Dodoma Jiji, Njombe Mji zaongoza

NA GODFREY NNKO

HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imeongoza katika halmashauri zinazotenga asilimia 60 kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa kutumia asilimia 65 ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze asilimia 62 na Jiji la Arusha asilimia 62.

Aidha, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi imekuwa ya mwisho kwa kutumia asilimia 34 ikifuatiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni asilimia 47 na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro asilimia 49 ya mapato yasiyolindwa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhesshimiwa Innocent Bashungwa ameyasema hayo leo Agosti 2, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa kuhusu mapato na matumizi ya ndani ya halmashauri kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Amefafanua kuwa, katika matumizi ya miradi ya maendeleo Mamlaka za Serikali za Mitaa zimegawanywa katika makundi mawili katika kuchangia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kutokana na mapato ya ndani yasiyolindwa.

Mheshimiwa Waziri Bashungwa amesema, Kundi la kwanza ni Halmashauri 17 zinazopaswa kuchangia asilimia 60 na kundi la pili ni Halmashauri 167 zinazopaswa kuchangia asilimia 40.

Uchambuzi wa taarifa za matumizi ya fedha za mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2021/22, kwa mujibu wa Waziri Bashungwa unaonesha kuwa halmashauri zimetumia Shilingi Bilioni 297.7 katika kutekeleza miradi ya maendeleo sawa na asilimia 43 ya mapato yasiyolindwa ambayo ni Shilingi Bilioni 689.5.

Halmashauri tatu zimetumia asilimia 60 au zaidi ya kiasi cha mapato yasiyolindwa, halmashauri 42 zimetumia kati ya asilimia 40 hadi 59 na halmashauri 139 zimetumia chini ya asilimia 40.

Asilimia 40

Akizungumzia, halmashauri zilizotenga asilimia 40 kwenye miradi amebainisha kuwa,katika kundi hili Halmashauri ya Mji wa Njombe imeongoza kwa kutumia asilimia 51 ikifuatiwa na Halmashauri ya Mji wa Tunduma na Halmashauri za Wilaya za Njombe na Mkuranga ambazo zimetumia asilimia 46 ya mapato yasiyolindwa.

Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti imekuwa ya mwisho kwa kutumia asilimia 16 ikifuatiwa Halmashauri za Wilaya za Gairo na Bunda ambazo zimetumia asilimia 17 ya mapato yasiyolindwa.

Uchambuzi wa matumizi unaonesha kuwa zipo baadhi ya Halmashauri ambazo zinauwezo mkubwa wa kuchangia zaidi ya kiwango cha chini kilichowekwa cha asilimia 40 au 60. Hivyo, katika mwaka wa fedha wa 2022/23 Halmashauri 5 zimewekwa kwenye kundi la kuchangia asilimia 70 kwa mwaka.

Mikopo

Waziri Bashungwa amefafanua kuwa, uchambuzi wa taarifa za matumizi ya fedha za mapato ya ndani kwa kipindi cha Julai 2021 hadi Juni 2022, unaonesha kuwa Halmashauri zimechangia Shilingi Bilioni 59.2 kwenye Mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, ambayo ni asilimia 9 ya mapato yasiyolindwa Shilingi Bilioni 674.8.

Taarifa zinaonesha kuwa Halmashauri 48 zimechangia asilimia 10 au zaidi, Halmashauri 135 zimechangia kati ya asilimia 5 hadi 9 na Halmashauri 1 imechangia chini ya asilimia 5 kwenye mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu.

Aidha, taarifa zinaonesha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli, Kilindi na Tandahimba zimeongoza kwa kuchangia asilimia 12 zikifuatiwa na Halmashauri za Majiji ya Arusha, na Dar es Salaam, Halmashauri za Wilaya ya Hai na Madaba asilimia 11.

Waziri Bashungwa amesema kuwa, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha imekuwa ya mwisho kwa kuchangia asilimia 3 ikifuatiwa na Halmashauri za Wilaya ya Morogoro, Chato, Bukombe, Masasi na Nkasi ambazo zimechangia asilimia tano.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news