NHIF:Tunatamani kila Mtanzania awe na bima ya afya

NA GODFREY NNKO

ASILIMIA 85 ya Watanzania wanalazimika kutumia bajeti zao za mfukoni kugharamia bajeti ya afya, jambo ambalo linatajwa kuwa ni changamoto licha ya juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali za kuhakikisha huduma za bima za afya zinapatikana kila mahali nchini.

Hayo yamebainishwa leo Agosti 11, 2022 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Bw.Bernard Konga katika kikao kazi na waandishi wa habari akielezea mfuko umetoka wapi,wako wapi na wanaelekea wapi kwa sasa.

"Kama nchi mpaka sasa tuna wastani wa asilimia 15 ya Watanzania wanaohudumiwa kwenye mfumo wa bima ya afya asilimia nane inachukuliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), asilimia sita inachukuliwa na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na asilimia moja ni bima binafsi,"amesema Bw. Konga.

"Kimsingi bado tunaona kama nchi hatujafika tunakotaka kufika kwa sababu lengo tunatamani kila Mtanzania awe na bima ya afya sasa hivi ni asilimia 15 kwenye mfumo kwa maana asilimia 85 leo hii wanapata matibabu kupitia bajeti kutoka mfukoni.

"Kama mfuko wa Serikali tunaona bado tuna kazi kubwa ya kufanya na tuna mipango ambayo inafanyika ndani ya Serikali kuona namna gani hili linakwenda.Pia kama mfuko tunaendelea kutoa elimu ya bima ya afya kwa wananchi kuelezea manufaa na faida ya kuwa na bima ya afya,"amesema Bw. Konga.

Konga amefafanua kuwa,hadi kufikia Juni,2022 mfuko huo unahudumia wanachama milioni 4,821,233 ikilinganishwa na wanachama milioni 4,550,000 mwezi Juni, 2021 sawa na asilimia nane ya Watanzania wanaohudumiwa na mfuko huo.

"Mpaka kufikia mwezi Juni, 2022 mfuko unahudumia takribani wanachama milioni 4, 821, 233 ikilinganisha na wanachama milioni 4,550,000 kipindi kama hicho mwezi Juni 2021. Kwa hiyo wanachama milioni nne na laki nane ni wanachama wachangiaji pamoja na wale wanufaika.

"Hii inafanya asilimia nane ya Watanzania wanaohudumiwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya. Tukisema Bima ya Afya nchini mfumo una maeneo makubwa matatu,moja ni Mfumo wa Taifa wa Bima ya Afya, mbili Mfuko wa Afya ya Jamii na tatu bima binafsi.

Bw.Konga amesema,katika hao milioni nne laki nane ambao ni asilimia 100 ya wale ambao wanawahudumia takribani asilimia 66 ni watumishi wa umma.

"Mtakumbuka mfuko ulivyoanza mwaka 2001, lengo lilikuwa ni watumishi wa umma kuingia kwa lazima na hao wote wameingia kwa lazima, na asilimia iliyobaki imegawanyika kwenye makundi mbalimbali.

"Kama sekta binafsi asilimia 16.9, wanafunzi wote sasa hivi wanaingia wote wa vyuo kwa lazima asilimia 7.15, watoto asilimia 4.2 yapo makundi mbalimbali, lakini asilimia kubwa inabebwa na watumishi wa umma,"amesema.

"Nitumie fursa hii kusema kwamba kupitia kundi hili Serikali imeona namna pekee ya kuweza kufanikisha bima ya afya sasa ni kujifunza kupitia kundi hili la watumishi wa umma, kwa sababu wanaingia kwa lazima inamaana wote tunaingia kwa pamoja inatusaidia kwamba hatusubiri mtu akiwa anaumwa ndio ajiunge.

"Mtumishi wa umma akishapewa barua yake ya ajira mshahara wake wa kwanza tayari kuna makato ya NHIF na hilo ndilo kundi ambalo limesaidia kuuweka mfumo hai na kuwa na nguvu mara kwa mara, leo kwa sababu Bima ya Afya inatutaka kuingia kwenye utaratibu kabla ya kuugua bahati mbaya wengi wanasubiri wakishaugua ndipo wajiunge kwenye Bima ya Afya sasa wale wanarudisha nyuma dhana nzima ya Bima ya Afya.

"Kupitia kundi hili mfuko umeendelea kuwa endelevu sana, Serikali imekuwa ikihakikisha hawa na wategemezi wao michango yao inakwenda kwa wakati kwa takwimu za haraka haraka tu tangu mwaka 2016 hatujawahi kuwa na deni lolote kwa Serikali.

"Serikali imekuwa ikiwasilisha kwa wakati. Lakini makundi mengine bahati nzuri yamekuwa yakichangia kabla ya huduma,changamoto ni moja tu yamekuwa yakiingia kwa uhiari na katika uhiari huo wengi unakuta tayari ana mwelekeo wa kuugua, kitu ambacho kinarudisha nyuma malengo ya kuanzishwa kwa mfuko.

"Kupitia takwimu hii Serikali inaandaa mpango kabambe kwa kuwa na kundi kubwa ambalo linaingia katika utaratibu huu ambao watumishi wa umma wanakuwa wakiingia nao,"amesema Bw. Konga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news