Simba SC yaanza Ligi kileleni, Coastal Union, Mbeya City na Azam FC patamu

NA GODFREY NNKO

WEKUNDI wa Msimbazi, Simba SC wameanza vyema safari ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara baada ya ushindi wa 3-0 dhidi ya Geita Gold ambao unawafanya kuwa kileleni.
Ni kupitia mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya NBC uliopigwa katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam tarehe 17 Agosti,2022.

Simba SC walianza mchezo huo kwa kasi wakiliandama lango la Geita Gold dakika 15 za mwanzo, lakini walikosa umakini katika eneo la mwisho.

Winga Augustine Okrah alitupatia bao la kwanza dakika ya 37 kwa mpira wa adhabu uliotinga wavuni moja kwa moja kwa mguu baada ya kiungo Clatous Chama kufanyiwa madhambi nje ya 18.

Moses Phiri alitupatia bao la pili dakika ya 61 baada ya kupokea pasi safi kutoka Clatous Chama akiwa ndani ya 18.
Chama alitupatia bao la tatu kwa mkwaju wa penati dakika ya 81 baada ya Okrah kufanyiwa madhambi ndani ya 18.

Kocha Zoran Maki aliwatoa Jonas Mkude, Phiri, Peter Banda, Pape Sakho na Chama na kuwaingiza Okrah, Dejan Georgejivic, Mzamiru Yassin, Kibu Denis na Nelson Okwa.

Huu unaweza kuutafsri kuwa, ni ushindi mnono ambao unawapa faraja ikiwa ni siku chache baada ya kuambulia kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa watani zao Yanga SC katika mtanange wa Ngao ya Jamii.

Aidha, Kocha Mkuu Zoran Maki alimpanga Moses Phiri kuongoza mashambulizi katika mchezo huo ikiwa mechi mbili zilizopita dhidi ya St. George kwa maana ya Simba Day na Yanga SC katika Ngao ya Jamii alimpanga Habib Kyombo kuongoza mashambulizi.

Jicho la mwalimu lilimouona Phiri atafaa zaidi huku akipata msaada wa karibu kutoka kwa viungo washambuliaji Clatous Chama, Pape Sakho na Peter Banda.

Mlinda mlango namba moja, Aishi Manula alirejea kwenye lango baada ya kukosa mechi mbili zilizopita kutokana na kuwa majeruhi.
Kikosi cha Wekundu hao kiliundwa na Aishi Manula (28), Shomari Kapombe (12), Mohamed Hussein (15), Henock Inonga (29), Mohamed Ouattara (33), Jonas Mkude (20), Pape Sakho (10), Sadio Kanoute (13), Moses Phiri (25), Clatous Chama (17), Peter Banda (11).

Wachezaji wa Akiba

Beno Kakolanya (30), Israel Patrick (5), Joash Onyango (16), Mzamiru Yassin (19), Nelson Okwa (8), Augustine Okrah (27), Dejan Georgijevic (7), Habib Kyombo (32), Kibu Denis (38).

Azam FC vs Kagera Sugar

Wakati huo huo, wenyeji Azam FC wametoka nyuma na kushinda 2-1 dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo wa kuhitimisha Raundi ya Kwanza ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.

Ni kupitia mtanange uliopigwa usiku wa Agosti 17,2022 katika dimba la Azam Complex lililopo Kata ya Chamazi katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Mshambuliaji Prince Dube dakika ya 17 na chipukizi Tepsie Evans dakika ya 58 ndiyo waliowezesha Azam FC kung'ara huku Kagera Sugar ambao walitangulia, bao lao lilifungwa dakika ya 10 na Anuary Jabir.

Mbeya City vs Dodoma Jiji

Katika hatua nyingine,Mbeya City FC imeanza vyema Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara baada ya ushindi wa 3-1 dhidi ya wenyeji, Dodoma Jiji FC.

Ni kupitia mtanange uliopigwa Agosti 17, 2022 katika dimba la Liti lililopo mkoani Singida ambapo Rashid Chambo aliyejifunga dakika ya 26, Sixtus Sabilo dakika ya 42 na Eliud Ambikile dakika ya 63 walifanikisha ushindi wa Mbeya City huku Paul Peter dakika ya 18 akiwafuta machozi Dodoma Jiji.

Coastal Union vs KMC

Mbali na hayo,penalti ya Mbaraka Hamza dakika ya 37 imeiwezesha Coastal Union kukomba alama zote tatu mbele ya timu ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni (KMC FC).

Ni kupitia mtanange wa Agosti 17, 2022 ambao ulipigwa katika dimba la Sheikh Amri Abeid uliopo jijini Arusha ambapo hadi dakika 90 zinafikia tamati ubao ulisoma KMC sufuri huku Coastal ukisoma bao moja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news