'Wanahabari mna majawabu ya wananchi kuhusu fursa zilizopo Jumuiya ya SADC'

NA GODFREY NNKO

WAANDISHI wa habari nchini Tanzania wametakiwa kutambua kuwa, wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanashiriki hatua kwa hatua kuibua fursa mbalimbali zilizopo katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na kusiwasilisha kwa wananchi kupitia vyombo vya habari ili waweze kuzitumia kwa maslahi mapana ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Rai hiyo imetolewa leo Julai 26, 2022 na Mwezeshaji wa Mafunzo kikanda kutoka nchini Zambia, Bw.Chibamba Kanyama wakati akizungumza na DIRAMAKINI muda mfupi baada ya kuhitimisha mafunzo ya siku mbili kwa wanahabari juu ya mtangamano wa kikanda wa nchi wanachama za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC,) na fursa zinazopatikana.

Mafunzo ambayo yameratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) ambapo yamefanyika mjini Bagamoyo mkoani Pwani.

"Mwanahabari ni zaidi ya muonaji, ukiwa muonaji unakiona kitu cha mbele zaidi ya wenzako, hivyo kwa upekee na nafasi kubwa waliyo nayo wanahabari wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa, wanachimbua na kuibua fursa zilizopo ndani ya SADC, kushiriki hatua kwa hatua kuzichakata kwa njia rahisi na kusiwasilisha kwa wananchi ili waweze kufahamu wapi waanzie waweze kunufaika na mtangamano huu.
"Kwa maana nyingine, ninyi wanahabari mmebeba majawabu ya wananchi kuhusu nini kinachofanyika ndani ya SADC, ni fursa zipi ambazo wanaweza kuzitumia waweze kuyaendea maono yao.Ndani ya nchi wanachama wa SADC kuna fursa nyingi, tena zingine hazijatumika kabisa, hivyo ni wakati wenu wa kuzichambua haraka na kuwaeleza wananchi,"amesema Bw. Kanyama katika mahojiano na DIRAMAKINI.

SADC ambayo ina miaka zaidi ya 40 ni Jumuiya ya Kiuchumi ya Kikanda inayojumuisha nchi wanachama 16 ikiwemo Angola, Botswana, Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Eswatini, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Seychelles, Afrika Kusini, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Zambia na Zimbabwe.

Dhamira ya SADC ni kukuza ukuaji wa uchumi endelevu na wenye usawa na maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia mifumo bora, yenye tija, ushirikiano wa kina na utangamano, utawala bora na amani na usalama wa kudumu; ili eneo hilo liwe na ushindani madhubuti katika mahusiano ya kimataifa na uchumi wa Dunia.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni miongoni mwa waasisi wa jumuiya hiyo, Bw.Kanyama anasema,ina fursa nyingi ambazo zinategemewa na nchi wanachama ili kufikia maendeleo ikiwemo bandari ambayo imekuwa lango kuu kwa baadhi ya mataifa, miundombinu unganishi ambayo inawezesha kusafirisha bidhaa na kutoa huduma kwa haraka.

Amesema, wakati mwingine inaweza kuwawia vigumu wananchi kufahamu kinachoendelea ndani ya jumuiya hiyo na wengine wakajihisi pengine inawalenga viongozi wakuu wa nchi kutokana na wanahabari kushindwa kuzitumia kalamu zao vizuri kutoa elimu.

"SADC ni ya wananchi na SADC ni zaidi ya kiwanda, nikisema ni zaidi ya kiwanda ninamaanisha kuna fursa zimejaa humo ambazo zinagusa maisha ya kila mwanachi kuanzia kiafya, kielimu, utamaduni, kijamii, kiuchumi, ulinzi na nyinginezo nyingi.

"Kwa hiyo, wanahabari mnapaswa kwenda kuzichimbua hizo fursa kama ni za uwekezaji,chambueni na mziwasilishe kwa wananchi, kuna Watanzania wanasubiria tu kufahamu wapi penye fursa pengine ya uwekezaji au masoko wakatoe huduma huko, na huko SADC zipo, hivyo mkifanikiwa kuwapa elimu, mnakuwa mmefungua macho wengi na wakizifanyia kazi, manufaa yanakuwa kwa kundi kubwa la jamii na Taifa kwa maana ya fursa za ajira,mapato na nyinginezo,"amesema Bw.Kanyana.

Wafanye nini

Wakati huo huo, Bw.Kanyama amesema kuwa, wanahabari wabunifu wana nafasi kubwa ya kuwa miongoni mwa washindi wa tuzo maalum inayotolewa kila mwaka na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

"Moja wapo ya siri ya kuzitwaa tuzo za SADC, ni kuhakikisha unatuliza akili, unaangalia miongoni mwa miradi au huduma zinazotolewa na SADC, ukishatambua huu ni mradi muhimu mfano sekta za afya, elimu, miundombinu, kiuchumi na nyinginezo, jiulize una matokeo gani katika ngazi zote kuanzia wananchi wa ngazi za chini hadi ngazi ya Serikali.Ukiona jibu linasisimua, anzia hapo na utafanikisha,"amesema Bw.Kanyama.

