KMC FC yaendelea kujinoa

NA DIRAMAKINI

BAADA ya kurejea jijini Dar es Salaam, kikosi cha KMC FC kimendelea na maandalizi ya kujiweka sawa katika michezo ya Ligi Kuu ya NBC Soka Tanzania Bara itakayoendelea Septemba 7, mwaka huu.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Agosti 24, 2022 na Afisa Habari na Mahusiano wa KMC FC,Christina Mwagala.

KMC FC ambayo ilikuwa jijini Arusha kwenye michezo miwili ya ugenini, ilirejea siku ya Jumatatu na kutoa mapumziko ya siku moja kwa wachezaji ambapo jana Agosti 23 jioni waliingia kambini na kuanza kwa programu ya mazoezi maalum ya viungo na leo asubuhi kuendelea na mazoezi ya kawaida ya uwanjani.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni chini ya kocha Mkuu Thierry Hitimana katika kipindi hiki cha mapumziko kitakuwa na programu mbalimbali ikiwemo kucheza mechi za kirafiki ambapo kesho Agosti 25 itakuwa ugenini dhidi ya As Arta Solar 7 kutoka nchini Djibout mchezo utakaopigwa katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Mbali na mchezo huo, KMC FC pia itakuwa na mechi nyingine za kirafiki kulingana na mipango ya Kocha Mkuu Hitimana ikiwa ni katika mpango wa kufanya maboresho kutokana na kile alichokiona katika michezo miwili ya awali ya Ligi kuu ya NBC ambayo ni dhidi ya Polisi Tanzania pamoja na Coast Union iliyopigwa katika uwanja wa Shekh Amri Abeid.

“Tumetoka kwenye mechi ngumu za ugenini, nakupata matokeo ambayo hayakuwa rafiki sana kama ambavyo malengo ya timu ilikuwa imejiwekea ya kupata alama sita, lakini tukapata alama moja na magoli mawili, wachezaji wetu walicheza vizuri hilo ni jambo kubwa.

"Kwa kipindi hiki ambacho tupo kwenye mapumziko ya kupisha michuano ya Kombe la CHAN dhidi ya Uganda, tunahitaji mechi nyingi za kirafiki kadiri ambavyo tutazipata, na tayari tumeshapata mechi moja ambayo tutacheza kesho lengo ni kufanya maboresho ambayo yataiwezesha Timu kufanya vizuri zaidi katika michezo inayokuja,"ameeleza.

KMC FC imecheza mechi mbili za Ligi Kuu ambazo ni dhidi ya Coast Union uliomalizika kwa kupoteza na mwingine ni Polisi Tanzania uliomalizika kwa sare ya magoli mawili kwa mawili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news