Hamasa ya Sensa yapamba moto Manispaa ya Musoma

NA FRESHA KINASA

HALMASHAURI ya Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara imezindua kampeni ya uhamasishaji na uelimishaji wananchi kujitokeza kushiriki kikamilifu kuhesabiwa siku ya sensa itakayofanyika Agosti 23, mwaka huu.
Uzinduzi huo umefanywa na Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt. Halfan Haule Agosti Mosi, 2022 katika soko la Saa Nane Kata ya Mshikamano Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali,viongozi wa dini, chama pamoja na wananchi.

Akizungumzia na wananchi waliojitokeza katika uzinduzi huo Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Mheshimiwa Dkt.Halfan Haule amesema, lengo la Sensa ya Watu na Makazi ni kupata taarifa sahihi za kidemografia, kijamii, kiuchumi, na hali ya mazingira kwa lengo la kupata takwimu sahihi zitakazo iwezesha Serikali kupanga kwa usahihi Mipango ya Maendeleo ya watu wake katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, hali ya ajira, miundombinu, nishati na maji safi.
Amesema, kwa mantiki hiyo, sensa ni zoezi muhimu ambalo kila mmoja kwa nafasi yake analazimika kushiriki na kutimiza wajibu wake ili kuhakikisha inakuwa na mafanikio makubwa katika kuisaidia Serikali kutimiza wajibu wake kwa wananchi kulingana na idadi ya watu wa eneo husika ukiwa kama msingi mkubwa wa utoaji wa maendeleo kwa kila eneo.

Mheshimiwa Dkt.Halfan Haule ameongeza kuwa, iwapo mkuu wa kaya hatakuwepo aache taarifa sahihi za watu wote katika kaya kwa mtu mzima aliyepo kusudi karani wa sensa na Mwenyekiti au kiongozi wa mtaa au kitongoji afikapo wapewe taarifa zote zinazohitajika.
"Watauliza pia kiwango chako cha elimu, shughuli zako, taarifa za ulemavu, Hali ya uzazi, taarifa za umiliki wa ardhi, taarifa za vifo na vifo vitokanavyo na uzazi, hali ya nyumba, anwani za Makazi, taarifa kuhusu Mpango wa TASAF, umri, jinsi, hali ya ndoa, taarifa za uhamiaji, taarifa za vitambulisho vya taifa na uhai wa Wazazi, taarifa za majengo niwaombe toeni taarifa kwa ushirikiano wa dhati kufanikisha Jambo hilo muhimu kwa nchi yetu,"amesema Dkt.Haule.

"Kujibu maswali ya Sensa ni matakwa ya kisheria kwa mujibu wa sheria ya takwimu sura namba 351. Ushirikiano wako na karani wa sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kwa kutoa taarifa sahihi ndio utakaorahisisha na kufanikisha sensa ambapo matokeo yake yatachochea kasi ya maendeleo ya watu na Makazi yao katika maeneo yote ya utawala nchini,"amesema Dkt.Haule.
Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, Mheshimiwa Vedastus Mathayo amewataka wananchi wa jimbo hilo kutolihusisha zoezi la sensa na imani za kishirikina, bali wote wahesabiwe.

"Serikali inataka ikileta fedha ilete kulingana na watu wa Musoma, Serikali inataka ikileta huduma mbalimbali ilete kulingana na idadi halisi ya wananchi. Niwaombe watu wote wa musoma Mjini tuendelee kuhamasishana siku ya sensa tuhesabiwe, hii pia inanipa Mimi nguvu kwenda bungeni na kusema nina Wananchi kadhaa mtaona kuanzia mwaka kesho napata fedha nyingi za masoko, zahanati na huduma mbalimbali." amesema Mheshimiwa Mathayo.
Mratibu wa Sensa Mkoa wa Mara David Danda amewataka wakuu wa Kaya na Wananchi wote kutowaficha Watu wenye ulemavu siku ya sensa bali wawape fursa ya kuhesabiwa kwa ajili ya Maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

Danda amesema kuwa, Kila mwananchi ahakikishe siku ya sensa anahesabiwa bila kukwepa au kukosa kwani sensa ni muhimu katika kuiwezesha serikali kupata idadi kamili ya Watu kwa ajili ya kupanga mipango na namna bora ya kuwahudumia.
Naye Mkufunzi wa Sensa Mkoa wa Mara, William Matee amesema kuwa Siku ya sensa kila mwananchi ahakikishe anahesabiwa Mara moja tu, na pia ameomba Wananchi wote kutoa taarifa sahihi kwa makarani wa sensa watakaopita Kila kaya na watoe ushirikiano wa dhati kwa makarani ili kufanikisha jambo hilo muhimu.
Katika uzinduzi huo, baadhi ya wananchi wamepata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali yahusuyo sensa na wamejibiwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news