Mashabiki Simba SC, Yanga SC watambiana bao la Sakho kutumika Agosti 13 kwa Mkapa

NA DIRAMAKINI

MASHABIKI wa Simba SC ya jijini Dar es Salaam wamesema kuwa, wameteta na mshambuliaji wa klabu hiyo raia wa Senegal, Peppe Ousmane Sakho ili bao kama lile ambalo lilitangazwa kuwa bora barani Afrika dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast aweze kuwapiga Yanga SC katika Ngao ya Jamii siku ya Agosti 13,2022.

Wameyasema hayo kwa nyakati tofauti nje ya dimba la Benjamin Mkapa siku ya Agosti 8, 2022 wakati wakizungumza na DIRAMAKINI kuelezea mikakati waliyonayo kuhakikisha Ngao ya Jamii wanaibeba kibabe.

"Sisi tumeshamwelekeza Papa Sakho afanye vile vile kwenye Ngao ya Jamii kama alivyofanya wakati wa Michuano ya Kombe la Shirikisho Hatua ya Makundi msimu wa 2021/2022 dhidi ya ASEC Mimosas na sisi wababe wa Kimataifa, Simba SC na amesema atafanya hivyo hivyo, kwa hiyo Yanga SC hawana chao.

"Huu msimu tumejipanga vema, ndiyo maana hata usajili wetu tumekwenda hadi Ulaya, hakuna aliyethubutu kuvuka mipaka mingi kwenda kuvuta vifaa vikali, kwa hiyo wajue tu kwamba, sisi huu ni mwaka na msimu wetu. Tupo vizuri,"anasema Rajabu Mohamed ambaye ni shabiki wa Simba SC jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wao, mashabiki wa Yanga wamesema kuwa, usajili wa Simba SC ni wakusikitisha kwa kuwa, wameleta Wazungu 'pori' katika klabu.

"Wanaleta Wazungu 'pori' nchini wanasema eti wameleta vifaa, huo ni uhuni, tusubiri msimu uanze kabla ya mambo kukolea sijui wataanza kumfukuza nani? Inawezekana yule kocha amekuja na ndugu yake ili amsaidie kubeba mabegi, sisi hatuna mengi. Muda utasema, na Yanga tupo vizuri, mwaka na msimu wa furaha unaendelea. Kiukweli Simba SC wamepigwa kupitia Mzungu au wazungu wao,"ameeleza Julius Julius ambaye ni shabiki wa Yanga SC jijini Dar es Salaam.

Pia, Nasra Khamis amewataka mashabiki wenzake wa Yanga SC kutulia, kwani Agosti 13, 2022 kuna watu ambao wanakwenda kulia. Huku Mwajuma J akisema kuwa, mashabiki wa Simba SC hawana presha, kwa sababu tamasha lao limeonesha nuru mbeleni.

Taji la Ngao ya Jamii 2021 lilitwaliwa na Yanga SC baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba SC katika mchezo uliopigwa kwenye dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Bao pekee la Yanga SC lilifungwa na mshambuliaji, Fiston Mayele dakika 11, baada ya kupokea asisti safi ya Winga, Farid Mussa Maliki aliyeichambua ngome ya Simba SC na kufanya mchezo huo kuisha ndani ya dakika 90 pekee.

Katika mtanange huo Yanga SC walionekana bora zaidi katika eneo la kiungo cha ukabaji kilichokuwa chini ya Yannick Bangala na Khalid Aucho wakiwalinda mabeki wa kati, Bakari Nondo Mwamnyeto na Dickson Job.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news