Hii ndiyo NHIF Tanzania, Konga asema wapo imara

NA GODFREY NNKO

AGOSTI 11, 2022 Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Bw.Bernard Konga akiwa pamoja na wasaidizi wake wameketi na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Ni kupitia kikao kazi ambacho ni sehemu ya vikao vya wadau viliyopangwa na mfuko ili kutoa elimu juu ya maboresho yanayofanywa na sababu zake, huku akielezea mfuko umetoka wapi,wako wapi na wanaelekea wapi kwa sasa.

"Mwaka jana ulikuwa mwaka maalumu kwetu, tuliadhimisha miaka 20 ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya tulikuwa na mengi ya kusema. Tunaendelea na mkutadha huo huo wa kusema tumetoka wapi, tuko wapi na tunaelekea wapi ili kuweza kutoa picha ya mfuko tukoje kwa sasa na kama Serikali mipango hasa inayohusu taasisi hii na dhana hii ya bima ya afya, mwelekeo wake ukoje na tuko wapi na tunatarajia nini tunako taka kufika huko.

"Mpaka kufikia mwezi Juni, 2022 mfuko unahudumia takribani wanachama milioni 4,821,233 ikilinganisha na wanachama milioni 4,550,000 kipindi kama hicho mwezi Juni 2021, kwa hiyo wanachama milioni nne na laki nane ni wanachama wachangiaji pamoja na wale wanufaika.

Ni asilimia 15 tu

"Hii inafanya asilimia nane ya Watanzania wanaohudumiwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya. Tukisema Bima ya Afya nchini mfumo una maeneo makubwa matatu, moja ni mfumo wa Taifa wa Bima ya Afya, mbili Mfuko wa Afya ya Jamii na tatu bima binafsi.

"Kama nchi mpaka sasa tuna asilimia 15 ya Watanzania wanaohudumiwa kwenye mfumo wa bima ya afya, asilimia 8 inachukuliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, asilimia sita inachukuliwa na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na asilimia moja bima binafsi,"amesema Bw.Konga.

Malengo yametimia?

"Kimsingi bado tunaona kama nchi hatujafika tunakotaka kufika kwa sababu lengo tunatamani kila Mtanzania awe na bima ya afya, sasa hivi ni asilimia 15 kwenye mfumo,hii inamaanisha asilimia 85 leo hii wanapata matibabu kupitia bajeti kutoka mfukoni.

"Kama Serikali tunaona bado tuna kazi kubwa ya kufanya na tuna mipango ambayo inafanyika ndani ya Serikali kuona namna gani hili linakwenda.

NHIF inafanya nini?

"Kama mfuko tunaendelea kutoa elimu ya Bima ya Afya kwa wananchi kuelezea manufaa na faida ya kuwa na Bima ya Afya.

"Lakini sasa katika hao milioni nne na laki nane ambao ni asilimia 100 wale ambao tunawahudumia takribani asilimia 66 ni watumishi wa umma, mtakumbuka mfuko ulivyoanza mwaka 2001 lengo ilikuwa ni watumishi wa umma kuingia kwa lazima na hao wote wameingia kwa lazima, na asilimia iliyobaki imegawanyika kwenye makundi mbalimbali kama sekta binafsi asilimia 16.9.

"Wanafunzi wote sasa hivi wanaingia wote wa vyuo, wanaingia kwa lazima asilimai 7.15. Watoto asilimia 4.2 yapo makundi mbalimbali, lakini asilimia kubwa inabebwa na watumishi wa umma.

Bima kwa wengi

"Nitumie fursa hii kusema kwamba kupitia kundi hili Serikali imeona namna pekee ya kuweza kufanikisha Bima ya Afya sasa ni kujifunza kupitia kundi hili la watumishi wa umma kwa sababu wanaingia kwa lazima, inamaana wote tunaingia kwa pamoja inatusaidia kwamba hatusubiri mtu akiwa anaumwa ndio ajiunge.

"Mtumishi wa umma akishapewa barua yake ya ajira, mshahara wake wa kwanza tayari kuna makato ya NHIF na hilo ndilo kundi limesaidia kuuweka mfumo hai na kuwa na nguvu.

"Kwa sababu Bima ya Afya inatutaka kuingia kwenye utaratibu kabla ya kuugua, bahati mbaya wengi wanasubiri wakishaugua ndipo wajiunge kwenye Bima ya Afya sasa wale wanarudisha nyuma dhana nzima ya Bima ya Afya," amesema Bw.Konga.

Uendelevu

"Kupitia kundi hili mfuko (NHIF) umeendelea kuwa endelevu sana, Serikali imekuwa ikihakikisha hawa na wategemezi wao michango yao inakwenda kwa wakati kwa takwimu za haraka haraka tu tangu mwaka 2016 hatujawahi kuwa na deni lolote kwa Serikali.

"Serikali imekuwa ikiwasilisha kwa wakati michango ya watumishi. Lakini makundi mengine bahati nzuri yamekuwa yakichangia kabla ya huduma,changamoto ni moja tu yamekuwa yakiingia kwa uhiari na katika uhiari huo wengi unakuta tayari ana mwelekeo wa kuugua, kitu ambacho kinarudisha nyuma malengo ya kuanzishwa kwa mfuko.

"Kupitia takwimu hii, Serikali inaandaa mpango kabambe kwa kuwa na kundi kubwa ambalo linaingia katika utaratibu huu ambao watumishi wa umma wamekuwa wakiingia nao,"amesema Bw.Konga.

Vyanzo vya mfuko

Bw. Konga anasema kuwa, "Mfuko tuna vyanzo vikubwa vitatu ikiwemo michango, uwekezaji pamoja na mapato yatokanayo na vyanzo vinginevyo.

