Augustino Lyatonga Mrema, shujaa aliyeondoka akiwa ameacha alama kwa Taifa

NA ADELADIUS MAKWEGA

AUGUSTINO Lyatonga Mrema amefariki dunia na tangu kuondoka kwake Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kwenda NCCR MAGEUZI na baadaye TLP sasa ni miaka zaidi ya 27.

Kwa hakika huo ni umri wa mtu mzima ambaye amepiga kura mara kadhaa kumchagua diwani, mbunge na hata Rais.

Kuwepo kwake upinzani, Mrema alikuwa amefunikwa na giza moja baya sana huku akitazamwa na baadhi ya watu kama ni mamluki, dhaifu, mwongo na mzandiki ambapo mimi binafsi siamini katika hilo kwani mtu anaweza akawa upande unaoaminika na akawa na sifa za mamluki, dhaifu, mwongo na mzandiki

“Augustino Mrema alikuwa mwanasiasa makini sana ambaye amewahi kulitumikia taifa hili kwa moyo wote, hasa hasa kwa wale tuliowahi kumuona na kushuhudia tunaweza kuwa mashahidi kwa wenzetu ambao hawakujaliwa hilo”

Mwaka 1992 nikiwa mwanafunzi wa kidato cha pili wa Tambaza sekondari, mheshimiwa Mrema alifika shuleni hapa na kuzungumza na wanafunzi wa shule hii nia ilikuwa kutatua mgogoro usafiri wa wanafunzi wa Dar es Salaam.

Mrema akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na baadaye akawa Naibu Waziri Mkuu alifika hapo kwa hoja moja tu ya kutatua mgogoro uliokuwepo baina ya makondakta wa Chai Maharage (Daladala za wakati huo) na wanafunzi juu ya idadi ya wanafunzi katika kila Chai Maharage.

Mgogoro huu ulileta taharuki huku wanafunzi wa Tambaza wakifanya vurugu zilisababisha hata kuondoa utulivu na kuharibu baadhi ya vyombo vya usafiri jijini Dar es Salaam

Tukiwa katika ukumbi wa Tambaza ambao ni ukumbi wa miaka mingi, wenye kujaza wanafunzi juu na chini, mkuu wa shule hii wakati huo aliyefahamika kama mwalimu Julius Mushi alisimama na kuukaribisha ugeni huo, kwa kumpa nafasi Afisa Elimu wa jiji Mwalimu Abdul Mbegu, Utambulisho uliendelea huku ukumbi ukiwa kimya, kwani ugeni huu mkubwa ulikuwa ni jambo muhimu sana kwa serikali, wanafunzi Tambaza na wanafunzi wote jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya wanafunzi watukutu wa Tambaza wakikacha kikao hicho wakidhani kuwa lingekuja Karandinga (lori la Polisi) kuwabeba na kuondoka nao.

Siku hiyo shule nzima ikiwa imezungukwa na polisi wenye silaha, baadhi ya wanafunzi wa Tambaza ukimbini safari za kwenda na kurudi maliwatoni zikiwa nyingikuonesha kuwa walikuwa na uwoga na ugeni huo.

Mara akakaribishwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam marehemu Ditopile Mzuzuri, alikuwa amevalia suti yake ya rangi ya kaki ikiwa na mifuko mifuko mingi kifuani kwake akasema,

“Mamboo! Hamjamboo! Mimi ndiye Ditopile Ukiwaona Ramandhani wa Mzuzuri ambaye nimewahi kusoma Tambaza…” Ukumbi ulilipuka kwa makofi, miluzi na mayowe… Buffalo Soldier…if you know your history, eh you know where you coming from…( Disc Joker akicheza wimbo huo). Hapo ukumbi wote ulianza kuucheza wimbo huko Ditopile naye akiungana na wanafunzi hao kwa dakika chache kuucheza muziki huo wa reggae.

DJ akazima wimbo huo … huku wanafunzi wa Tambaza wakiguna mheshimiwa Mzuzuri akasema tutacheza baadaye, mkutano ukaendelea, Mzuzuri alitambulisha viongozi wengine wa mkoa huo akiwamo RPC wa Dar es Salaam wakati huo Afande Typhone Maji.

Ditopile alisisitiza umuhimu wa wanafunzi kusoma kwa dakika chache alafu akamkaribisha Waziri wa Mambo ya Ndani mheshimiwa Mrema. Ndugu huyu akaanza kuzungumza kwa lafudhi ya kichaga.