Awali Balozi Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga alieleza kuwa, GIZ kwa kushirikiana na wizara wameandaa na kutoa mafunzo hayo kwa kundi la wanahabari kwa manufaa ya Umma wa watanzania ambao watashirikishwa fursa zenye manufaa ya kiuchumi za SADC.
 
Balozi Kayola

Kwa upande wake,Mratibu Mkuu wa Kitaifa wa Masuala ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kikanda Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Agnes Kayola wakati akifunga mafunzo hayo amesisitiza kuwa, Serikali inathamini na itaendelea kushirikiana na vyombo vya habari kwa kutambua kuwa, mchango wake katika kuhabarisha umma na kuelimisha kuhusu masuala mbalimbali.

"Hivyo, wakati wote tunavyoandika tuendelee kuandika habari ambazo ni chanya, maana mkifanya hivyo mtawezesha wananchi kupata taarifa sahihi ambazo watazitumia kwa ajili ya kufanya maamuzi sahihi ya kushiriki katika fursa na miradi mbalimbali ya maendeleo ndani na nje ya SADC.

"Hivyo, tuendelee kutumia kalamu zetu kwa usahihi ili ziweze kuleta matokeo mazuri katika jamii yetu na Taifa kwa ujumla.

Julai 25,2022 wakati akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine, Balozi Kayola alisema kuwa,lengo la mkutano huo ni kuwajengea uelewa wanahabari kuhusu Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ili waweze kushiriki kikamilifu kutoa taarifa chanya ambazo zitakuwa na hamasa kwa Watanzania waweze kuzitambua fursa zilizopo katika jumuiya hiyo.
"Tanzania ni miongoni mwa nchi waanzishi wa SADC ambayo ina umri wa miaka 40. Waandishi wa habari mna mchango mkubwa kuhakikisha kundi la vijana linafahamu ipasavyo umuhimu wa SADC ili waweze kushiriki na kuzitumia fursa zilizopo katika jumuiya hii ya kikanda kwa manufaa,"amesema Balozi Kayola. 
 
Amesema, licha ya fursa nyingi zilizopo katika nchi wanachama wa jumuiya hiyo, pia Tanzania inazo huduma nyingi ambazo zikitumika ipasavyo zitaweza kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa jamii na Taifa kwa ujumla.

"Pia kutokana na fursa zinazopatikana tutaendelea kutumia lugha yetu ya Kiswahili kama bidhaa, hivyo jukumu kubwa ambalo mnapaswa kulifahamu ni kuhakikisha mnakitumia Kiswahili ipasavyo katika kutoa taarifa zenu,"amesema.

Amefafanua kuwa, malengo ya SADC kama ilivyoelezwa katika Kifungu cha 5 cha Mkataba wa SADC (1992) ni kufikia maendeleo ya kiuchumi, amani na usalama, na ukuaji, kupunguza umaskini, kuimarisha kiwango na ubora wa maisha ya watu wa Kusini mwa Afrika.

Sambamba na kusaidia watu wasiojiweza kijamii kupitia Ushirikiano wa Kikanda. "Malengo haya yanapaswa kufikiwa kwa kuongezeka kwa Mtangamano wa Kikanda, unaojengwa kwa misingi ya kidemokrasia, na maendeleo yenye usawa na endelevu,"amesema.

Mikakati

Balozi Kayola amesema kuwa, kupitia SADC wana mikakati mbalimbali ikiwemo kuwaenzi viongozi waanzilishi akiwemo Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

"Kwa kuzingatia hilo sanamu ya Mwalimu Nyerere itajengwa kwenye jengo la amani na usalama huko Addis Sababa nchini Ethiopia, mkakati huo unaendelea,"amesema.

Pia amesema, jukumu lingine walilonalo ni kuhamasisha jamii ya Watanzania waaweze kufahamu kuhusu majukumu, malengo na fursa zinazopatikana kwenye jumuiya ya SADC.
"Lengo lingine ni kuhamasisha umoja na ushirikiano katika nchi wanachama, kwa kulizingatia hilo Mheshimiwa Dkt.Jakaya Kikwete,Rais mstaafu waa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Jopo la Wazee wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), linaloshughulikia migogoro katika nchi wanachama wa jumuiya,"amesema Balozi Kayola.

Amesema, lengo lingine ni kutoa elimu kuhusu mtangamano wa jumuiya hiyo na ushiriki wa sekta ya habari katika kuhakikisha wanashiriki kikamilifu kufikisha taarifa chanya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news