Mkurugenzi mpya wa UTPC Kenneth Simbaya akabidhiwa ofisi rasmi

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania Deogratius Nsokolo amemkabidhi rasmi ofisi Bw. Kenneth Simbaya ambaye ni Mkurugenzi mpya wa UTPC, Bw. Simbaya anachukua nafasi ya Bw. Abubakar Karsan ambaye amemaliza muda wake.
Makabidhiano hayo yamefanyika Agosti 1,2022 katika ofisi za UTPC zilizopo Isamilo Jijini Mwanza ambapo Rais Nsokolo amesema UTPC inamatarajio makubwa kutoka kwa Bw. Simbaya na kwamba uzoefu wake kwenye kazi utasaidia kuendeleza kazi nzuri iliyoachwa na mtangulizi wake na kuipeleka taasisi mbali zaidi.

Pamoja na mambo mengine Rais Nsokolo ametoa nasaha zake kwa mkurugenzi mpya, huku akigusia zaidi kuendeleza ushirikiano kati ya UTPC na wadau mbalimbali lakini pia kutumia fursa ya uwepo wa mkurugenzi aliyemaliza muda wake katika kubadilishana maarifa ya kiuongozi.

Pia amemtaka Bw. Simbaya kushirikiana na wafanyakazi wa UTPC, Bodi ya Wakurugenzi pamoja na viongozi wa Klabu za waandishi wa habari katika utendaji wa kazi kwani anaamini ushirikishwaji huleta tija zaidi kwa maendeleo ya taasisi na kwamba taasisi haiwezi kuendeshwa na mawazo ya mtu mmoja.

Aidha amesisitiza kuhusu uadilifu na ubunifu katika utendaji wake wa kazi na kuimarisha ushirikiano na wafadhili ikiwemo kutafuta fursa mpya za kupata fedha. Hata hivyo alimdokeza kuhusu uwepo wa changamoto ndogondogo zilizopo katika klabu za waandishi wa habari licha ya jitihada zilizofanyika kutatua changamoto hizo.
"Uhai wa UTPC unategemea uwepo wa klabu za waandishi wa habari hivyo ni lazima tuhakikishe tunashirikiana kuzisimamia na kuzijengea uwezo klabu zetu'' amesema Rais Nsokolo

Naye Mkurugenzi anayemaliza muda wake ndugu Abubakar Karsan ameeleza changamoto iliyokuwepo wakati anakabidhiwa nafasi ya ukurugenzi na kwamba hapakuwa na nyaraka zozote za makabidhiano hali iliyompa wakati mgumu katika kuifufua na kuiendeleza taasisi hiyo mpaka kuifikisha hapa ilipo leo.

"Nilikabidhiwa ukurugenzi hapa bila kua na nyaraka zozote, niliambiwa chukua kijiti nenda ukafufue taasisi" Karsan

Hata hivyo Bw. Karsan ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa mkurugenzi mpya kwa kipindi cha muda wa miezi mitatu ili kubadilishana uzoefu wa kiutendaji na ndugu Kenneth Simbaya.

Kwa upande wake Bw. Kenneth Simbaya amesema nafasi ya ukurugenzi ni nafasi ambayo anaweza kupewa mtu yeyote hivyo ameahidi kuhakikisha anataguliza mbele maslahi ya waandishi wa habari na klabu zake na yale yote mazuri yatabaki kuwa mazuri kwa maslahi ya waandishi wa habari Tanzania.

Pia ameahidi kushirikiana na wafanyakazi pamoja na wadau wa UTPC katika kuhakikisha taasisi inasonga mbele "Maamuzi binafsi huyumbisha mwelekeo wa taasisi, hivyo niwahakikishe Bodi ya Wakurugenzi kwamba kila kitu kitaenda sawa kulingana taratibu zilizowekwa na kwa mujibu wa miongozo ya UTPC," amesema Simbaya.

Aidha ameongeza kuwa kesho ya UTPC inategemea maamuzi mazuri yatakayofanywa leo, hivyo ili kuacha alama ni lazima kufanya kazi kwa ufanisi na weledi wa hali ya juu na kwa maslahi ya waandishi wa habari nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news