"Kwenye eneo la michango nalo tumeendelea kufanya vizuri mpaka kufikia mwezi Juni kuna ongezeko la fedha zikizokusanywa mathalani mpaka kufikia mwaka jana tulikuwa tumekusanya shilingi bilioni 489.4, lakini kwa hesabu tulizonazo mpaka sasa kabla ya CAG (Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) kukagua, maana baadaye CAG anakuja kukagua tumekusanya takribani shilingi Bilioni 529.

"Sasa hizi figures kwa baadaye zikikaguliwa tutakuja kusema hesabu zilizokaguliwa, lakini kwa hesabu zetu tunaona tayari kuna ongezeko la fedha kwa maana ya makusanyo yatokanayo na makusanyo ya wanachama,"amesema Bw.Konga.

"Hii inamaanisha kwamba kumekuwa na nyongeza ya michango, makusanyo mwaka hadi mwaka, lakini kwa upande mwingine tumeendelea kupata fedha kutokana na uwekezaji.

"Kama taasisi tuna jukumu la kukusanya michango na kuhakikisha tunawekeza, kwa sababu biashara ya bima unalipa leo shilingi 10 na unakuja kutibiwa kesho thamani ya fedha ya leo na kesho inatofautiana, lazima uwekeze eneo ambalo utapata kiwango fulani cha fedha za kuendesha taasisi kwa maana ya kulipia gharama,"amesema Bw.Konga.

Mkurugenzi Mkuu huyo amefafanua kuwa, "Kwa kifupi kwenye eneo la michango tunaendelea kukamilisha hesabu zetu vizuri, tutatoa taarifa baada ya Mkaguzi Mkuu kupita kukagua, lakini bado tunaona kuna nyongeza ya michango ikilinganisha na kipindi kilichopita.

Matumizi

"Kwenye eneo la matumizi kama mfuko, tuna matumizi ya maeneo matatu eneo la kwanza ni kulipia matibabu hili ni eneo linalochukua fedha nyingi sana ya fedha ambazo huwa zinakusanywa na mfuko.

"Mnafahamu gharama za matibabu zinakuwa juu siku hadi siku, teknolojia ya kutambua magonjwa inabadika kila leo na magonjwa mapya yanakuja kila leo, miaka 10 iliyopita tulikuwa hatuzungumzii kuhusu UVIKO-19. Sasa imeshaingia kuitambua kuna taratibu zake.

"Kasi ya maambukizi nayo ilikuwepo hapo katikati ninashukuru Mungu sasa hivi tumetulia baada ya chanjo kupita...kwa hiyo kwa ujumla wake matumizi kwenye eneo la matibabu yameendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka.

"Ndiyo maana tuna jitihada mbalimbali zinafanyika kuona eneo la matumizi linakwenda kupungua, ndilo eneo linaangalia zaidi ustawi huu na uendelevu wa mfuko,"amesema Bw.Konga.

Vituo vya huduma

"Kwenye eneo jingine la vituo vya kutolea huduma tumeendelea kusajili mwaka hadi mwaka, kwa sababu ni suala letu la msingi sana.

"Mathalani kama mfuko mwaka 2020/2021 tulikuwa na vituo 8482, lakini mpaka mwezi Juni tuna vituo 9178 na vituo hivi vinaanzia ngazi ya zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, maduka ya dawa, kliniki, Hospitali ya Taifa, zote zinaingia humu ndani, vituo hivi vinamilikiwa na Serikali, sekta binafsi ambayo inajiendesha pasipo kutarajia kupata faida na vile ambavyo vinatarajia kupata faida.

"Vile vya kidini ambavyo si vya faida vipo asilimia tisa, vya Serikali asilimia 70, vya binafsi asilimia 21. Takwimu hizi zinaonesha kama mfuko tuna wigo mpana wa kutoa huduma mnakumbuka mfuko ulivyoanza ulianza na kundi la walimu ambao wametapakaa nchi nzima vijijini, tunakotoka zimejaa shule kwa hiyo tuna jukumu la kuhakikisha wanapata matibabu kuanzia huko na inakuja mpaka ngazi ya Taifa kulingana na mahitaji yao.

"Hi ndiyo imetupa nguvu kama mfuko leo hii tunakuwa na uwezo wa kuwa na wanachama wengi kwa sababu mtu ni mwajiri yuko Dar es Salaam ana ofisi popote tuna uhakika wa kumhudumia kutokana na na idadi ya vituo ambavyo tunavyo 9,178 na tumeona mwamko mkubwa sana wa watu kujitokeza kwenye afya.

"Kama mfuko tunaendelea, tunajumuisha vituo vingi kadri iwezekanavyo katika kuwezesha kupatikana kwa huduma za matibabu kwa wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya,"amesema.

Eneo lingine

"Eneo jingine tunaloliangalia ni namna gani sasa hawa tulioingia nao mkataba wananufaika na huduma au malipo ambayo tunafanya, bado tunaona ushiriki wa sekta binafsi katika utoaji wa huduma za afya ni wa kiwango cha juu sana. Mnakumbuka kama nchi tulikubali kuingia kwenye mashirikiano baina ya sekta ya umma na binafsi.

"Baadaye tukaingia makubaliano na sekta binafsi, kwa hiyo tunaona sisi tunavyozidi kwenda vituo vya sekta binafsi vinaendelea kunufaika na mfuko huu wa Bima ya Afya. Na tunaangalia kiasi ambacho sekta binafsi ambacho inapokea mfano kwa mwaka uliopita Juni 2022 wastani wa asilimia 42 ya fedha zote tulikuwa tumezilipa;

"Hii inamaanisha nini? Wanachama wetu wana wigo wa kuchagua kwenda kupata huduma sehemu ambayo anaona yeye.

