BALOZI MBAROUK AFUNGUA MKUTANO WA 15 WA JPC YA TANZANIA NA MSUMBIJI

NA MWANDISHI WETU

JAMHURI ya Muungano wa Tanzania imeihakikishia Jamhuri ya Msumbiji kuwa vyombo vyake vya ulinzi na usalama likiwemo Jeshi la Wananchi vitaendelea kufanya kazi mkono kwa mkono na Serikali ya Msumbiji na nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kukabiliana na vitendo vya kigaidi nchini Msumbiji.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk wakati akifungua Mkutano wa 15 wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano ngazi ya Mawaziri kati ya Tanzania na Msumbiji unaoendelea jijini Dar Es Salaam tokea tarehe 22 Agosti 2022.

Amesema Tanzania na Msumbiji ina uhusiano wa kihistoria ambao ni wa kindugu na kwamba Tanzania itaendelea kushirikiana nayo ili kuhakikisha amani inapatikana huko kaskazini mwa nchi hiyo.

"Wakati tukikutana hapa jijini Dar es Salaam nchi zetu na ukanda wa kusini mwa bara la Afrika unakabiliwa na tishio la vitendo vya kigaidi katika jimbo la Gabo del Gado", alisema na kuongeza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Msumbiji ili kuhakikisha amani inapatikana katika eneo hilo.
Amesema kuwepo kwa vitendo vya kigaidi vinavyosababishwa na wanamgambo walioko katika jimbo hilo vinasababisha uharibifu wa mali,vifo na majeruhi kwa watu wasio na hatia na hivyo kuleta tishio la usalama kwa watu wa ukanda wote wa kusini mwa bara la Afrika.

Amesema ni matumaini yake kuwa mkutano huu wa 15 utaimarisha zaidi ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Msumbiji na kusaidia harakati za kujiendeleza kiuchumi kwa faida na manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.
Akizungumza katika mkutano huo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Jamhuri ya Msumbiji Balozi Manuel Gon├žalves amesema kufanyika kwa mkutano huu wa 15 kutaimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Msumbiji.
Amesema, Msumbiji ni ndugu na Tanzania na kusisitiza kuendelea kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja.
Ameishukuru Serikali na wananchi wa Tanzania kwa kuendelea kuwasaidia na kuchangia jeshi la pamoja la SADC katika kukabiliana na vitendo vya kigaidi nchini Msumbiji.

Post a Comment

0 Comments