Dkt.Magembe aguswa na utekelezaji miradi ya Afya wilaya za Lindi,Mtama

NA OR - TAMISEMI

NAIBU Katibu Mkuu (Afya) Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Dkt.Grace Magembe amepongeza kasi ya utekelezaji wa miradi katika Halmashauri ya Wilaya ya Lindi na Mtama na kuwasisitiza kuendeleza kasi hiyo kwa miradi mingine inayoendelea kutekelezwa katika halmashauri hizo.
Dkt.Magembe ameipongeza Manispaa ya Lindi kwa kuimarisha usimamizi wa fedha na kuwa wabunifu katika utekelezaji ambapo kwa kutumia shilingi milioni 250 walizopewa na Serikali kujenga jengo la wagonjwa wa nje, maabara na kichomeo taka katika kituo cha Afya Ng’apa kwa kutumia fedha hiyo hiyo wameongeza mnara wa tenki la maji na shimo la kutupia kondo la nyuma.

Hayo yamebainishwa Julai 25, 2022 baada ya ziara yake ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za Afya katika Halmashauri hizo mkoani Lindi.

“Nimeona namna ambavyo kamati ya usimamizi wa ujenzi, ofisi ya Mhe.Mkuu wa Wilaya, Ofisi ya Mkurugenzi na wananchi mnavyoshirikiana kutekeleza na kusimamia miradi, hongereni sana na endeleeni na utekelezaji ili miradi iishe kwa wakati na kuanza kutoa huduma,” amesema Dkt.Magembe.
Aidha, amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama kwa kuwa mbunifu katika kusimamia matumizi ya fedha katika utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya Afya ya Hospitali ya Wilaya ya Mtama na kuagiza baadhi ya huduma za afya zianze kutolewa kwakuwa majengo tayari yamekamilika.

Awali akipokea taarifa ya utekelezaji wa huduma za Afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtama.

Dkt.Magembe amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kutekeleza afua za lishe na Ustawi wa Jamii pamoja na kendelea kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii ambapo kwa sasa uandikishaji upo asilimia 15 tu.
Kupitia taarifa hiyo ambayo imeonesha kiwango cha maambukizi ya malaria bado kiko juu katika Halmashauri ya Mtama, Dkt. Magembe amemtaka Mkurugenzi kujikita katika kuua mazalia ya mbu na kuhamasisha wananchi kufanya usafi wa mazingira ili kuondoa mazalia ya mbu yanayosababisha maambukizi ya ugonjwa wa Malaria.

Manispaa ya Lindi imepokea shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Nga’apa, Halmashauri ya Mtama imepokea zaidi ya shilingi Bilioni 3 kwa ajili ya uendelezaji wa hospitali ya halmashauri.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news