Huduma bora iwe kipaumbele kwa mteja-Jaji Mfawidhi Ngwembe

NA EVELINA ODEMBA-Mahakama

JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe amewataka watumishi wote wa Mahakama mkoani hapa kutoa huduma bora ili wajitofautishe na wengine, hivyo kuwafanya wananchi waione Mahakama ndio sehemu sahihi ya kuikimbilia.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe 

Mhe. Ngwembe alitoa wito huo Julai 5, 2022 alipokuwa akifungua mafunzo ya namna ya kuwahudumia wateja yaliyotolewa kwa watumishi wa Mahakama Kanda ya Morogoro ili kuboresha hali ya uwajibikaji na utoaji huduma kwa wateja wanaofika mahakamani hapo. 

“Ili wote tusafiri katika chombo kimoja ni muhimu tukatambua kuwa jukumu la kutoa huduma bora kwa mteja ni la kila mmoja wetu bila kujali cheo na wadhifa alionao, ndio maana mafunzo haya yametolewa kwa watumishi wa ngazi zote,” alisema. 
Picha juu na chini ni sehamu ya watumishi waliohudhuria mafunzo hayo.

Jaji Mfawidhi huyo alisema kuwa mafunzo hayo yatakuwa endelevu kwa watumishi wa Mahakama ngazi zote, hivyo ni bora kila mmoja awe tayari kujifunza,kuelewa na kuyafanyia kazi mafundisho yote yatakayotolewa. 

Mhe. Ngwembe alisisitiza kila mmoja kujifunza matumizi ya vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuendana na Mahakama ya kisasa. Aidha amewashauri wote wenye umri unaowaruhusu kurudi shule ili kujiendeleza kielimu wafanye hivyo kwani Mahakama ya sasa ni Mahakama ya kisasa, sio ile ya karne ya 18 au karne ya 19. 
Hakimu Mkazi Mfawidhi Japhet Manyama.

Mkufunzi wa mafunzo hayo ambaye ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Mhe. Japhet Manyama alibainisha kuwa huduma nzuri kwa mteja ndio itakayowatofautisha watumishi hao na watoa huduma wengine, hivyo kuwavutia wananchi kuiona Mahakama kama sehemu sahihi ya kuikimbilia na sio kuikimbia. 

Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Sylvester Kahinda alisema wameitikia wito na maelekezo ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahimu Hamis Juma na uongozi mzima ngazi ya taifa kuwataka kutoa mafunzo ya aina mbalimbali kwa watumishi wa Mahakama, hivyo kuamua kuanza na mafunzo ya namna ya kuwahudumia wateja. 
“Tumeanza na hili tukiamini kuwa litachangia kwa kiasi kikubwa kutatua kero za wananchi jambo lililosisitizwa hata katika mpango mkakati wa Mahakama,” amesema. 

Akitoa shukrani kwa waandaaji wa mafunzo hayo, Msaidizi wa Kumbukumbu kutoka Mahakama ya Mwanzo Kihonda, Bw. Ally Mkasi alisema hatua hiyo imewaongezea uwezo wa namna ya kuhudumia wateja na wapo tayari kuendana na Mahakama ya kisasa ili kumrahisishia mwananchi kupata huduma sahihi kwa wakati. 

Katika mafunzo hayo, Mahakama Kanda ya Morogoro haikuishia kutoa elimu kwa watumishi pekee bali watoa huduma wanaofanya kazi katika jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki nao walishirikishwa ambapo kulikuwa na mwakilishi toka kampuni ya usafi na mwakilishi toka kampuni ya ulinzi.
Muonekano wa jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro ulipo ukumbi ambao ulitumika katika mafunzo kwa watumishi.

Sanjari na hilo, wateja pia wana darasa lao maaalumu linalotolewa mara tatu kwa juma, lengo likiwa ni kuweka mikakati kuanzia mteja anapofika getini mpaka anapotoka nje ya jengo baada ya kupatiwa huduma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news