Ustawi wa huduma

"Niseme kupitia takwimu hizi vituo vya vya Serikali vinazidi kunyanyuka ikilinganisha na kipindi kilichopita baada ya maboresho makubwa yaliyofanyika kwa maana ya ujenzi wa miundombinu, ukarabati, upatikanaji wa huduma, pamoja na vifaa katika hospitali za serikali, upatikanaji wa dawa tumeona Serikali nayo ikipata shares kubwa kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya maana inaonesha sasa dhana ya ushindani katika utoaji wa huduma bora inazidi kuimarika.

"Tunaona sasa hivi huduma nyingi ambazo zilikuwa zinapatikana nje ya nchi na wanachama wetu walikuwa wakifika hatua inabidi waende nje ya nchi sasa hivi zinapatikana nchini. Ni suala la kuipongeza Serikali kwa mikakati mizuri, kwa hiyo vituo vya Serikali vinapata share kubwa kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

Huduma zinazokula fedha

"Hapa tunazungumzia ni kwa asilimia nane tu kwa wale ambao wanakuwa wakilipa fedha kutoka mfukoni, tunaona sasa vituo hivi vinapata fedha nyingi na mwisho wa siku vinaweza kujiendesha. Lakini pia kama mfuko tunavyolipa fedha kwenye vituo tunaangalia tunalipia zaidi kwenye eneo gani, eneo mojawapo tunaloona fedha nyingi tunalipia ni kwenye eneo la dawa.

"Tunafahamu ukienda hospitali ukipewa dawa ndio unaona matibabu yako yamekamilika kwa hiyo na sisi kama mfuko kwa mwaka uliopita tumelipa kwenye eneo la dawa takribani shilingi bilioni 250 kati ya shilingi bilioni 564 ambazo tumelipa kwenye vituo.

"Kiasi kikubwa tunalipa zaidi kwenye dawa, kwenye vipimo na consultation fee, kwa sababu mwanachama wetu sisi ana uwezo wa kuwaona madaktari wa ngazi zote Clinical Officer, kwenda mpaka kwa daktari bingwa mbobezi wote anaweza kwenda kuwaona.

"Katika mfumo wa afya tumezungumzia kuhusu zahanati mpaka Hospitali ya Taifa, katika mwelekeo huo tunalipa wapi fedha zaidi?

"Kwa mwaka wa fedha uliopita fedha nyingi tumelipa kwenye Hospitali za Kanda na hii pia inatoa picha nzuri zaidi kwa sababu siku za nyuma tulikuwa tunalipa ngazi ya Taifa sasa hivi tunalipa zaidi ya asilimia 23 kwenye hospitali za ngazi za kanda hizi ni KCMC, Bugando, Hospitali ya Kanda Mbeya, Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma, na Hospitali ya Mtwara ambayo imefunguliwa siku za hivi karibuni na Hospitali ya Chato hizo ndizo hospitali za kanda," amesema Bw.Konga.

Kuimarika huduma

"Kwa hiyo tunaona kuimarika kwa huduma katika Hospitali za Kanda na sasa wanachama wetu wanapatahuduma za kibingwa na za kibobezi karibu na maeneo yao sio wote wanahitaji kusafiri kuja Dar es Salaam, mathalani huduma za saratani, kusafisha figo (Dylisis) zamani ilikuwa lazima uje Muhimbili sasa hivi unazipata Bugando, KCMC,Mbeya Rufaa, Benjamin Mkapa.

"Hii yote inaonesha mfumo wa afya unaimarika na huduma zinasogea karibu na wanachama wetu. Eneo la pili ambalo tumelipa zaidi ni hospitali za rufaa, tumelipa takribani asilimia 20 na haya yote yanaonekana kutokana na uwekezaji uliofanywa na Serikali yetu,"amesema Bw.Konga.

Pia anfafanua kuwa, "Asilimia 20 tumelipa kwenye hospitali za ngazi ya mkoa na hii inatuonesha kwamba hizi afua zinazofanywa na Serikali moja kwa moja zinazidi kusogeza huduma kwa wananchi na kwa wanachama wetu nao wananufaika kupitia hizo.

"Kama nilivyosema sekta binafsi kuna utaratibu wa kliniki ambazo wanafungua madaktari nazo ni asilimia 17 na Hospitali za Taifa tunazungumza Ocean Road, Muhimbili JKCI tumeweza kulipa takribani asilimia 17, tunaona huduma zikiendelea kusogea, tunaamini siku zijazo kutoka Hospitali za Mikoa hadi Hospitali za Wilaya tutajikuta tunalipa zaidi ikilinganishwa zaidi na siku za nyuma ni wazi kwamba huduma zinaendelea kusogea karibu na wananchi na wanachama wetu wananufaika zaidi.

Magonjwa mzigo

"Lakini kama mfuko tuna utaratibu wa kuangalia tunalipia kwenye huduma zipi, magonjwa yapi katika kipindi kilichopita 2021/2022 tumeona magonjwa mengi yasiyo ya kuambukiza fedha nyingi zinatumika kwa hiyo hapa panaonesha mwelekeo wa Serikali ni sahihi kuongeza jitihadi za kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

"Mathalani kwa mwaka uliopita fedha nyingi tumelipia kwenye dawa za saratani, tunafahamu haya ni magonjwa yanayotokana na chakula tunachokula, mtindo wa maisha tunaoishi na huko pia tumelipa gharama za kuchuja damu (Dylisis) takribani shilingi Bilioni 35.4 zililipwa kwenye eneo hili, kwa kifupi magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni mzigo mkubwa ni suala la kitaifa linazungumzwa hasa wanachama wetu wengi tunagharamia fedha nyingi kulipa huko.

