Miradi ya TEA yaneemesha taasisi za elimu nchini, Mkurugenzi Mkuu ataja mikakati ijayo

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Elimu Tanzania (TEA) imesema kuwa, katika mwaka huu wa fedha wa 2022/2023 imepanga kutumia shilingi Bilioni 8.9 kwa ajili ya kufadhili miradi ya kuboresha miundombinu ya elimu nchini.

Fedha hizo zitatumika kufadhili miradi 96 katika shule 96 za msingi na sekondari katika maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara pamoja na taasisi mbili za elimu ya juu kwa upande wa Zanzibar.
Hayo yamesemwa leo Agosti 4, 2022 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Bi.Bahati Geuzye wakati akielezea majukumu ya mamlaka hiyo kwa waandishi wa habari kupitia mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO jijini Dar es Salaam.

Bi.Geuzye amesema, miradi itakayofadhiliwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa 99, matundu ya vyoo 792, maabara 10 za masomo ya sayansi kwa ajili ya shule tano za sekondari, nyumba za walimu 52 na mabweni 10.

Pia amefafanua kuwa,miradi mingine itakayotekelezwa ni ujenzi wa miundombinu ya wanafunzi wenye mahitaji maalum inayojumuisha madarasa 10, matundu ya vyoo 40 pamoja na mabweni mawili katika shule sita za msingi na moja ya sekondari.

Wakati huo huo, Bi.Geuzye amesema, katika mwaka huu wa fedha Mfuko wa Elimu wa Taifa utaboresha miundombinu na kuwezesha ununuzi wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia kwa taasisi mbili za elimu ya juu zilizopo Zanzibar.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa TEA,miradi hiyo imepangwa kutumia shilingi milioni 500 katika utekelezaji wake.

Miradi mingi

Aidha, Bi.Geuzye amesema, zaidi ya miradi 3,314 yenye thamani ya shilingi Bilioni 212.6 imetekelezwa nchini na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) tangu kuanzishwa kwake hapa nchini.

Wanufaika wa miradi hiyo amesema, ni taasisi za elimu zikiwemo shule za awali, shule za msingi, shule za sekondari, vyuo vya ualimu, vyuo vya ufundi na vyuo vikuu.

Amesema,TEA ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge ya Mfuko wa Elimu Na. 8 ya mwaka 2001 chini ya kifungu 5 (1) pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2013 kwa lengo la kuratibu uendeshaji wa Mfuko wa Elimu.

Bi.Geuzye amesema, mfuko huo pia ulianzishwa kwa Sheria hiyo Na.8 ya mwaka 2001, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuongeza upatikanaji wa elimu bora na kwa usawa nchini.

"Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), hii ni taasisi ya umma inayofanya kazi chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,"amebainisha huku akifafanua kuwa, Mfuko wa Elimu unapata fedha kutokana na vyanzo vya kisheria vilivyoainishwa katika Sheria ya Mfuko wa Elimu Na. 8 ya mwaka 2001.

Vyanzo hivyo ni pamoja na tengeo la kibajeti kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. "Mfuko pia unapokea michango ya fedha na vifaa kutoka kwa wadau wa elimu,"amesema.

Miradi ya pamoja

Bi.Geuzye amesema, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, TEA ilipokea michango na kutekeleza miradi ya pamoja na mashirika ya umma na yasiyo ya kiserikali yenye thamani ya shilingi milioni 556.3.

Amefafanua kuwa, mashirika hayo yaliyoshirikiana na TEA ni pamoja na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Taasisi ya Flaviana Matata, BRAC- Maendeleo Tanzania, Taasisi ya Asilia Giving, Taasisi ya SAMAKIBA na Kampuni ya Dash Industries.

Pia amesema kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa unaoratibiwa na mamlaka hiyo, katika mwaka wa fedha 2021/2022, shilingi bilioni 8.6 ziligharimia ufadhili wa miradi 160 ya kuboresha miundombinu ya elimu katika shule 151 nchini.

Amesema, miradi hiyo ilijumuisha ujenzi wa madarasa 210 katika shule 65 (shule za msingi 53 na sekondari 22), maabara nne za sayansi katika shule mbili za sekondari, matundu ya vyoo 1920 katika shule 80 (za msingi 58 na sekondari 22).

Mambo mengine amesema, ni vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika shule tisa za wanafunzi wenye mahitaji maalum kati ya hizo shule za msingi zikiwa nane na moja ya sekondari na ujenzi wa ofisi mbili za walimu katika shule mbili za sekondari.

Ujuzi

Amesema kuwa, katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa miradi ya kuratibu Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (Skills Development Fund-SDF), mafunzo yalijikita katika sekta ya Kilimo na Kilimo-Biashara na shilingi bilioni 3.1 zilitumika kufadhili taasisi 15 za kutoa mafunzo ya ujuzi.

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema kuwa,kupitia mfuko huo kiasi cha Shilingi Milioni 385.8 kimetolewa kunufaisha vijana 1,018 katika programu ya utarajari (Internship Program) katika sekta za TEHAMA, utalii na huduma za ukarimu, nishati, ujenzi na uchukuzi.

Amesema, Mfuko wa SDF pia unafadhili mafunzo ya ujuzi kwa wanufaika 4,000 kutoka kaya maskini na makundi maalum hadi ifikapo Desemba 2022 lengo ni kuwezesha vijana wanaotoka katika kaya maskini kupata ujuzi na kujikwamua kiuchumi kote Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news