Mbunge Prof.Muhongo atoa saruji ujenzi zahanati, vyumba vya madarasa

NA DIRAMAKINI

MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara, Prof. Sospeter Muhongo ametoa saruji mifuko 200 yenye thamani ya shilingi milioni 4.5 kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa zahanati tatu na vyumba vipya viwili vya madarasa ndani ya Kata ya Bukumi.
Wasaidizi wa Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini wamekabidhi mifuko hiyo ya saruji kwa viongozi wa Kata ya Bukumi siku ya Agosti 3, 2022.

Ambapo Prof. Muhongo ametoa mifuko 50, kwa kila zahanati na mifuko mingine 50 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vipya viwili vya madarasa katika Shule ya Msingi Busekera na hivyo kufanya jumla ya mifuko 200 aliyoitoa.

Kata ya Bukumi ina vijiji vinne ambavyo ni Buira, Bukumi, Buraga na Busekera ina zahanati moja tu, ambayo iko kwenye Kijiji cha Buraga, Kitongoji cha Kurugee.

Vijiji vingine vitatu vimeamua kujenga Zahanati zake na ujenzi tayari umeanza kwa kasi ya kuridhisha katika kuhakikisha huduma za afya zinaimarika.
Ambapo michango ya wanavijiji hivyo ni nguvu kazi, fedha taslimu shilingi 10,000-15,000. Huku diwani wa kata ya Bukumi Mheshimiwa Munubhi Musa akichangia Shilingi 300,000 ambapo kila Kijiji kikipata shilingi 100,000.

Aidha, michango mingine ya Mbunge Prof. Muhongo kwenye Sekta ya Afya ndani ya Kata hiyo ni gari la Wagonjwa (Ambulance) kwa Zahanati ya Kurugee, Kijijini Buraga Saruji Mifuko 100 kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Bukumi inayojengwa kwenye Kitongoji cha Kukema Burungu.

Wananchi wa Jimbo la Musoma Vijijini wamempongeza Mbunge Prof. Muhongo kwa kuendelea kuchangia maendeleo jimboni humo kwa kuzigusa sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, kilimo, michezo, pamoja na ushiriki wake katika masuala mbalimbali ya kijamii.

"Tunamshukuru sana Prof. Muhongo kwa kuendelea kutuunganisha wananchi wa Musoma Vijijini katika masuala ya maendeleo,amekuwa mstari wa mbele kuchangia mambo mengi katika elimu kuna michango yake mingi, kwenye afya pia, kusaidia mbegu na zana za kilimo kwa wananchi, kuanzishwa mashindano na michezo mbalimbali, kutuhamasisha wananchi kushiriki katika maendeleo tukishirikiana na Serikali yetu. Hakika mbunge wetu ni chachu kubwa ya maendeleo ya Jimbo letu tunamuahidi ushirikiano wa dhati,"amesema Neema Pius.

"Musoma Vijijini tunajivunia kuwa na Mbunge ambaye amekuwa akitushirikisha wananchi kuhakikisha kwamba tunapiga hatua mbele za kimaendeleo. Prof. Muhongo anaposema jambo lazima atimize ahadi hii ya saruji mifuko 200 alisema siku ya uzinduzi we hamasa na uelimishaji jamii kushiriki kuhesabiwa siku ya sensa ilikuwa ni Julai 30, 2022 pale Busekera na kweli ametekeleza kwa vitendo yapo mengi ambayo ameshiriki kuyafanya ya kimaendeleo akishirikiana na wananchi na serikali katika kulifanya jimbo letu lizidi kusonga mbele,"amesema James Hezron.
Jimbo la Musoma Vijijini lina Kata 21 zenye jumla ya Vijiji 68. vituo vya afya vitatu, Zahanati za serikali 23, Zahanati binafsi 4, Zahanati za vijiji zinazojengwa 17,Vituo vya afya vinavyojengwa 3, pamoja na Hospital ya Wilaya ambayo bado inajengwa.

Post a Comment

0 Comments