"Wanachama wetu wengi tunagharamia fedha nyingi kuelekea huko. Ni jukumu letu kama mfuko kuunga mkono jitihada za Serikali katika katika kupambana na haya.

"Zamani tulikuwa tunaugua malaria siku tatu unakwenda kazini, leo hii ukianza matibabu ya figo inamaana ni life time na gharama za kusafisha figo zinakwenda shilingi 240,000 au 250,000 na unaweza ukaambiwa session nne kwa wiki ukienda kwa mwaka ni takribani shilingi milioni 52.

"Katika hali ya kawaida ni gharama kubwa sana na yakishaingia utokaji wake si rahisi, na hata kuyachunguza kwamba yapo yana gharama zake na ni magonjwa ambayo ni endelevu, kwa hiyo kama mfuko tutaendelea kuunga mkono jitihada hizo na kuhakikisha wanachama wetu hawaingii huko kwa kutoa elimu kutokana na gharama zake.

Makundi yanayoongoza

"Kama mfuko tunaangalia katika makundi tuliyonayo ni kundi lipi linatumia zaidi huduma za afya ni wazi tunaona unapokuwa na miaka 0-5 muda mwingi ni hospotali na unapokuwa na miaka 60 na zaidi unakuwa mhudhuriaji mzuri wa hospitali.

"Kwa hiyo tunaona mfuko unatumia fedha nyingi kwa watoto na wazee zaidi ya miaka 60, takwimu zetu zinaonesha fedha asilimia 29 tunahudumia wazee zaidi ya miaka 60 na mtakumbuka kwamba mfumo kuna fao la wastaafu waliokuwa kwenye sekta ya umma, kwa hiyo tunawahudumia kama nchi huduma zimeimarika mfumo wa maisha umeimarika life expectancy ya Tanzania imeongezeka na tunaona gharama kubwa zinakwenda hiko,"amefafanua Bw.Konga.


Wakati huo huo, Bw. Konga kupitia mkutano huo alitoa ufafanuzi hoja ambazo zimekuwa zikijitokeza. "Nimezungunzia kuhusu Serikali maana ina watumishi wengi na sekta binafsi nayo imekuwa ikitoa michango yote, lakini changamoto sekta binafsi sio wote wameingia, kwa hiyo juhudi zimeendelea kufanywa ili nao wote waingie kwenye mfuko huu.

Ushindani

"Kuna suala la ushindani ambalo limewekwa vizuri tu, kwa nia njema baina ya mfuko na makampuni binafsi, kwa hiyo tunashindana huko huko kutafuta wanachama kwa hiyo wanaotuelewa wanakuja kwetu na wengine wanakwenda huko.
 
"Tunaishukuru Serikali kwa kuendelea kutuletea michango kwa wakati kwa ukamilifu wake na kwetu sisi tukisikia Mheshimiwa Rais ametangaza ajira mpya, kwetu sisi tunafurahi, tukisikia mishahara imeongezeka kwetu sisi ni habari njema, kwa hiyo zote ni jitihada Serikali inafanya kwa ajili ya watumishi wake na sisi kama mfuko tunanufaika na hayo.

"Eneo la pili ambalo nilipenda niliweke vizuri lifahamike ni hili la uwekezaji na uwekezaji wetu unafanywa kwa kusimamiwa na usimamizi wa fedha, Benki Kuu ndiye anayetusimamia sisi na kusema weka hapa, usiweke pale.

"Kwa hiyo kama mfuko tumekuwa tukielekezwa kuwekeza sehemu ambazo zinaendana na kuboresha suala zima la afya. Hatuwekezi sehemu ambazo haziendani na huduma za afya,"amesema Bw.Konga.

"Mathalani leo hii mfuko umewekeza kwa kujenga Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma, uwekezaji uliofanyika mpaka 2020, mambo yote yaliwekwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

"Eneo jingine ni MOI ukienda MOI ile ya zamani na mpya zile ni fedha kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, ukienda Muhimbili walivyosema wanaanza huduma za kuhamisha figo zile center zote mpaka vifaa ni fedha za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ukienda KCMC ukizungumza emergency yao department yao ya oxygen plant vyote ni Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

"Ukienda Bugando kuna jengo limejengwa na mfumo wa Taifa wa Bima ya afya, ukienda Mbeya Zonal Referral hospitali kuna private wing na mifano mingi mingi...ni kweli tunawekeza kwenye maeneo makubwa mawili eneo la kwanza miundombinu kwa kutoa mikopo.

"Lakini fedha hizo mwisho wa siku ni kuboresha huduma ambazo leo hii tunazipata unaweza ukafikirai leo hii tusingharamia Dodoma bila Benjamin Mkapa wote tungejaa kwenye Hospitali ya Mkoa au tungehitaji Serikali ichukue fedha zake ijenge ambazo zilikuwa ziende kwenye maeneo yake ya kipaumbele sasa ijenge hospitali kubwa ya kisasa kama hiyo, lakini mfuko ukifanya hivyo kwa makubaliano na serikali inatambua na fedha hizo zinarudishwa awamu kwa awamu.

"Eneo la pili tunalowekeza ni kwenye taasisi za fedha za Serikali, tunawekeza huko kulinda thamani ya fedha tulizonazo, nisema kule mwanzoni michango unayopokea leo thamani yake kesho ni tofauti na katika hali tuliyonayo sijui vita sijui ya wapi thamani ya fedha inashuka kwa hiyo lazima uweke fedha kugharamia matibabu siku za kesho.

