Waziri Nape atoa maelekezo kwa TCRA

NA DIRAMAKINI

WAZIRI wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kujenga jengo la kudumu ndani ya viwanja vya Maonesho ya Biashara ya Kimataifa (DITF) Sabasaba ili wananchi waweze kupata huduma iliyo bora.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufanya ziara ya kutembelea mabanda mbalimbali amesema, ameshaongea na Mamlaka ya Biashara Tanzania (TANTRADE) ili kuhakikisha kuwa, TCRA inakuwa na ofisi ya kudumu ndani ya viwanja hivyo vya Mwalimu Julius Nyerere kwa kuwa, wana majukumu makubwa kwa jamii.

Nnauye amesema uwepo wa banda la kudumu la TCRA ndani ya maonesho hayo litarahisha wananchi kupata huduma kwa wakati,kupunguza gharama ambazo zinatumiwa na mamlaka hiyo kila mwaka wakati wa maonesho.

"TCRA ni wadau muhimu kwa watanzania kama mtakuwa na jengo la kudumu mtaweza kuwasaidia watanzania walio wengi kuweza kupata huduma sahihi,"amesema Nnauye.

Amesema, Tanzania ni sehemu sahihi ya uwekezaji hivyo mawasiliano yakipatikana katika ubora itaifanya Tanzania kuwa bora zaidi.

Aidha, amesema licha ya makampuni ya nje kuwekeza Tanzania, TCRA isisite kutoa huduma kwa watanzania.

"Pamoja na huduma zote mnazotoa mtanzania anatakiwa apewe kipaumbele katika suala zima la utoaji huduma,"amesema.

Amesema, pamoja na hayo yote ni jukumu la vyombo vya habari kutangaza vitu vizuri vilivyopo Tanzania ili kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan.

Vilevile amevitaka vyombo vya habari kutangaza soko la ndani ili watanzania wavutiwe kuwekeza nchini.

Wakati huo huo, alipotembelea banda la Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) amezitaka taasisi za Serikali kutumia teknolojia ya TEHAMA ya video conference katika mikutano yao.

Amesema, TEHAMA hiyo itasaidia kupunguza gharama kwa serikali na itawawezesha kuwasiliana kwa urahisi zaidi kwa watumishi wao."Serikali ipo tayari kuwawezesha kutekeleza mpango huo wa TEHAMA,"amesema.

Naye Mkurungezi wa TTCL, Mhandisi Peter Ulanga amesema, wao ndio wa kwanza kutekeleza agizo la Serikali la kutumia video conference katika mikutano."Tuna wateja zaidi ya 10 mkoani Dodoma ambao tumeshawaunganishia huduma hiyo,"amesema Mhandisi Ulanga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news