Misingi ya sheria kuulinda uhuru wa vyombo vya habari ni tamanio la wote-Wakili Marenga

NA MWANDISHI WETU

UHURU wa vyombo vya habari unaozungumzwa sasa, bado haujawekewa misingi ya kisheria kuulinda.
Kuna sheria mbovu za habari ambazo hutumika tu pale mwandishi ama chombo cha habari kinapowindwa, jambo hili linaua tasnia ya habari nchini.

Ni kauli ya James Marenga, Wakili wa Kujitegenea akizungumza na Kituo cha Televisheni cha Azam katika Kipindi cha Morning Trump tarehe 2 Agosti 2022.

Wakili Marenga amesema, kwa sasa vyombo vya habari nchini vinaandika na hata kukukosoa lakini pale mwandishi ama chombo cha habari kinapowindwa, sheria zilizopo zinatumika.

“Kwa sasa vyombo vya habari vinaandika kwa uhuru, vinakosoa lakini kilichopo, kama mwandishi ama chombo cha habari kinawindwa, sheria hizi hizi zinatumika kuumiza chombo ama mwandishi.

“Mwandishi anaweza kufungwa kwa sheria zile zile ama chombo cha habari kinaweza kuondolewa sokoni kwa sheria hizo hizo, ndio maana tunasema uhuru wa habari lazima ulindwe kisheria,” amesema Wakili Marenga ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA-TAN).
Amesema, kuwepo kwa sheria hizi za habari, kwa kiwango kikubwa kumesababisha kushuka kwa habari za uchunguzi, na kwamba baadhi ya wanahabari wamepoteza vifaa vyao kutokana na polisi kuvitwaa kwa ajili ya upekuzi.

“Sheria hii imewapa mamlaka makubwa polisi, wanapoamua kukufuatilia na hata kuchukua vifaa vyako, wanaweza kufanya hivyo kwa sheria hii. Kwa nchi ya Ghana lazima polisi awe na kibali, lakini hapa kwetu hiyo haipo,” amesema.

Pia Wakili Marenga amesema, miongoni mwa mambo yanayokwaza tasnia ya habari ni pamoja na sheria kuelekeza usajili wa magazeti kila mwaka.

Amesema, kwa magazeti ingetosha kusajiliwa mara moja na sio kila mwaka kama inavyoelekezwa na sheria ya sasa.

“Unakuwa ni usumbufu na kupoteza pesa, yaani ukimaliza mwaka unaanza kukusanya documents (nakala) ambazo ulizipeleka awali unapeleka tena, tena unatakiwa kulipa. Hili jambo tunasema hapana, tunapaswa kusajili mara moja basi,” amesema.
Angela Akilimali, Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), amesema, uimara wa vyombo vya habari nchini utatokana na kuundwa kwa sheria rafiki na si zile zenye vitisho, kukandamiza na kunyanyapaa wanahabari.

Ameeleza kuwa, mchakato wa mabadiliko ya sheria za vyombo vya habari nchini, unalenga kujenga mazingira rafiki na bora kwa wanahabari katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Amesema, sheria zilizopo sasa zinakinzana na malengo ya ukuaji wa tasnia ya habari nchini hivyo kuwa chanzo cha kudumaza tasnia hiyo.

“Yapo mabadiliko mengi yaliyofanywa mwaka 2016 kwenye Sheria ya Habari yanayokinzana na kukua kwa tasnia hii, mfano huwezi kuunda Bodi ya Idhibati halafu serikali iisimamie bodi hiyo.

“Wanahabari kama taaluma nyingine, ina watu wenye weledi wa kutosha hivyo badala ya kuwa na vyombo vingi kama vilivyotajwa kwenye sheria hii (Bodi ya Idhibati, Mfuko wa Mafunzo na Baraza Huru la Vyombo vya Habari), tunaona tuwe na chombo kimoja tu ambacho ni Baraza Huru la Vyombo vya Habari ili kusimamia mambo yote ya wanahabari na tasnia kwa ujumla,” amesema Angela.

Amesema, kikwazo kingine kwenye tasnia ya habari ni sheria kulazimisha chombo cha habari hususani magazeti kuomba leseni kila mwaka na kwamba, jambo hilo limekuwa likisababisha usumbufu mkubwa.

“Hatuoni sababu kwa vyombo vya habari hususani magazeti kuwekewa utaratibu wa kukata leseni kila mwaka, kama ilivyokuwa awali kabla ya mabadiliko ya 2016 kwamba usajili ni mara moja, utaratibu huu unafaa kuendelea,” amesema Angela.

Amesema, tasnia ya habari inahitaji uwekezaji mkubwa na kwamba, kuweka mipaka ya uwekezaji kwa wageni kutoka nje kama inavyoelekeza sheria, kunaua tasnia hiyo.

“Kwenye hii sheria yapo mambo mengi magumu, lipo hili la kulazimisha mwekezaji kutoka nje awe na asilimia isiyozidi 49, lakini tunajiuliza mbona wawekezaji kwe nye mitandao ya simu wanawekeza kwa asilimia 100 tuna wao wana wateja zaidi ya milioni 10.

“Kwanini kwenye tasnia ya habari wazuiwe, hii tunasema hapana. Tunasema hivyo kwa kuwa uwekezaji kwenye habari unahitaji mtaji hivyo kama ilivyo kwenye uwekezaji mwingine, kwenye Habari akiwemo mwekezaji anayetaka kuwekeza kwa 100%, aruhusiwe,” amesema.

Wallace Maugo, Mhariri wa Gazeti la The Guardians amesema, wanahabari wanapaswa kuwa pamoja katika kuhakikisha sheria hizi zinazominya uhuru wa habarui na wanahabari zinabadilishwa.

Amesema, mchakato wa mabadiliko haya umeanza wakati muafaka kwa kuwa, rais aliyepo madarakani (Rais Samia Suluhu Hassan) ni msikivu katika mambo mbalimbali.

“Tunapaswa kuwa pamoja wanahabari wote, lakini tuna bahati nzuri maana katika mchakato huu rais ni msikivu kabisa na anaonekana kuwa na dhamira ya kweli,” amesema Maugo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news