DC Mkasaba asisitiza ushirikiano kuharakisha maendeleo Kusini Unguja

NA DIRAMAKINI

MKUU wa Wilaya ya Kusini Unguja, Mheshimiwa Rajab Yussuf Mkasaba amesisitiza umuhimu wa kuwepo ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake kwa azma ya kuwatumikia wananchi ipasavyo na hatimaye kufikia lengo lililokusudiwa.
Hayo ameyasema leo Agosti 9, 2022 katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja iliyopo Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja mara baada ya makabidhiano ya ofisi yaliyofanyika ofisini hapo kati yake na Kaimu Mkuu wa Wilaya hiyo, Marina JoelThomas ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kati katika mkoa huo.

Katika maelezo yake, Mkuu huyo mpya wa Wilaya alieleza kuwa ushirikiano ndio msingi mkubwa wa utendaji kazini kwani bila kuwepo ushirikiano wa pamoja hakuna maendeleo yatakayofikiwa.

Alieleza matarajio yake kwamba kuwepo ushirikiano wa pamoja kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha utendaji wa kazi hasa kwa umuhimu wa ofisi hiyo sambamba na kwenda na kasi ya maendeleo iliyokusudiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi.

Aidha, alisema kuwa mbali ya kuwepo kwa ushirikiano suala la kuimarisha amani, umoja, utulivu na mshikamano nalo ni suala la lazima katika wilaya hiyo kwa lengo la kuwatumikia wananchi.

Sambamba na hayo, Mkuu wa Wilaya hiyo ya Kusini Unguja alieleza kwamba ushirikiano wa pamoja utasaidia kwa kiasi kikubwa katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
 
Aliongeza kuwa, Rais Dkt. Mwinyi ana maono makubwa katika kuwapelekea wananchi wake maendeleo, hivyo ushirikiano wa pamoja utasaidia katika kufikia lengo hilo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kati ambaye alikuwa akikaimu Wilaya hiyo, Marina Joel Thomas alimkaribisha Mkuu huyo wa Wilaya hiyo na kuwaomba viomgozi na watendaji wote wa wilaya hiyo kumpa ushirikiano mkubwa ili iwe rahisi katika kutekeleza majukumu yake.
Pamoja na hayo, Mkuu huyo wa Wilaya ya Kati alieleza mafanikio pamoja na changamoto zilizopo katika Wilaya hiyo na kusisitiza kwamba kwa ushirikiano wa pamoja ana matumaini makubwa kwamba ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zilizopo utapatikana.

Nae Mwalimu Said Hamad Ramadhan kwa niaba ya Wazee wa Wilaya hiyo alimkaribisha Mkuu huyo mpya wa Wilaya ya Kusini Unguja na kumueleza kwamba, kwa niaba ya wazee wote wa wilaya hiyo wamempokea na wako tayari kufanya kazi nae pamoja na kushirikiana nae wakati wote.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Abdulazizi Hamad Ibrahim akitoa neno la ukaribisho kwa Mkuu wa Wilaya hiyo kwa niaba ya chama hicho Wilaya, aliahidi kumpa ushirikiano mkubwa Mkuu wa Wilaya huyo mpya na kusisitiza kwamba juhudi za makusiudi zitachukuliwa katika kuhakikisha Ilani ya Uchaguzi ya CCM inatekelezwa kwa vitendo.

Mapema Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Mbaraka Omar Kasongo alimuahidi Mkuu wa Wilaya huyo ushirikiano mkubwa ili ofisi hiyo iweze kutekeleza kwa vitendo maono ya Serikali ya Awamu ya Nane chini ya uongozi wa Rais Dkt. Mwinyi katika kuwatumikia wananchi ambapo tayari ishara kubwa ya mafanikio na maendeleo zimeanza kuonekana.

Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja aliteuliwa Agosti 3, mwaka huu 2022 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi na kumuapisha mnamo Agosti 5,2022 katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news