Bunge latoa ratiba za kamati kukutana, Mkutano wa Nane kuanza Septemba 11

NA GODFREY NNKO

KAMATI za Kudumu za Bunge zitaanza kukutana Agosti 29, 2022 hadi Septemba 11, 2022 jijini Dodoma.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Agosti 22, 2022 na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa, Ofisi ya Bunge.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kamati hizo zinakutana kabla ya Mkutano wa Nane wa Bunge uliopangwa kuanza Septemba 11, 2022.

Aidha, kamati nne zitaanza vikao Agosti 25, 2022 ikiwemo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, shughuli zilizopangwa kufanywa na kamati katika vikao hivyo ni uchambuzi wa sheria ndogo zilizowasilishwa wakati wa Mkutano wa Saba wa Bunge, kazi ambayo itafanywa na Kamati ya Sheria Ndogo. Huku kamati tisa za kisekta zitapokea na kujadili taarifa mbalimbali za utendaji.

Pia kamati mbili zinazosimamia matumizi ya fedha za umma zitachambua taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2021.

Wakati huo huo, kwa mujibu wa taarifa hiyo, kamati tatu zitafuatilia utekelezaji wa maazimio ya Bunge yaliyotokana na taarifa za mwaka za kamati zilizowasilishwa bungeni mwezi Februari, 2022.

Katika hatua nyingine, kwa mujibu wa taarifa hiyo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imepanga kupokea na kuchambua taarifa za uwekezaji wa mitaji ya umma ili kubaini iwapo uwekezaji huo una ufanisi na kuwa umezingatia taratibu na miongozo mujarabu ya biashara.

Aidha, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama itapokea na kujadili taarifa za wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki na za wawakilishi wa Bunge la Tanzania katika vyama vinne vya Kibunge.

Mbali na hayo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imepanga kupokea na kujadili taarifa ya yatokanayo na kikao kilichofanyika kwa mujibu wa Kanuni ya 124 (1) ya Kanuni za Bunge kwa ajili ya majumuisho ya hoja zilizojitokeza wakati wa kujadili utekelezaji wa bajeti za wizara hizo kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Vile vile itapokea taarifa zinazoiwezesha kamati kufuatilia ukusanyaji na vyanzo vya mapato nchini. Pia kamati mbili zitajadili miswada mitatu ya sheria ikiwemo kupokea maoni ya wadau kuhusu miswada hiyo.

Post a Comment

0 Comments