"Jambo la tatu ambalo la kutolea ufafanuzi ni gharama zipo za aina mbili gharama za matibabu na gharama za utawala huduma za kiuendeshaji nimezungumza hapa gharama za matibabu zinaongezeka kila siku, kama mfuko tunahakikisha kwamba tunasimamia vizuri nini tunalipa kwenye nyenzo ya gaharama.

"Kwenye upande wa uendelezaji sheria imetuwekea asilimia 15 ya michango itumike kwenye uendeshaji wa mfuko ni shughuli zote zinazohusiana na kuhubiria huyo mwanachama habari za bima ya afya, kumsajili, kusimamia utoaji wa huduma, kukiwa na malalamiko tukaangalie hiyo hospitali kwa nini inakiuka makubaliano.

"Kuna mahali ilitajwa tumevuka tuko mbali sana nitoe taarifa tangu kuanzishwa kwa mfumo hatujawahi kufikia asilimia 15, tuko kwenye wastani wa asilimia 12 na tunafahamu tukizembea kwenye gharama za uendeshaji malengo ya mfuko yatarudi nyuma kwa hiyo tunatumia mbinu mbalimbali kuhakikisha kwamba gharama hizi zinaendana zisifike kwenye asilimia 15 kwa kuwa na kuna nmna mbalimbali ya kufanya hivi.

"Mfano leo hii tungehitaji kutembea nchi nzima kueleza haya tunayowaelezea (waandishi wa habari), lakini kwa kuwatumia ninyi wanahabari taarifa zote zitafika, lakini tungekuwa katika matumizi ambayo hayajadhibitiwa tungekuwa kila mahali tunachanja mbuga, kwenye eneo la uendeshaji tunakwenda vizuri.

"Eneo la nne ni kuhusu sekta binafsi pia inaonekana kana kwamba sekta binafsi hatuipi kipaumbele, lakini sekta binafsi tunaishirikisha sana wana chombo chao kinaitwa Association of Private Health Facilities in Tanzania (APHFTA) kwa wale ambao wana vituo binafsi, BAKWATA, mashirika ya dini kila kundi tunalishirikisha kwa wakati wake.

"Tunatambua mchango wao na kuwathamini sana ikiwemo kuwasajili na kuwatambua kama wadau vile vile zile fedha tunazozipa sekta binafsi, lakini tatu kwenye majadiliano tumekuwa tukishirikiana nao kwa karibu, hivyo tunapotaka kufanya maamuzi mathalani mwezi wa saba hapa Dar es Salaam tulikaa nao na kila kundi tunalishirikisha.

"Eneo jingine ambalo nimeona nilisemee ni hili la kujumisha makundi mbalimbali yote kwenye Mfuko wa Bima ya Afya na hapa nisemee kwenye sekta isiyo rasmi mtakumbuka kama nchi asilimia 100, asilimia 20 iko kwenye sekta rasmi ambayo mwisho wa siku unajua kuna mshahara mwisho wa mwezi, lakini asilimia 80 iko kwenye sekta isiyo rasmi achilia mbali ile ambayo Serikili inarasimisha kupitia masuala ya ushirika.

Isiyo rasmi

"Sasa ukiongelea sekta isiyo rasmi kama mfuko tulitaka tulitengenezee kila kundi utaratibu wake ndio maaana tulikuja na huduma ya watoto kwa maana ya Toto Afya Kadi, wanafunzi...Students Card. Wanahabari tukaanzisha utaratibu wenu, wakulima kupitia Ushirika Afya, kwa hiyo kila kundi tumeliwekea utaratibu wake na tukaanzisha vifurushi mwaka 2019 kwa wananchi ambao hawakujiunga sehemu yoyote, niwashukuru wanahabari tulifanya kazi nzuri sana kuwaelimisha na kuwahimiza kwenye uzinduzi na kuvielezea bado ni wachache.

"Tumekuwa na changamoto na hiyo ya vifurushi, lakini makundi mengine utaratibu umekwenda vizuri tu, kwa mfano wahariri kulikuwa na hoja siku za nyuma kuwa,hatujawatengenezea utaratibu, tumeshawatengenezea utaratibu ili wote wajiunge wote kwa pamoja sio tusubirie wawili wanaumwa tulete picha zao tuingie wote.

"Kwa mfano tukisema tuna Kikoba cha Wahariri, Wanafunzi, Wakulima sasa kikoba hiki cha kifurushi kimekuwa na changamoto zake kwa sababu hawaingii kwa umoja wao. Wahariri ni rahisi kuwabana mfano unaweza kufahamu wahariri ni wangapi tuko100, wanafunzi shule hii mko wangapi 500 wakiumwa 100, 400 wazima tunajua sasa hawa wanachangia pote shughuli zao za kila siku hatujaweza kuwabana. Wanaingia wachache kikoba chao hakijawa na nguvu sana kama ambavyo tulitarajia.

"Na ndiyo maana sasa mikakati ya makusudi inatatakiwa kuimarisha kikoba hiki cha kifurushi, sisi tunaona kundi hili waingie kwa lazima mfano huyu ana biashara hawezi kupata leseni mpaka awe na Bima ya Afya, kama ni mfanyabiashara mkubwa anachukua vitu China hawezi kupata passport bila kuwa na Bima ya Afya.

"Kama ni mtalii, hivyo hivyo kwa hiyo ndio tunafikiria kwa siku zijazo, lakini kama mfuko tunaendelea kujipanga kuona namna bora ya kuweza kuimarisha, kutokana na uchache wao kasi ya ukuaji wa huduma na manufaa nayo inakuwa ni ndogo, mathalani unakuta mtu analipia 192,000 kwa mwaka unakuta ana tatizo la fulani, tuseme labda ni figo unamsajili umpe na huduma ambayo matibabu yake ni zaidi ya shilingi 250,000 kwa session moja.

