

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Iringa iliyokaa kikao chake katika Mahakama ya Hakimu mkazi Mkoa wa Njombe imewahukumu washtakiwa watatu, Elias Jackson Mwenda (31), Hussein Khamis (31) na Orestus Mbawala (51) kunyongwa hadi kufa baada ya kukutwa na hatia ya mauaji ya James Kaengesa mkazi wa Makambako mkoani Njombe.

Akisoma hukumu hiyo Julai 6, 2022 Jaji Dkt.John Utamwa amesema, tukio hilo la mauaji lilitokea Mtaa wa Mashujaa uliopo Halmashauri ya Mji wa Makambako.

Amesema, tukio hilo lilitokea Juni 2016 saa mbili usiku ambapo marehemu ambaye alikuwa dereva wa bodaboda aliyokuwa akiimiliki, alikodiwa na moja ya washtakiwa hao na alipofika eneo la Mashujaa aliambiwa asimame na mshtakiwa huyo ambaye alikuwa amepakiwa kwenye bodaboda hiyo.

Amesema, eneo ambalo marehemu alisimamisha pikipiki yake hiyo kumbe washtakiwa walikubaliana endapo mwenzao atakodi bodaboda mpya asimame eneo hilo.

"Ndipo walimkaba marehemu na kumnyonga kwa kutumia kamba na kupora pikipiki," amesema Dkt.Utamwa.

Amesema, baada ya kumyonga marehemu na kumuua washtakiwa hao walimtupa kwenye shamba la mahindi na kutoweka na pikipiki kuelekea mkoani Mbeya ambako walikamatwa eneo la Rujewa wakiwa na pikipiki hiyo.

Amesema, hukumu hiyo kwa washtakiwa hao imetolewa kutokana na wao kwenda kinyume cha sheria chini ya kifungu cha 196 na 197 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2019.

Awali mawakili wa Jamhuri, Matiku Nyangero na Andrew Mandwa waliiomba mahakama kutoa adhabu kwa mujibu wa kifungu cha 197 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya 2019 kwa kuwa adhabu ya mauaji ya kukusudia ni moja tu ya kunyongwa hadi kufa.

"Pikipiki iliyokuwa kielelezo cha sita upande wa jamhuri iliyokuwa mali ya marehemu arudishiwe mke wa marehemu anayeitwa Enelika Nyenzi," amesema Nyangero.

Kwa upande wa utetezi uliowakilishwa na Musa Mhagama, Byton Kaguo na Octavian Mbungani wamekubaliana na maombi yaliyotolewa na mawakili upande wa Serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news