Mtanzania atunukiwa Tuzo ya Marianne Initiative ya Rais wa Ufaransa

NA FRESHA KINASA

MTANZANIA Rhobi Samwelly amekuwa miongoni mwa washindi 15 walioshinda Tuzo ya Marianne Initiative ambayo ilianzishwa mwaka jana na Serikali ya Ufaransa chini ya Rais Emmanuel Macron kwa lengo la kutambua wale wanaopigania haki za binadamu hasa wanawake katika nchi zao.

Rhobi Samwelly ni Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania linalojishughulisha na mapambano ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na kutetea haki za binadamu lenye makao makuu yake Mugumu Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara.

Ambapo tuzo hiyo inahusisha programu ya miezi sita hadi mwaka mmoja na washindi wa tuzo wanashiriki katika mikutano mbalimbali na kupata fursa ya kukutana na mashirika mbalimbali na mashirika yanayosaidia kujua yanavyofanya kazi na hivyo kutengeneza mtandao mkubwa wa kuendeleza shughuli zao wanazofanya sambamba na kupewa mafunzo ya idara mbalimbali ya Serikali ya Ufaransa inavyofanya kazi.

Akizungumza katika mahojiano na Radio France International Kiswahili katika Makala ya 'Jua haki zako' ambayo huangazia haki za binadamu inayoendeshwa na Mtangazaji Benson Wakoli, Rhobi amesema,

"Nilichaguliwa kuwa miongoni mwa wanawake 15 kutoka ulimwenguni kupokea tuzo ya 'Marianne Initiative' kutoka kwa Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron. Hii ni kutokana na shughuli zangu kupitia shirika la kupambana na ukatili wa kijinsia na mila na desturi ambazo zinakandamiza wasichana na wanawake kwa kutoa elimu katika jamii na kutetea haki zao,"amesema Rhobi Samwelly.

"Kutoa hifadhi kwa wasichana ambao hukimbia kukeketwa na aina nyingine za ukatili wa kijinsia na kutoa huduma ya Nyumba Salama. Na pia kwa kushirikiana na Polisi Dawati la Jinsia na Watoto na Maafisa wa Maendeleo ya Jamii tumekuwa tukijenga mahusiano baina ya watoto wa kike na Wazazi wao baada ya ukeketaji kuisha." amesema.

"Najisikia fahari Sana, tuzo hii imenipa nafasi ya kujiona sipo peke yangu katika kazi hii. Kumbe pia unapofanya kazi si wewe mwenyewe unajiona kumbe Kuna watu wengine mbali wanakuona katika harakati unazozifanya mradi uamini kwamba ninachokifanya ni kitu chema na ni kwa ajili ya kuwasaidia watu wengine kama ninavyofanya kusaidia watoto wa kike pamoja na wanawake," amesema Rhobi.
"Tuzo hii imenipa nguvu, imenipa faraja na kunifungua ufahamu, nipo hapa Ufaransa ni miezi sita inakaribia sasa niko imara zaidi nimeongeza ufahamu kwa jinsi gani ya kupambana na kwa kiwango zaidi ili kuweza kusaidia wanawake na wasichana nchini Tanzania.

"Lakini pia tuzo hizi zinamaana kubwa sana kwangu na si kwangu tu bali kwa wanawake wote ambao wanatetea haki za wanawake na watoto wa kike, lakini hata ambao bado wanashikilia mila na desturi wakiona hivi wanapata funzo,ni uhamasishaji mkubwa sana ndani ya jamii nchini Tanzania na nje ya Tanzania,"amesema Rhobi.

Aidha, Rhobi amesema kuwa wazazi na walezi wanajukumu la kusikiliza sauti za watoto wa kike ambao wamekuwa wakipaza sauti zao wakikataa kukeketwa na kupelekea wakimbie kutoka katika familia zao kupata hifadhi (Nyumba Salama) kutokanata elimu ya madhara ya vitendo vya ukeketaji wakiwa shuleni akitolea mfano wa Wilaya ya Serengeti ambayo wasichana hawataki kukeketwa baada ya kupata elimu thabiti ya madhara yatokanayo na ukeketaji.

Kwa upande wake Balozi wa Mpango huo, Balozi Delphine Borione akizungumzia mpango huo kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa amesema kuwa, mpango huo ni wa watu wanaotetea haki za binadamu katika nyanja tatu, moja kuwatia motisha wanaharakati wanaopigania haki za binadamu katika mataifa husika na hapo kuna mipango miwili ikiwemo kuwapa uwezo zaidi na nguvu za mawasiliano.

"'Pili, ni kuwaalika baadhi ya wale wanaopigania haki za binadamu kuja Ufaransa kuwapa mafunzo ya ziada na kuwakutanisha na wenzao na mwaka huu tunao wanaharakati 15 kutoka mataifa 13.

"Na tatu, kuhakikisha kuna ushirikiano kati ya wanaopigania haki za binadamu na wakimbizi wanaoishi Ufaransa. Mpango huu unafadhiliwa na Serikali ya Ufaransa. Na mpango huo unahusisha Dunia japo ni mataifa machache yaliyoteuliwa na baadhi yao kutoka Latine America, Syria Sudan, Iraq na Tanzania," amesema Balozi Borione.

"Kuwekeza katika wanawake na usawa wa kijinsia hausaidii tu wanawake bali pia jamii nzima maana ukimpa mwanamke uwezo umeipa jamii.nzima tunaamini msingi wa haki za binadamu ni usawa kwa wote bila kubagua ni mtu wa maana sana.Ufaransa inajihusisha sana kuwapa uwezo na usawa wa kijinsia wanawake,"amesema Balozi Borione.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news