Balile:Waziri Nape katuelewa, lakini hauwezi kusema 'deal done'

NA MWANDISHI WETU

MHESHIMIWA Nape Nnauye ambaye ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ana dhamira njema na tasnia ya habari, lakini imebainika dhamira yake haijalindwa na sheria za tasnia hiyo.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Bw.Deodatus Balile ameyabainisha hayo wakati akizungumza katika Kipindi cha Jambo kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha TBC1 siku ya Agosti 11, 2022 jijini Dar es Salaam.

Amesema, dhamira ya Mheshimiwa Nape ya kutotaka kuona kosa la mwandishi linagharimu chombo cha habari ipo wazi, lakini bado sheria ina dhamira kinyume na dhamira yake.

“Waziri Nape katuelewa, lakini hauwezi kusema 'deal done' (kazi imekwisha). Tunamshukuru sana kwani ameonesha dhamira njema katika kuhakikisha kosa la mwandishi haliathiri chombo cha habari.

“Tumeona ameshughulikia kuvitoa vyombo vya habari vilivyokuwa kifungoni, tunaamini ana dhamira njema, lakini bado sheria ni zile zile ambazo zikitumika, maafa ni yale yale,” amesema Balile.

Pia amesema, mwandishi wa habari anapoteleza katika uandishi wake, hapaswi kupelekwa mahakamani kama ilivyo taaluma zingine nchini bali anapaswa kushtakiwa kwenye bodi ya taaluma yake.

“Kosa la kitaaluma halipelekwi mahakamani, unampelekaje mahakamani mtu kwa kosa la kitaaluma? Ndio maana tunasema kuwepo na chombo ambacho kitasimamia tasnia kama ilivyo kwenye taaluma zingine.

“Mwanasheria akifanya kosa,Serikali haimsimamishi bali chombo ndani ya taaluma yake ndio kinamsimamisha ama kumpa adhabu, hivyo hivyo kwa daktari na hata wahandisi, lakini kwa nini waandishi ndio wahukumiwe moja kwa moja?,” amehoji Balile.

Pia Balile amesema, wadau wa habari nchini wanataka sheria katika tasnia hiyo zitoe mwongozo wa kukuwa kwa uhuru wa habari na sio kudhibiti habari na wanahabari.

“Rais Samia (Suluhu Hassan) tulipokutana naye, alisisitiza anataka sheria zirekebishwe na ziwe bora. Tunaamini tutajadili na tutakubaliana ili tuwe na sheria zinazokubalika kimataifa,”amesema Balile.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news