Waziri Simbachawene ashiriki maziko ya Padre Onesmo Wissi

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. George Simbachawene ameshiriki ibada ya mazishi ya Padre Onesmo Wissi iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Jimbo Kuu Dodoma, na baadaye mwili wake kuzikwa katika makaburi ya mapadre yaliyopo Bihawana jijini Dodoma. Padre Onesmo Wissi (62) ambaye wakati wa uhai wake alikuwa Makamu wa Askofu Jimbo Kuu Katoliki Dodoma nchini alifariki dunia katika Hospitali ya DCMC iliyopo Ntyuka mkoani humo alipopelekwa baada ya kujisikia vibaya.

Awali Mkurugenzi wa Mawasiliano Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, Padre Paul Muhindi alisema kuwa, Padre Wissi alipelekwa katika hospitali hiyo Julai 25,2022 saa 1.00 jioni.
“Alianza kujisikia vibaya, akasema mbona hali inazidi kuwa mbaya akatupigia simu, tukaja na kum-rush (kumkimbiza) kule Ntyuka,” amesema Padre Muhindi.

Alisema Padre Wissi ambaye pia alikuwa Paroko wa Parokia ya Kanisa Kuu la Paul wa Msalaba, alifariki saa 3.00 usiku Julai 25, 2022 kwa ugonjwa wa kiharusi.
“Kabla ya hapo alikuwa anaongea na watu vizuri, aliongea na watu hadi jioni,”alisema Padre Muhindi.
Misa ya mazishi ilianza saa 3.30 leo asubuhi Kanisa Kuu la Kiaskofu la Paul wa Msalaba na baadae kwenda kuupumzisha mwili wa marehemu.

Post a Comment

0 Comments