Aliyazungumza mengi likiwamo suala la kutumia muda wa shule kusoma, huku akisema kuwa serikali italifanyia kazi tatizo la usafiri wa wanafunzi katika Jiji la Dar es Salaam.

“Mimi sitaki kuona wanafunzi mnagombana na makondakta wa Chai Maharage, nataka msome kwa bidi, huu mgogoro baina yetu na makondakta utamalizika, isitoshe madereva na makondakta ni ndugu zenu, nani anayependa kugombana na ndugu yake?.”

Alipomaliza kuzungumza alitoa nafasi ya kuulizwa maswali na mwanafunzi wa kwanza ambaye jina silikumbuki alimuuliza juu ya idadi ya wanafunzi wanaotakiwa kupanda katika Chai Maharage moja.

Kwa msomaji wangu ambaye hawakuziona Chai Maharage zilikuwa ni kama lori ndogo kama Canter /Fuso ambazo zina bodi, ndani ya bodi zina mabenchi mawili yanayotazama kama watu wanakunywa chai na maharage gengeni na ndiyo maana waswahili wa Dar es Salaam wakaziita Chai Maharage.

Faida yake kubwa abiria wengi walikuwa wanasimama, kwa hiyo ziliweza kubeba abiria wengi kuliko daladala na mabasi mengine.

Katika kulijibu swali hilo mheshimiwa Mrema alimnyanyua RPC Maji, kwanza alimuuliza idadi ya abiria wanaojaza chombo hicho? Alafu alipojibiwa akasema haya,

“Mambo haya yanatakiwa hekima tu, kwani kama kuna abiria wengi angalau wanafunzi 10 lakini hakuna abiria kwanini muwaache wanafunzi.”

Wanafunzi wa Tambaza waliendelea kuuliza maswali na sasa ilikuwa juu ya wanafunzi kuketi katika viti ndani ya Chai Maharage,“Siyo hekima mtu mzima kusimama nawe mwanafunzi umekaa katika kiti.” Mheshimiwa Mrema alijibu.

Ndugu Mrema aliuzwa swali lingine juu ya mabasi ya mashirika ya umma kuwachukua wanafunzi waliokuwa wakiingia mchana maana kulikuwa na makundi mawili wiki asubuhi kundi A na wikihiyo hiyo mchana kundi B kutokana na uhaba wa madarasa Jijini Dar es Salaam.

Swali hilo liliulizwa kwa kuwa zoezi lilikuwepo lakini lilikuwa linasuasua, kweli zoezi hilo nalo lilifanyika ambapo mabasi hayo yalitakiwa kutoa huduma hiyo kwa wanafunzi na kusimama Fire karibu na Azania, Jangwani sekondari pia Elimu Kwa Njia Ya Posta

Maswali yaliendelea kumiminika mheshimiwa huyu aliulizwa swali lingine juu ya basi ndogo zilizokuwa zinabeba abiria kutoka Msimbazi hadi Muhimbili (town hiace) kwamba wanafunzi wa Tambaza wanapata tabu wanakataliwa kupanda. Mheshimiwa Mrema alimnyanyua RPC Maji tena akamuuliza namna hizo Town Hiace zilivyo. Alipomaliza kujibiwa na RPC Maji aliagizwa haya,

“Kila Town Hiace iwe na kiti nyuma ya kiti cha dereva na kiwe kiti cha wanafunzi watano na viti vingine waketi abiria tu na RPC Maji fuatilia hilo.” Mwanakwetu yote yalitekelezwa na ndiyo maana siku hizi hiace zote zina kiti hicho nyuma ya mgongo wa dereva. Hiace zilianza kubeba abiria ambapo wakati huo nchini nzima Hiace zilikuwa ni Msimbazi-Muhimbili tu.

Katika kikao hicho mheshimiwa Mrema alishangiliwa na wanafunzi wa Tambaza, huku alitoa siku saba kwa Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Dar es Salaam Afande Maji kuhakikisha yote aliyoagiza yanakamilika na kweli baada ya siku hizo wanafunzi tulisafiri kwa utaratibu huo.

Mheshimiwa Mrema amefariki na ameyamaliza maisha yake ya dunia je? Mimi na wewe tutakumbukwa kwa lipi? Viongozi wajitahidi sana kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto za Watanzania na siyo vinginevyo hilo liwe darasa kubwa kwa maisha ya Augustino Lyatonga Mrema.

Raha ya milele umpe ee Bwana, Mwanga wa milele umuangazia, apumzike kwa amani, amina.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news