Bwawa la maji la Kwenkambala wilayani Handeni kufanyiwa maboresho

NA MWANDISHI WETU

NAIBU Waziri wa Maji Mheshimiwa Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amekabidhi hundi za thamani ya shilingi milioni 60.6 kwa wananchi waliopisha maeneo kwa ajili ya ujenzi wa bwala la Kwenkambala wilayani Handeni mkoani Tanga.
Hundi hizo amezitoa akiwa katika ziara ya kikazi yenye lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya maji wilayani hapo.

Mheshimiwa Mahundi amesema, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ina nia ya dhati kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma ya majisafi karibu na makazi yake.

Pamoja na hilo, Mheshimiwa Mahundi ametembelea bwawa la maji la Mdoe na kutoa maagizo kwa uongozi wa Mradi wa Kitaifa wa Handeni (Handeni Trunk Main) kuweka miundombinu rafiki itakayowezesha wananchi kupata huduma ya majisafi na salama nje ya eneo la bwawa.

Vilevile, amemtaka Mkurugenzi wa Bodi ya Maji ya Bonde la Pangan kuhakikisha ndani ya wiki moja wanatembelea eneo hilo na kuweka mipaka ya hifadhi ya bwawa.

Amesema sambamba na shughuli hizo serikali inaendelea na utekelezaji wa ujenzi wa miradi mingine ya maji ambayo itasaidia upatikanaji wa huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza katika maeneo yote ya wilaya ya Handeni.

Post a Comment

0 Comments