"Sasa kutokana na hilo limeanza kuleta malalamiko kwamba sisi watu wa namna hizi utaratibu huu hatupati moja, mbili, tatu.

Tujiunge wengi

"Suluhu yake ni watu wengi kujiunga zaidi kujiunga, nitumie fursa hii kuwaomba wanahabari mtusaidie kusambaza habari hizi kwa umma wa Watanzania uweze kufahamu kuwa, tukiwa wengi kwenye mfumo wa Bima ya Afya ndipo tunakuwa na amani, nchi nyingi za wenzetu zimeendelea vizuri sana kwenye sekta ya afya kwa sababu wananchi wengi wamejiunga kwenye sekta ya afya kwenye huduma za matibabu.

"Kwa sababu wengi zaidi wako kwenye mfumo wa bima ya afya, mfano Rwanda zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wote wako kwenye mfuko wa bima ya afya, ukizungumza nchi ya Marekani au Uingereza huwezi kuingia kama huna bima ya afya, kwa hiyo wengi wao kuingia zimeshushasha hadi gharama za matibabu.

"Nitoe rai tuendelee kuhimiza wananchi wajiunge kwenye Bima ya Afya ndio njia bora imethibitika kuwasaidia wananchi kupata huduma stahiki na endelevu za matibabu na kuimarisha mfumo mzima wa utoaji huduma za afya.

Malipo mtoa huduma

"Utaratibu wa malipo kwa Mtoa huduma, sheria inatutaka ndani ya siku 60 tuwe tumeshalipa baada ya mwisho wa mwezi kuisha mtoa huduma awe amewasilisha madai yake, ana siku 30 baada ya mwezi ule, mathalani ametoa huduma mwezi wa pili inampa siku 30 ya kuandaa bills zake halafu inatupa sisi siku 60 za kuchakata madai yake.

"Kwa nini tumepewa siku 60 ni kuhakikisha kama mfuko tunalipa fedha halali kwa huduma halali, sasa kuna mahali pengine tumefanya vizuri zaidi tumelipa zaidi zaidi ya siku 40 au siku 35, kuna mahali tunalipa zaidi ya siku 60 na mahali ambapo tunaona kuna viashiria vya madai ambayo si sahihi lazima tutumie muda mrefu kwa sababu hizi ni fedha za umma.

"Tukisema tu tuwe tunagawana kama njugu, kuna mahali tukifika tutashindwa kuendelea. Kuna baadhi ya madai ambayo yana walakini tunalazimka kwenda mpaka saiti na kuwatafuta wanachama ndio maana sasa hivi tumeweka utaratibu ukienda hospitali unapata meseji kadi yako inatumika, imetumia kiasi kadhaa hii yote ni kukushirikisha mwanachama wetu na wewe uone kwamba kweli nimetumia shilingi milioni 5,000,000?

"Na ujumbe huo unaambatana na namba, leo ukiona unaona piga namba hii ukitupigia sisi tunaanza kutarack, kwa hiyo ni kweli wakati mwingine tunalipa zaidi ya siku 60, lakini si lengo, kwa sababu tunahitaji watoa huduma nao wapate fedha kwa hiyo tumekuwa na mikakati yetu, mojawapo ni kuongeza watumishi mpaka sasa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya unawatumishi takribani 700 ikilinganisha na watumishi 200.

"Leo hii tuna vituo 9,000. Tunawachama milioni nne na laki nane. Tuna watumishi 700 Serikali ikija na bima ya afya kwa mfano watu twende tukatekeleze kwa sensa iliyopita tulikuwa wananchi takribani milioni 50 inamaana tutakuwa na Watumishi zaidi ya milioni tano, sijui itakuwa taasisi gani, itakuwa taasisi kubwa sana.

TEHAMA

"Kama mfuko tumewekeza sana kwenye TEHAMA (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano) na ndio maana sasa hivi kuna vituo vina uwezo wa kuwasilisha madai siku hiyo hiyo na sisi tangu amemaliza kuwasilisha madai yake tunajipa siku 14 hadi 20 tuwe tumelipa madai yake.

"Kuna vituo ambavyo vimekwishawekeza humo kwenye TEHAMA kama sisi tunakwenda sambamba na tunaweza kulipa kwa wakati na hilo ndilo eneo la kipaumbele la mfuko kwa sasa kwa mwaka huu tunaouelekea nitoe rai kwa watoa huduma kuingia kwenye mfumo huo ili tuweze kulipana fedha hizo kwa wakati, kituo kikiwa na fedha kitaweza kutoa huduma kwa wanachama na kuondoa malalamiko kwa wanachama.

"Kituo kikiwa hakina fedha hata dhana ya unyanyapaa inaanza kujitokeza, akimuona mwanachama wa NHIF anasema atamcheleweshea hela anampa kipaumbele mteja anayetoa fedha mfukoni.

"Tunawekeza sana kwenye TEHAMA nitoe rai kwa watoa huduma tuingie kwenye huu mfumo ili haya malalamiko tuyamalize tukiwa kwenye forum moja ya kuwasilisha madai kwa wakati, tukayashughulikia kwa wakati basi malalamiko hayo tutayamaliza.

"Na sisi tusingependa tufike mahali wanachama wetu wanacheleweshewa kupata huduma eti kwa sababu sisi tumechelewa kulipa kwa wakati na mikataba yetu na watoa huduma haitoi fursa hii.

