HGWT yatumia Maonesho ya Utalii wa Kitamaduni kufikisha elimu ya ukatili wa kijinsia Serengeti

NA FRESHA KINASA

SHIRIKA la Hope for Girls and Women in Tanzania ( HGWT) linalojishughulisha na mapambano ya ukatili wa kijinsia na kutetea haki za binadamu lenye makao makuu yake Mugumu Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara limefanikiwa kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia kwa zaidi ya watu 7,000. 

Ni katika Maonesho ya Utalii wa Kitamaduni (Serengeti Cultural Centre) ambayo yalifanyika uwanja wa Right to Play uliopo Mugumi wilayani humo kuanzia Julai 25, 2022 hadi Julai 29, 2022.
Afisa Mwelimishaji Jamii kutoka Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Emmanuel Goodluck ameiambia DIRAMAKINI kuwa, elimu hiyo ilitolewa kwa watu waliofika katika banda la shirika hilo ambapo pia Filamu ya 'Kwa Jina la Binti Yako' (In the Name of Your Daughter) iliweza kutazamwa na watu kipindi chote cha maonesho.

Pia wananchi walipata elimu ya madhara ya ukatili wa kijinsia kupitia filamu hiyo pamoja na kupewa vipeperushi vyenye jumbe mbalimbali za kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.

"Tulitoa elimu na ufafunuzi wa kina tukieleza maana ya ukatili wa kijinsia, aina za ukatili wa kijinsia, njia za kutokomeza ukatili wa kijinsia, adhabu kwa wahusika wa vitendo vya ukatili wanaotiwa hatiani, kwa nini watu wanakumbatia mila ya ukeketaji, madhara ya ukeketaji, ndoa za utotoni na aina mbalimbali za ukatili wa Kijinsia," amesema Goodluck.

"Tuliwaeleza sehemu za kuripoti taarifa za ukatili wa kijinsia haraka, tukawapa namba ya kutoa taarifa za ukatili, jambo jingine tuliwahimiza wananchi umuhimu wao katika kupambana na ukeketaji hasa kipindi hiki cha likizo ambacho baadhi ya wazazi hutumia mwanya wa likizo kukeketa watoto wa kike pamoja na kazi za shirika chini ya Mkurugenzi wa HGWT, Rhobi Samwelly ambazo limeendelea kuzifanya ikiwemo kutoa hifadhi kwa mabinti wanaokimbia ukeketi na kuja Kituo cha Hope Mugumu Nyumba Salama na Butima Nyumba Salama,"amesema.

"Pia kuwasaidia kwa kuwaendeleza kielimu na kifani wanaokimbia ukeketaji kutoka katika familia zao na kuja katika vituo kikiwemo Kituo cha Hope Mugumu na Butiama Nyumba Salama, sambamba na kuwapa msaada wa kisaikolojia na mafundisho ya kiroho katika kuwajenga na kuwaimarisha waishi kwa amani na utulivu tukiwa nao," amesema na kupongeza kuwa.

"Shabaha yetu kubwa ni kuona ukeketaji na ndoa za utotoni hauna nafasi kabisa katika Wilaya ya Serengeti na wasichana (watoto wa kike) wote wanapata fursa ya elimu kufikia ndoto zao na pia tulihimiza wananchi kuwa mabalozi katika kuwafichua mbele ya sheria wanaoendekeza ukeketaji. Kwa sababu wapo katika jamii sambamba na kuwataka wazee wa kimila kuunga mkono juhudi za Serikali, kwani wanaaminika na kuheshimika na wakikemea pia itasaidia sana kufanikisha,"amesema.

Aidha,amesema kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali na wananchi wote katika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia na pia ameomba wananchi kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba watoto wa kike wanalindwa na kuthaminiwa. Hasa kipindi hiki cha likizo ikizingatiwa kuwa, mwaka huu unagawanyika kwa mbili hivyo ukeketaji lazima upigwe vita na kila mtu.

Akizungumza akiwa katika banda la Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania wakati wa ufunguzi wa maonesho ya Utalii wa Kiutamaduni (Serengeti Cultural Centre) Julai 27, 2022 mgeni rasmi katika ufunguzi huo Katibu Tawala Wilaya ya Serengeti, Mheshimiwa Cosmas Qamara alipongeza juhudi zinazofanywa na Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania katika mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia wilayani humo.
Aidha, Mheshimiwa Qamara aliwataka wananchi kuachana na mila ya ukeketaji kwani madhara yake ni makubwa ikiwemo kuchangia ndoa za utotoni, maumivu makali wakati wa kukeketwa, kutokwa damu nyingi wakati wa kukeketwa na hivyo kupelekea kifo, hatari ya kupata magonjwa ya kuambukiza, madhara ya kisaikolojia, ulemavu na kukosa kujiamini. 

Huku akisema serikali wilayani humo imejipanga kuwawajibisha wale wote watakaobainika kuwakeketa wasichana kwani ni kinyume cha sheria za nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news