MREMA ALIKUWA NI MWANASIASA ASIYEISHIWA VITUKO

NA HAPPINESS KATABAZI

LEO asubuhi Agosti 2, 20221 nimepokea taarifa za kifo cha Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour ( TLP), Augustine Lyatonga Mrema kuwa amefariki katika Hospital ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa tangu Agosti 16, mwaka huu kwa ajili ya matitabu.

Taarifa hiyo ilisababisha nilie, kisha nianze kucheka. Nililia kwa sababu Mrema alikuwa ni rafiki yangu,chanzo changu cha habari na kwamba ndio sitaweza kuongea tena kwa simu na Mrema masuala mbalimbali ya siasa za nchi hii.

Taarifa hiyo ya kifo ilisababisha pia niangue kicheko kwa sababu nilijikuta nakumbuka baadhi ya vituko alivyokuwa akififanya katika ulingo wa siasa na vituko vingine alikuwa akivifanya kwa siri alikuwa akinieleza nikiendaga nyumbani kwake enzi zile akiishi Masaki na Sinza ambapo nilikuwa nikifika mara kwa mara kupiga nae stori za siasa na tunacheka sana.

Kutokana na kuwa karibu na Mrema na kuripoti habari zake nilipokuwa mwandishi wa habari gazeti la Mwananchi, Mtanzania, Tanzania Daima, waandishi wa habari wenzangu walinipachika jina la utani la Mrs Mrema na mkewe Mrema ambaye kwasasa ni marehemu alifariki mwaka jana katika Hospitali ya Muhimbili,Rose Mrema naye ilimlazimu kuniita mimi mke mwenza kila ninapofika nyumbani kwake au tunapozungumza na simu.

Enzi zake Mrema alikuwa ni MWANASIASA wa vyama vya upinzani aliyepitia machungu mengi ya mkono wa dola, kwa mfano kukamatwa mara kwa mara na Jeshi la Polisi,kushtakiwa mahakamani kwa kesi mbalimbali ikiwemo kesi ya shilingi milioni 500, kesi ya uchochezi aliyoshtakiwa Mrema na Tundu Lissu katika Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu ambapo upande wa Jamhuri ulidai washtakiwa hao walitoa taarifa za uchochezi kuhusu mgodi wa Blyankulu na baadaye DPP aliamua kuwafutia kesi hiyo.

Mrema mwaka 2005 aligombea urais kupitia NCCR Mageuzi, lakini hakushinda baadae akaenda kujiunga na chama na TLP,nako TLP aligombea urais hakushinda. Baadae akaamua kwenda kugombea ubunge Jimbo la Vunjo akashinda.

Mrema alikuwa na karama moja ambayo niliigundua anayo ambapo ukifika ukamueleza jambo fulani akaliona linamfaa katika mtaji wake wa kisiasa anakusikiliza vizuri sana anayachukua akipanda jukwaani anayabadilisha yale maelezo uliyompa.

Mwaka juzi nilimtembelea nyumbani kwake akaniambia bila Mungu na Rais John Magufuli kumpeleka nje ya nchi kutibiwa angekuwa ameshakufa akawa anamshukuru sana Magufuli.

Ni Magufuli ambaye kwasasa ni marehemu ndiye aliyempa Mrema wadhifa wa Mwenyekiti wa PAROLE.mNitamkumbuka Mrema kwa vituko vyake alivyokuwa akiniadithia ambavyo siwezi kuviandika katika makala hii.

Nitamkumbuka Mrema enzi zile naongozana nae katika misafara yake ya kampeni na lile lori lake limefungwa mziki mkubwa linapita mitaani na vijijini likitumbuiza wimbo aliotungiwa na mwanamuziki Remmy Ongala ambaye naye ni marehemu usemao ' Mremaaa ahh Mrema Jamani Mrema'.

Na pia Mrema gari Hilo lilikuwa likiwekwa nyimbo za mipasho ikiwemo wimbo wa Nasma Hamisi "Achia Ngazi bibi mchuma unaondoka huooo'.

Basi tulikuwa tukifika katika ngome za CCM na Hilo gari linaimba utasikia gari linasimamishwa na kuambiwa na maaskari Zima mzika haraka sana.

Vituko vingine vya Mrema awapo jukwaani mkutano wake kabla ya kuisha alikuwa akiwarushia vijembe polisi kuwa wanatumika vibaya na CCM anawashambulia basi kabla ya mikutano yake kuisha waandishi tulikuwa tunakimbilia kwenye magari ya msafara wa Mrema kujisalimisha roho zetu kwani kilichokuwa kikifuata ni vurugu kuanza mkutanoni hapo na virungu vya polisi kuanza kutembea kutawanya baadhi ya mikutano yake.

Mrema alipwendwa sana na wanawake kwani akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani alitaka wanawake wote wanaoteswa na waume zao wawafichue.

Pia Mrema akiwa Mwenyekiti TLP,polisi wakati wanamkamata na kumuita kumhoji mara kwa mara ndipo baadhi ya wanawake wa TLP wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa TLP, Getrude Pwila waliandamana hadi nje ya geti la Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi Dar es Salaam wakavua blauzi wakabaki na sidiria ikiwa ni kuonyesha hisia zao kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi wa enzi hizo Omary Mahita na askari wake waache kumnyanyasa Mwenyekiti wa chama chao, Mrema.

Huwezi taja historia ya Mageuzi bila kutaja jina la Mrema kwani nae ni miongoni mwa watanzania wachache ambaye walijitoa kimasomaso nakufanya siasa za vyama vya upinzani.

Mema uliyoyafanya hapa duniani rafiki yangu Mrema tutayaenzi. Mungu aiweke roho yako mahali panapostahili.Amina.
 
Happiness Katabazi
 0755 312859

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news