"Mikataba yetu inawataka watoa huduma watoe huduma kwanza mwisho wa siku tukae na watoa huduma tukae chini kuona namna ya kuboresha, kwa hiyo kama mfuko tunayo mikakati ya wazi mbali na kuendelea kuongeza madaktari na kada mbalimbali mpaka sasa tuna vituo 150 vimeshajiunga na utaratibu huo ukienda tu hospitalini ukifika unapotoa kadi unaambiwa kwamba kadi yako inatumika na ukishaondoka tu siku hiyo unaambiwa umetumia kiasi gani kwa hiyo vituo hivyo vimekwishaingizwa kwenye TEHAMA.

"Tunaanza kulichakata deni lake mapema, ukifika mwisho wa mwezi anatoa invoice mfano anadai Bilioni 2 ndani ya siku 14 sisi tunaweza kulipa ukienda sehemu fulani ukakutana na hali kama hiyo jua vituo hivyo vimeunganishwa na TEHEMA.

"Hiyo imetuonesha ni kwa namna gani tumeweza kupunguza malalamiko kutoka kwa wanachama na unyanyapaa. Kwa yale ambayo tunachelewa kulipa huwa tunamwambia kabisa mtoa huduma kwamba hapo kuna haja ya kujiridhisha kwanza maana hizi ni fedha za umma.

"Katika utaratibu wetu tuna namna tano ya kujiridhisha kabla hatujalipa kwa hiyo hata kama tunalipa tunaweza kurudi tunaangalia je? Tumelipa fedha halali.

Kujiridhisha lazima

"Ni eneo ambalo tunapambana nalo sana ukiangalia siku za nyuma ilikuwa inatuchukua hadi siku zaidi ya 100,lakini sasa hivi tumeimprove ukiangalia wastani wetu sasa hivi ni siku 45 mpaka 50 na lengo zile ambazo zimeingia kwenye mfumo ni siku 14 na zile ambazo haziko kwenye mfumo tuwe tumetumia siku 30 mpaka 35 tuwe tumelipa hayo madai,"amesema Bw.Konga.

"Tunafanya hivyo kwa sababu, kwenye msafara wa mamba kenge hawakosekani, kwenye vituo 9,000 tulivyonavyo kuna baadhi wakati mwingine vinaingia kwenye masuala ya udanganyifu tukishabaini kuwa udanganyifu niseme wazi tu hatua huwa ni kali sana.

"Moja ni kurejesha fedha ambazo umelipwa kwa udanganyifu, pili kukupa onyo na ukirudia ni kusitisha mkataba na nyie mtakuwa mmeona mwezi uliopita vituo kama 10 tulivitoa kwenye utaratibu huo na sasa hivi tutakwenda tena.
"Tunaona ni wazi kituo ambacho kinakuwa na wizi ni kituo ambacho kinahatarisha uendelevu wa mfuko na pia afya ya wanachama wa mfuko na Watanzania kwa ujumla,''amesema Bw.Konga.

"Sisi kama mfuko jukumu letu ni kuhakikisha tumelipia huduma halali zilizotolewa kulingana na miongozo iliyopo tukimaliza hapo, sisi lazima tuzichukue fedha za umma tuzirudishe, lakini hilo zoezi haliishii hapo tunakwenda wizarani tunaiambia wizara vituo hivi tumebaini vinatoa huduma ambazo haziendani.

"Wizara itafanya Clinical Audit kujiridhisha huduma zinazotolewa, itaangalia maeneo makubwa mawili eneo la kwanza wataalamu waliopo kama wamekwenda kinyume cha taratibu, pili itakwenda kwenye usajili je? Kituo hiki kina haja ya kuendelea kutoa huduma wao wana maamuzi, tatu kumbuka hizi ni fedha za umma vipo vyombo ambavyo vitachukua hatua, kwa maana ya vyombo vya serikali kwa hiyo ni zoezi ambalo lazima lisimamiwe vyema. duniani kote mifuko yote ya afya ya bima imekumbwa sana na changamoto na sisi hatuko salama.

NHIF ni wakali

"Ndio maana na sisi ni wakali sana, tukikuta kituo kinafanya fraud kwa kweli hatukifumbii macho na katika hili niishukuru sana wizara na Serikali tumekuwa bega kwa bega na mfumo kuhakikisha kwamba wale wote wanaumiza mfuko kwenye vitendo hivi wanawajibishwa.

"Na nitoe rai sasa kwa watoa huduma wazingatie matakwa ya mkataba tuzingatie miongozo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, ameshasema kwamba afya ni huduma na sio biashara kama mtu anaona kwenye huduma hakumlipi kuna biashara nyingine.

"Wale wachache wanaotaka kujinufaisha ndio wale ambao tunakutana nao kwenye mikwaruzano, huko sasa wanaanza kusema bima wametuonea, wamefanya nini? Ipo mifumo ya wazi ya kushughulikia kama wanaona tunawaonea waje tukae nao tunaweza kuwaeleza utaratibu mzina tuliotumia.

"Amekwenda mbali Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya afya anakwenda kuimarisha chombo cha usuluhishi pale ambapo itaonekana bima tumemuonea mtoa huduma, anakwenda huko na sisi akituonea tunashitaki kule tunaamini malalamiko hayo yatakwisha.

"Hicho chombo kipo mbioni kuanza majukumu yake sisi uchunguzi tunaufanya hata baada ya miaka mitatu je, tumelipa vizuri ndio maana walisema hela ya umma ukiila lazima uitapike.

NHIF yashukuru

"Mwaka 2016 tulikuja na mipango yetu ambayo tuliweza kuitengeneza na tuliweza kupitia taasisi nyingi za umma na binafsi na mpaka leo taasisi za umma tunazo na taasisi nyingi za binafsi tunazo kutokana na huduma bora tunazotoa.

