Waziri Aweso atoa maelekezo kwa ofisi za mabonde ya maji nchini

NA DOTO MWAIBALE

WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amezindua jengo la ofisi kuu ya Bonde la Kati zilizopo mjini Singida na maabara za ubora wa maji na kuyataka mabonde mengine kwenda kujifunza utendaji mzuri wa kazi unaofanya na viongozi wa bonde hilo.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (kushoto) akikagua ujenzi wa mradi wa maji, Dareda, Singu, Sigino na Bagara unaotekelezwa Mkoa wa Manyara ambao utagharimu shilingi bilioni 12.

Akizungumza Julai 30, 2022 mara baada ya kuzindua jengo hilo ambalo ujenzi wake umegharimu zaidi ya sh.bilioni 2.9 hadi kukamilika kwake, alisema Bonde la Maji Kati litakuwa kama chuo kwa mabonde mengine kwenda kujifunza kutokana na jinsi wanavyofanya kazi kwa ufanisi mkubwa.

Aweso alisema, Wizara ya Maji ina jukumu la kuhakikisha nchi inakuwa na maji ya kutosha hivyo bodi za maji nchini ziache kuweka bei za kuwakandamiza watumiaji wa maji ili wapate nguvu za kuendelea kutunza vyanzo vya maji.
Waziri wa Maji Jumaa Aweso akizindua jengo hilo lililopo Kata ya Utemini mjini Singida.

Aidha, alisema baada ya kukamilika kwa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi kukamilika, mabonde yote tisa ya maji nchini yarejewe takwimu za upatikanaji wa maji nchini.

Aweso alisema Bodi za Maji zihakikishe zinawatambua na kuwashirikisha watumiaji wa maji kwani wapo baadhi wanatumia maji bila kuwa na vibari lakini hawatambuliwi.

"Moja ya changamoto ya mabonde yetu yanatumika tu kwa ajili ya 'ambush' tu, washirikisheni, watambuweni wadau wenu wa maji na msiweke bei za kuwakandamiza, wekeni bei rafiki," alisema.

Aweso alisema wakurugenzi na maafisa wa mabonde ya maji watambue wajibu wao kwa kutoka maofisini kutoa elimu sahihi ya juu uanzishwaji wa mabonde ya maji.
Waziri wa Maji Jumaa Aweso (kushoto) akipata maelezo ya ujenzi wa mradi ya ofisi ndogo ya Bodi ya Maji Bonde la Kati inayojengwa Babati mkoani Manyara ambao ujenzi wake utagharimu zaidi ya Sh.700 Milioni. Katikati ni Afisa Maji Bodi ya Maji Bonde la Kati, Mhandisi Danford Samson.

"Wakati mwingine anapoambiwa mtu kuna taasisi ya bonde anajua pengine ni kimlima kidogo kidogo, maafisa wa bonde mtoke muwaelimishe wananchi," alisema.

Aweso alisema haiwezekani unajiita afisa bonde halafu hata vyanzo vya maji huvijui na hata watu wanapokuwa na changamoto ya maji hauna ufumbuzi wa tatizo hilo.

Alisema zifanyike jitihada za kuongeza rasilimali za maji kwani haiwezekani mvua zinanyesha halafu maji yote yanapotea kwenye bahari.

Waziri Aweso alisema ni muda mwafaka rasilimali za maji kwa maana ya mvua isiwe kama laana bali iwe baraka na fursa kwa maji ya mvua kuvunwa kwa kujenga mabwawa ya kimkakati ili maji hayo yatumike kwa matumizi ya kunywa.

Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji Dk.George Lugomela alisema Bodi ya Maji Bonde la Kati iliyomaliza muda wake imejitahidi kufanya kazi ambapo imeongeza ukusanyaji wa mapato kutoka Sh.Milioni 300 zilizokiwa zikikusanywa awali na kufikia Sh.mil.800.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Pakas Mlagiri, alisema Bonde ndio injini ya maji sababu wao ndio wanaovisimamia vyanzo vyote vya maji.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Manyara (BAWASA) Idd Msuya (katikati) akimuelezea Waziri wa Maji Jumaa Aweso kuhusu mradi huo.
Alisema kutokana na umuhimu huo wa mabonde ya maji, kufanyike utafiti wa kuainisha vyanzo vyote vya maji kuanzia ngazi ya kijijjj na kata kufanya hivyo kutasaidia upatikanaji mkubwa wa maji.

Meya wa Manispaa ya Singida, Yagi Kiaratu, alisema upatikanaji wa maji katika manispaa hiyo umefikia kiwango za asilimia 80.

Kiaratu alishauri Bonde la Maji Kati kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Singida kutunga sheria ndogo kwa ajili ya kulinda vyanzo vya maji.

Mwenyekiti wa Bodi ya Maji Bonde la Kati, William Mabula alisema wamejipanga kufanya vizuri zaidi kwa kusimamia rasilimali za maji na kuongeza mapato kutoka Sh.milioni 800 hadi kufikia shilingi bilioni moja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news