DC Mkasaba:Makarani wa Sensa hakikisheni mnatunza siri za wananchi mtakaowahesabu

NA DIRAMAKINI

MKUU wa Wilaya ya Kusini, Rajab Yussuf Mkasaba amewataka Makarani wa Sensa ya Watu na Makaazi kuhakikisha wanatunza siri za wananchi wanaokwenda kuwahesabu kama sheria ya Takwimu zinavyoelekeza.
Mkuu wa Wilaya ya Kusini aliyasema hayo mara baada ya kushuhudia kiapo na ujazaji mkataba kwa Wasimamizi Maudhui, Wasimamizi Tehama pamoja na Makarani, hafla iliyofanyika katika kituo cha mafunzo ya Sensa Skuli ya Sekondari Mtule, iliyopo Paje Mkoa wa Kusini Unguja.

Katika maelezo yake Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka watendaji hao waliokula kiapo kuhakikisha wanakwenda kutekeleza vyema majukumu yao kwa wananchi kama mafunzo yalivyowaelekeza huku wakihakikisha taarifa za wananchi zinakuwa ni za siri kama inavyoelekeza Sheria ya Takwimu Sura ya 351.
Aliwataka kuhakikisha wanatoa ushirikiano mzuri kwa wananchi ili waweze kupata taarifa sahihi wanazozihitajia ili ziweze kusaidia katika malengo yaliyokusudiwa.

Sambambana hayo, Mkuu huyo wa Wilaya aliwasihi watendaji hao kuhakikisha wanatumia lugha nzuri wakati wote wa utekelezaji wa zoezi hilo kwa wananchi ili waweze kupata taarifa wanazozitaka kwa ufanisi zaidi.

Nae Mratibu wa Sensa ya Watu na Makaazi wa Wilaya ya Kusini, Mhina Khamis Omar aliwataka watendaji hao kufuata maelekezo pamoja na nasaha walizopewa na Mkuu huyo wa Wilaya ili waweze kutekeleza vyema majukumu yao sambamba na kufanikisha vyema zoezi hilo muhimu la Kitaifa ambalo litasaidia kupanga na kupeleka maendeleo kwa wananchi.

Post a Comment

0 Comments