"Niwashukuru sana taasisi zote za serikali na binafsi kuendelea kuwa pamoja na sisi na niseme tu kama mfuko tutaendelea kutumia utaalamu wetu wote kuhakikisha wanaridhika na huduma tunazozitoa, wanaendelea kufanya kazi na sisi ili mwisho wa siku wawe na uhakika wa matibabu wanayoyapata waweze kushiriki katika ujenzi wa nchi yetu,"amesema Bw.Konga.

Umuhimu wa maboresho

Bw.Konga anasema, maboresho na udhibiti wowote unaofanywa na mfuko huo ni kwa nia njema ya kumlinda na sio kumwadhibu mwanachama wake.

Pia amesema kuwa, mfuko una wajibu wa kuhakikisha unalinda uhai wake, ubora wa huduma anazopata mwanachama ili kuepukana na matatizo yanayoweza kujitokeza kutokana na kutolewa kwa huduma kiholela.

"Control tunazoziweka hazina maana ya kumuumiza mwanachama wetu, kama Mfuko tunao wajibu wa kulinda na kuhakikisha ubora wa huduma anazopata mwanachama wetu kulingana ni miongozo ya tiba iliyipo, mfano dawa zikitumika vibaya ni sumu hivyo udhibiti tunaoufanya ni kwa maslahi makubwa ya mwanachama wetu," amesema Bw. Konga.

Ametolea mfano wa udhibiti katika baadhi ya vipimo na akaweka wazi kuwa katika eneo hilo takwimu zilionesha namna vipimo vilivyokuwa vikitumika vibaya kabla ya kuweka udhibiti katika mifumo.

"Nitoe mfano wa eneo moja tu la kipimo cha MRI kabla ya kuweka udhibiti vipimo vilifanyika kwa idadi kubwa na baada ya kuweka udhibiti wa mifumo kulingana na miongozo ha tiba vilipungua kutoka 800 hadi 400 kwa mwezi," amesema Bw.Konga.

Kutokana na hilo niweke wazi kuwa Mfuko utafanya maboresho yake kwa kuzingatia uhalisia na miongozo ya Afya iliyopo nchini.

Gharama za matibabu

Akizungumzia suala la gharama za matibabu, Bw. Konga amesema kuwa mfuko unao wajibu wa kuhakikisha unaweka gharama zake kwa kuzingatia hali halisi ili kuepuka kusababisha mfumuko wa gharama katika eneo la matibabu na kuleta changamoto kwa wananchi.

"Zipo huduma ambazo awali hapa nchini hazikupatikana kwa wingi na gharama zake zilikuwa juu sana lakini kwa sasa zipo kwa wingi na gharama kwenye soko imeshuka hivyo ni muhimu kufanya mabadiliko hayo, huduma hizo ni pamoja na za kusafisha damu, dawa za kansa na huduma nyingi za kitalaam," amesema Bw. Konga.

Ili kwenda na uhalisia wa soko, alisema kuwa Sheria inautaka Mfuko kutoa taarifa kwa Watoa huduma wenye mkataba na NHIF za mabadiliko ya bei za huduma za matibabu kwa muda wa siku 90 na tayari Mfuko umeshatoa taarifa hiyo na katika kipindi hicho hadi kufikia Novemba Mosi mwaka huu Mfuko utakutana na kujadili na wadau wake mabadiliko hayo kabla ya kuanza kuyatekeleza.

Alitumia nafasi hiyo pia kuwahakikishia wanachama kuwa Mfuko iko imara na una fedha za kutosha kuwahudumia na mkakati uliopo sasa ni wa kufikia wananchi wengi zaidi ili kusaidia kuuimarisha zaidi kwa kuwa wingi wa wanachama huwezesha Mfuko kuongeza wigo wa huduma kwa wanachama wake.

Sayansi ya mfuko

"Mfuko unaendeshwa na Sayansi, hii inafanyika kisheria kila baada ya miaka mitano, mara ya mwisho tulikuwa nayo mwaka 2019 na sasa hivi mwezi huu mwishoni tunapokea taarifa ya evaluation (tathimni) mpaka 2022 kwa hiyo sayansi yake inaonesha bado mfuko ni imara.

"Mfuko utakufa...baada ya miaka miwili au mitano kuna kuwa na assumption, mfano endapo Serikali haitachangia lakini moja kwa moja tunaona jitihada za Serikali kwa zaidi ya miaka saba haijawahi kuwa na deni, inachangia kwa wakati.

"Lazima niseme hili, mfuko una sayansi yake ya kutumia hiyo hesabu na sayansi yake inagawanyika na tarehe 30 mwezi huu wa Agosti nitarudi kuwaambia kwa miaka minne wanachama thamani halisi ya mfuko wao na hata CAG anakagua na kuona kweli mfuko umeenda na anashauri, kwa hiyo niondoe hiyo taharuki, mwingine anaweza akasema kwamba usijiunge na NHIF leo itakufa, NHIF bado ina fedha za kutosha kuwahudumia wanachama wake.

"Na sisi jukumu letu ni kuhakikisha wananchi walio wengi wanajiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, kwa hiyo mikakati ya Serikali inazidi kuimarisha uhai na maendeleo ya mfuko. Mfuko uko chini ya Waziri wa Afya inaonekana Kama kama kwamba kila tunapoamka tuna jambo la kuamua, hapana. Katika kila tunachokifanya tunahakisha kinapata baraka na idhini za wizara husika.

"Kumekuwa na uhitaji wa kuwa na mdhibiti wa Bima za Afya nchini kwa hiyo Serikali inaangalia namna bora ya kuwa na mdhibiti atakayesimamia hili na hili ni kilio cha watoa huduma, lakini na sisi tunatamani,"amefafanua kwa kiba Bw.Konga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news