Mhandisi Kasekenya:Tumieni uwepo wa barabara za lami kuwekeza

NA MWANDISHI WETU

NAIBU Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amezungumzia umuhimu wa watanzania kutumia fursa zinazotokana na ujenzi wa miundombinu hususan barabara za lami kuwekeza katika nyanja za kilimo, mifugo, uvuvi, na utalii ili kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.
Muonekano wa barabara ya Nyamuswa-Bulamba KM 56.4 mkoani Mara ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami unaendelea.

Akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara Naibu Waziri Kasekenya amesema Serikali inatumia fedha nyingi katika ujenzi wa barabara za lami hivyo ni wajibu wa wananchi kunufaika kijamii na kiuchumi kutokana na uwekezaji unaofanywa na Serikali katika barabara hizo.

“Zitunzeni barabara hizi za lami kwa kuhakikisha mnazitumia kuchochea maendeleo na kukuza uchumi wenu”, amesisitiza Mhandisi Kasekenya.
Mhandisi Paul Margwe wa Wakala wa Barabara Tanzania TANROADS mkoa wa Mara akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Nyamuswa-Bulamba KM 56.4 mkoani Mara.

Amebainisha kuwa Serikali itaendelea kujenga barabara za lami kimkakati ili kuwapunguzia wananchi gharama za kusafiri umbali mrefu kwa kujenga njia mbadala na fupi akitolea mfano wa barabara ya Mwigumbi-Maswa-Bariadi ambayo ujenzi wake katika sehemu zinazofanyiwa maboresho utakamilika Septemba mwaka huu.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya akifafanua jambo kwa wakazi wa mji wa Mugumu wilayani Serengeti alipokagua barabara ya Mogabiri-Nyamongo-Tarime inayotarajiwa kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami hivi karibuni.

Kuhusu barabara ya Nyamuswa-Bulamba KM 56,4 ambayo ni sehemu ya barabara ya Nyamuswa-Bunda-Kisorya-Nansio KM 121.9 mkoani Mara Naibu Waziri Kasekenya ameelezea kuridhishwa na kasi ya ujenzi wake na kumtaka mkandarasi anayejenga barabara hiyo China Civil Engineering Construction Cooperation (CCECC), kuongeza kasi ya ujenzi na kuhakikisha anajenga vivuko katika maeneo ya makazi na yenye huduma za jamii ili kulinda kingo za barabara hiyo.

Amebainisha kuwa nia ya Serikali ni kuunganisha barabara za mkoa wa Mara na Arusha ili kukuza utalii wa kisasa kufuatia ongezeko kubwa la watalii katika hifadhi za Serengeti na Ngorongoro.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya akisisitiza jambo kwa Mhandisi Paul Margwe wa Wakala wa Barabara Tanzania TANROADS mkoa wa Mara wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Nyamuswa-Bulamba KM 56.4.

Naye Mbunge wa Bunda, Mhe. Boniface Getere ameipongeza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa namna inavyofuatilia miradi ya ujenzi wa barabara mkoani Mara na kumhakikishia Naibu Waziri elimu ya kuilinda na kuitumia miundombinu hiyo itatolewa ili kuiwezesha kudumu kwa muda mrefu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news