Silinde:Serikali inatambua changamoto za Shule ya Msingi Kiboriani, ipo katika hatua za utatuzi

NA OR-TAMISEMI

NAIBU Waziri anayeshughulikia Elimu Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI),Mhe. David Silinde amesema, Serikali katika mwaka huu wa fedha inapeleka vyumba vinne vya madarasa, matundu ya vyoo na nyumba moja ya walimu (3 in 1) kwenye Shule ya Msingi Kiboriani iliyopo Kata ya Mpwapwa wilayani Mpwapwa Mkoa wa Dodoma.
Amesema shule hiyo ilikuwa miongoni mwa vipaumbele vyake katika mwaka huu wa fedha ulioanza Julai Mosi, mwaka huu na taratibu za kutekeleza mipango hiyo zilikuwa katika hatua za mwisho.

Mhe.Silinde ametoa kauli hiyo leo Agosti 9, 2022 wakati wa ziara yake wilayani humo ya kutembelea shule hiyo na kukagua miundombinu na mazingira ya shule hiyo akiambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama huku akitoa wito kwa wanahabari kuendelea kutumia vema kalamu zao, kwa kuwa tayari OR-TAMISEMI kupitia watendaji wake wametoa nafasi kwa kila mwenye hitaji la ufafanuzi kupata taarifa sahihi.

Amegusia hilo baada ya moja ya chombo cha habari licha ya kupewa taarifa sahihi na mipango iliyopo kuhusu shule hiyo, kwenda kuripoti taarifa ambazo hazijaijumuisha wizara, jambo ambalo linaweza kuleta taharuki katika jamii wakati tayari maelezo ya kutosha kuhusu shule hiyo yalishatolewa kwa mwandishi husika.

"Nimefika shuleni hapa nimebaini changamoto kadha wa kadha kama uhaba wa vyumba vya madarasa, uchakavu wa miundombinu ya vyoo, na uhaba pamoja na uchakavu wa nyumba za walimu. Shule hii ya Msingi ya Kiboriani ipo katika mipango yetu tangu awali na katika mwaka huu wa fedha tumeshajipanga kufanya ujenzi na maboresho makubwa.

“Nisema kama Serikali tuna mipango mbalimbali ya kutatua changamoto kama hizi nchi nzima kupitia Mradi wa BOOST ambao una lengo la kuimarisha Elimumsingi na una fedha takribani shilingi trilioni moja ambao utajenga madarasa ya shule za msingi 9,705 na kukarabati shule za msingi kongwe kwa mwaka wa fedha 2022/23,"amesema Mheshimiwa Silinde.
Pia amesema, kupitia mradi huo changamoto kama hizo katika shule za msingi zitakuwa historia na bado wanaendelea kutafuta vyanzo mbalimbali vitakavyosaidia kumaliza kabisa changamoto hizo.

"Halikadhalika tuna mradi wa kuboresha Elimu ya Sekondari (Sequip) ambao unajenga shule za sekondari 1,000 na shule za sayansi za wasichana kwenye mikoa yote 26 nchini na kwa mwaka huu wa fedha tumeshaanza kujenga shule 224 za sekondari na shule za wasichana kwenye mikoa 10 nchini.

"Lakini tuliona tusiwekeze kwenye madarasa tu, bali pia tuboreshe mazingira ya walimu, hivyo kwenye Bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23 tumetenga jumla ya shilingi Bilioni 55 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu 809 zenye uwezo wa kuchukua kaya 1,916.

"Hivyo sio kwamba Serikali hatuoni hizi changamoto au hatuzifanyii kazi tunajitahidi kuzitatua kadri rasilimali zinavyopatikana kwa sababu tuna shule za msingi zaidi ya 17,000 na shule za sekondari zaidi ya 4,000 na kati ya hizo nyingi ni za zamani, hivyo zinahitaji ukarabati wa mara kwa mara, lakini bado tunahitajika kuendelea kujenga miundombinu mipya kwa kadri ya mahitaji.

"Kutokana na changamoto niliyoiona hapa tutaleta madarasa yote yenye upungufu ambayo ni manne, matundu ya vyoo sita pamoja na nyumba ya mwalimu standard yenye uwezo wa kubeba familia tatu yaani '3 in 1',"amesisitiza Mhe. Silinde.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe.Rosemary Sinyamule amesema, ataendelea kuhamasisha jamii ili iweze kuchangia juhudi za Serikali katika kuboresha miundombinu ya shule.

"Kazi kubwa inafanywa na Serikali, lakini pia jamii ina wajibu wa kushiriki na kuunga mkono jitihada hizo, hivyo leo hii nafanya kikao na wananchi wa Kiboriani ili tuweze kuhamasishana kuendelea kuboresha shule hii ambayo ni muhimu kwa watoto wa kijiji hiki,"amesema RC huyo.

Akisoma taarifa ya shule hiyo, Kaimu Afisa Elimumsingi wa Halmashauri ya Mpwapwa, Bi. Agness Nkacha amesema kuwa, Shule ya Msingi Kiboriani ni miongoni mwa shule 122 za halmashauri hiyo na ilianza mwaka 1979 na mpaka sasa ina wanafunzi 428 na walimu sita wote wa kiume.

Shule ya Msingi Kiboriana iko umbali wa kilomita 20 kutoka makao makuu ya wilaya na ina upungufu wa madarasa manne, nyumba za walimu na matundu ya vyoo sita.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news