Maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi yapamba moto

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imesema maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi yamefika zaidi ya asilimia 95 hivyo ni vyema kuendelea kushirikiana kwa pamoja kwa kuzingatia muda uliobaki ili kulifikia lengo lililopo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene katika Mkutano Maalum wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa alipokutana na sekta binafsi kwa lengo la kutambua mchango wao katika kuelekea siku hiyo ikiwemo ya rasilimali fedha, huduma na vifaa kwa ajili ya zoezi la Sensa ya watu na makazi ya Mwaka 2022.
Alisema kuwa, Serikali inatambua mchango wa sekta binafsi hivyo ni vyema kwa kila mdau kushirikia katika zoezi hili kwa kadri awezavyo kwa kuchangia rasilimali fedha, huduma na vifaa vitakavyosaidia kufanikisha zoezi la sensa.

“Karibu kila mdau ameshiriki katika maandalizi ya sensa kupitia taasisi ya sekta binafsi (TPSF) na tumekutana hapa ili kuonesha mshikamano wetu na kutambua michango yenu ninawapongeza sana," alisema Simbachawene.
Naye katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu amesema serikali imeshirikiana sekta binafsi katika maandalizi ya kuelekea siku ya sensa kwa namna mbalimbali ikiwemo, kugharamia matangazo yanayotoka kwenye vyombo vya habari.

“Kampuni za simu zilisaidia kutoa ujumbe mfupi wa kuhamasisha wananchi na kuelimisha wananchi juu ya zoezi la sensa ya watu na makazi na baadhi kuahidi kuchangia fedha na vifaa mbalimbali ili kufanikisha zoezi la sensa ya watu na makazi,”alisisitiza Dkt.Jingu.
Naye Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Mhe. Anne Makinda ameshukuru sekta binfasi kwa mchango wao katika kuwezesha maandalizi ya kuelekea siku ya sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika tarehe 23 Agosti, 2022.
“Tumejipanga kusimamia matumizi yote tunayopewa na kuhakikisha tunapata matunda tunayotegemea,”amesema Mhe.Makinda.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news